Wanafunzi masomo ya akili mnemba waula ufadhili asilimia 100

Unguja. Wanafunzi watakaosemea sayansi ya data na akili mnemba katika Taasisi ya Teknolojia ya India Madras, Kampasi ya Zanzibar (IITMZ) kwa mwaka wa masomo 2024/2025 watapata ufadhili wa masomo kwa asilimia 100.

Hatua hiyo ni kuongeza ushawishi na kupata wataalamu wengi katika sekta hiyo, ikizingatiwa kwa sasa dunia inaelekea katika matumizi makubwa ya akili mnemba (AI).

Ufadhili huo unajumuisha wanafunzi sita kutoka Tanzania Bara na watatu kutoka Zanzibar, mmoja akitokea nchini Kenya ambao ni wa ngazi wa shahada ya kwanza watakaosoma fani hizo kwa miaka minne.

Taarifa ya mkurugenzi wa taasisi hiyo, Profesa Preeti Aghalayam  iliyotolewa jana Jumapili, Septemba 15, 2024 imeeleza ufadhili huo unatolewa na Airtel Africa Foundation.

“Ufadhili huo unalenga kuwafadhili wanafunzi 10 malipo yao ya ada kwa kila mmoja ya Dola 12,000 za Marekani kwa mwaka, ambayo ni sawa na Sh33 milioni kwa kipindi chote cha masomo yao katika kampasi hii,” amesema.

Mbali na ufadhili huo wa ada, taarifa hiyo imeeleza ufadhili zaidi kwa kulipia Dola 500 za Marekani, sawa na Sh1.375 milioni, zikiwa ni miongoni mwa gharama za wanafunzi katika huduma zao za chakula na makazi ndani ya kampasi hiyo.

Profesa Preeti ametaja miongoni mwa vigezo vya ufadhili huo kuwa ni lazima mwanafunzi ajenge na kuendeleza nidhamu katika kipindi chote cha masomo, pia na kulinda ufaulu wake kwa kiwango kisichopungua GPA 7.5 kwa kila mwaka.

Mkuu wa kitengo cha Uhusiano IITMZ, Mwatima Rashid Issa amesema wanafunzi wanaotegemea kujiunga kwa mwaka huu ni 70, kati ya hao 30 ni wanaosoma shahada ya pili na 40 shahada ya kwanza.

 “Huu mpango ni mzuri, wapo vijana wengi wanapenda kusomea taaluma hii, lakini uwezo unakuwa mdogo na gharama ni kubwa, kwa hiyo tunapongeza na sasa ni fursa kwa vijana,” amesema Mussa Juma Iddi, mwanafunzi kutoka Chuo cha Taifa Zanzibar (Suza).

Ametoa wito kwa wazazi kuwahamasisha watoto wao kusoma masomo ya sayansi, hivyo wanapaswa kuchangamkia fursa hiyo na hawana sababu ya kuwa na hofu, kwani misaada inatolewa ili watoto wasome.

Taasisi ya IITMZ kampasi ya Zanzibar ilifunguliwa rasmi mwaka jana, lengo ni kuongeza wataalamu katika sayansi. Wanafunzi wanaoingia hapo lazima wafaulu somo la fizikia, kemia na hesabu kwa kuwa na uwezo wa kuchakata data (data science and artificial intelligence).

Related Posts