WANAKIJIJI WA KATA YA UCHAMA WAELEZWA KUWA MAENDELEO NI HATUA, SERIKALI IMEDHAMIRIA KUWALETEA NEEMA ZAIDI


Vijiji vya Undomo na Mbogwe vilivyopo katika Kata ya Uchama, Wilaya ya Nzega vimeahidiwa kujengewa Kituo cha Zana za Kilimo na kupatiwa trekta tano ili kusaidia shughuli za kilimo. Vijiji hivyo vipo katika Kata ya Uchama ina Vijiji 59 na Vitongoji 356.
Hayo yamesemwa na Mhe. Hussein Bashe (Mb), Waziri wa Kilimo wakati wa ziara yake tarehe 16 Septemba 2024 wilayani humo. “Tumejenga shule za sekondari kila kata; ujenzi wa zahanati mbalimbali na barabara; kusogeza huduma za Maafisa Ugani; na mengine. Niawatie moyo kuwa tulikotoka ni mbali na tutaendelea kuboresha huduma na kuleta maendeleo,” amesema Waziri Bashe.
Aidha, ameielekeza Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) kusambaza magunia 20 ya mahindi ili watoto wa shule za msingi wapate uji. Kuhusu matumizi ya mbegu za ASA, amehamasisha wakulima kutumia mbegu hizo ili msimu ujao apate taarifa kuhusu waliolimiwa kwa trekta na kupanda kwa kutumia mbegu bora za ASA ili kuona tija ya mavuno iliyopatikana.
Ameongeza kuwa mbegu aina ya T-115 yenye mche wenye mahindi mawili ndiyo mbegu ambayo wakulima watauziwa na ASA.
Katika tukio tofauti, Waziri Bashe pia amechangia shilingi milioni kumi kuanza ujenzi jengo la wodi ya kinamama kwa ajili ya kujifungulia. Fedha iliyosalia ya ujenzi ameomba Halmashauri isaidie ukamilishaji wa wodi hiyo.
Kuhusu zao la Pamba, amehamasisha wakulima wajaribu kutenga maeneo yao ili walime zao la Pamba, huku a kuwaeleza kuwa watapatiwa mbegu bure na dawa za kupulizia. Aidha, ameeleza kuwa kutakuwa na ujenzi wa kıwanda cha kusafisha mbegu ili kusogeza huduma kwa wakulima.

Related Posts