Watetezi haki za binadamu wahimiza ulinzi kwa watoto

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) kwa kushirikiana mashirika wanachama ambao ni watetezi haki za watoto umemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuchukua hatua dhidi ya vitendo vya ukatili kwa watoto kwa masilahi ya taifa la leo na la kesho.

Septemba 14,2024 watetezi hao wameungana katika matembezi ya amani ya kuhimiza ulinzi wa haki za watoto wa Tanzania yenye kaulimbiu isemayo ‘Hakuna ukimya tena tunadai ulinzi wa watoto wetu’.

Huo ni mwendelezo wa harakati ambazo THRDC imekuwa ikizifanya kwa kuungana na wanachama wake kutetea haki za watoto nchini ambapo hatua hiyo ya matembezi ya amani imechukuliwa na wanachama hao wa haki za watoto kama mojawapo ya njia ya kuonyesha hali mbaya ya ukatili wa watoto iliyopo katika jamii.

Wanachama hao wameonyesha kutoridhishwa na matukio ambayo yamekuwa yakitokea kwa siku za karibuni kama mauaji, ulawiti, ubakaji, utekaji na utumikishwaji.

Takwimu zinaonesha kuna ongezeko la ukatili kwa watoto ambapo Ripoti za Takwimu za Msingi za mwaka 2023 zinaonyesha matukio ya ubakaji na ulawiti, ikiwa ulawiti yameongezeka kutoka kesi 1,205 mwaka 2020 hadi 2,488 mwaka 2023, sawa na ongezeko la asilimia 57.

Pia ubakaji umeongezeka kwa kasi kutoka matukio 6,827 mwaka 2022 hadi 8,691 mwaka 2023, hali inayodhihirisha usalama wa watoto kuwa shakani.

“Sisi kama Mtandao wa watetezi wa Haki za Binadamu kwa kuungana na mashirika wanachama wa haki za watoto tunalaani vikali vitendo vya kubakwa, kulawitiwa,
kutekwa, kupotea, kuibiwa na mauaji ya watoto vinavyoripotiwa katika maeneo mbalimbali nchini.

“Vitendo hivi vinadidimiza hali ya usalama wa watoto nchini na pia ni kinyume na haki za binadamu ambazo Tanzania imeridhia kuzitekeleza katika mikataba ya Kikanda na Kimataifa ikiwemo mkataba wa kimataifa
wa haki ya mtoto na mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa mtoto,” wamesema.

Wamesema mikataba hiyo imetoa wajibu kwa nchi wanachama kuhakikisha inaweka mifumo itakayotoa ulinzi stahiki kwa mtoto bila ubaguzi na kuhakikisha watoto wanafurahia haki zao kama zilivyoainishwa.

Pia wanachama hao wametoa wito na kuhimiza serikali kuchukulia kwa uzito matembezi hayo na matamko mbalimbali ambayo yamekuwa yakitolewa na THRDC na wadau wengine.

Related Posts