Viongozi ulimwenguni walaani shambulio dhidi ya Trump – DW – 16.09.2024

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amelaani vurugu za kisiasa kufuatia jaribio la kumuua Donald Trump ambalo linadaiwa kufanywa na mshukiwa aliyewahi kusafiri hadi Ukraine kuunga mkono juhudi za vita. Akitoa salamu za pole kuhusu tukio hilo, Zelensky amesema ni “jambo jema kwamba mshukiwa wa tukio hilo amekamatwa haraka” na kutilia mkazo kwamba hiyo ndio kanuni kubwa ambapo utawala wa sheria ni muhimu na vurugu za kisiasa hazina nafasi mahali popote ulimwenguni.

Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer ni miongoni pia mwa viongozi walioelezea “wasiwasi mkubwa” kuhusu matukio kama hayo yanayomlenga Trump. “Nafikiri ni muhimu kwamba sote tuwe wazi kwamba vurugu hazina nafasi katika michakato yote ya kisiasa”. Starmer ameyasema hayo mjini Rome, Italia ambako amekutana na kufanya mazungumzo na kiongozi mwenzake wa Italia Giorgia Meloni.

Soma: FBI yasema Trump alilengwa katika jaribio la mauaji

“Nilikuwa na wasiwasi sana na habari kuhusu tukio hili, linaloonekana kama jaribio la mauaji. Nina wasiwasi sana kuhusu hilo. Wacha uchunguzi uchukue nafasi yake lakini kwa uwazi kabisa, nisema ghasia hazina nafasi katika majadiliano ya kisiasa hata kidogo, popote.”

Eneo la tukio karibu na uwanja wa gofu wa Trump Florida
Eneo la tukio karibu na uwanja wa gofu wa Trump FloridaPicha: CHANDAN KHANNA/AFP via Getty Images

Wakati salamu za pole zikitolewa, Rais Joe Biden amesema idara ya usalama inahitaji usaidizi zaidi na kuongeza kwamba hadi kufikia sasa hajapokea ripoti kamili kuhusu tukio hilo la Jumapili lakini anashukuru kwamba kiongozi huyo yuko salama.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini Marekani mshukiwa wa jaribio la mauajid dhidi ya Trump amefahamika kuwa Ryan Wesley Routhambaye amewahi kuonekana viunga vya mjini Kiev mwaka 2022 akiunga mkono Ukraine katika mapambano yake dhidi ya Urusi.

Kuhusishwa kwa mshukiwa huyo na Ukraine kumeiibua Ikulu ya Urusi Kremlin iliyoinyesha kidole Marekani. Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov alisema kwamba ni Marekani na idara zake za usalama ndio zinapaswa kutafakari. Ameongeza kuwa “kwa namna yoyote, kucheza na moto kuna madhara yake”.

Soma: Trump yuko salama baada ya risasi kufyatuliwa kwenye uwanja wa mpira wa gofu

Ama kwa upande mwingine maafisa wa Ukraine, wamekanusha uhusiano wowote na mshukiwa huyo na kuituhumu Moscow kwa kutaka kueneza propaganda. Afisa mmoja mwandamizi wa Ukraine aliyezungumza na shirika la habari la AFP kwa sharti la kutotajwa majina amesema “mshukiwa huyo hakuwahi kutumika nchini humo na wala hana uhusiano wowote na nchi hiyo. Aliingia kama mtu wa kawaida ambaye alikuwa mfuasi kama walivyo watu wengine wengi”.

Jeshi la kimataifa la Ukraine linalojumuisha wafanyakazi wa kujitolea wa kigeni pia limekanusha uhusiano wowote, likisema mshukiwa “hajawahi kuwa na uhusiano wowote na kitengo hicho”.

 

Related Posts