Vipigo mfululizo vyawashtua Namungo | Mwanaspoti

VIPIGO vitatu mfululizo ambavyo imepokea Namungo msimu huu katika Ligi Kuu Bara, vimewafanya wachezaji wa timu hiyo kukaa chini na kutafakari jambo.

Namungo ambayo haina pointi katika mechi tatu ilizocheza kutokana na kupoteza zote huku ikifunga bao moja na kuruhusu matano, leo Jumanne itakuwa na kazi ya kujiuliza mbele ya Coastal Union.

Mchezo huo wa kesho ambao utachezwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, unazikutanisha timu zote ambazo hazijapata ushindi msimu huu kwenye ligi ingawa Coastal wana cha kutambia kutokana na pointi moja waliyonayo katika mechi mbili walizocheza.

Mechi tatu ambazo Namungo imecheza, mbili imefungwa nyumbani matokeo yakiwa; Namungo 1-2 Tabora United na Namungo 0-2 Fountain Gates, kisha ugenini Dodoma Jiji 1-0 Namungo.

Kiraka wa Namungo, Erasto Nyoni alikiri kuumizwa na matokeo hayo, lakini wana imani wakishinda mechi mbali mfululizo zijazo ikiwemo ya leo dhidi ya Coastal Union kisha Tanzania Prisons, zitawasaidia kuwapa morali ya juu ya kupambana zaidi.

“Ni upepo mbaya wa matokeo maana tunacheza vizuri ila changamoto ni kupata ushindi, tunajifunza tumekwama wapi michezo iliyopita ili tuwe bora zaidi mechi zijazo,” alisema.

Kipa wa timu hiyo, Beno Kakolanya alisema: “Tumeanza na mwanzo mgumu wa kupoteza mechi kwa mfululizo, pamoja na hilo tuna matumaini makubwa ya kushinda mechi zinazokuja mbele yetu, hivyo tunawaomba mashabiki wasikate tamaa bado tuna safari ndefu.

Related Posts