WAZIRI MKUU AHIMIZA USIMAMIZI WA MAADILI MEMA KWA JAMII.

*Asema lengo ni kuepusha uovu na kuchochea maendeleo

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ametoa wito kwa viongozi wa dini na Watanzania kwa ujumla wahakikishe wanasimamia na kuimarisha maadili mema kwa jamii ili kuepuka maovu na kuleta maendeleo endelevu kwa Watanzania.

“Nitumie fursa hii kuendelea kutoa rai kwa wananchi, wazazi na viongozi wa dini kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika malezi ya watoto wetu katika ngazi zote kwa kuzingatia maadili na tamaduni ya Taifa letu. Ni wajibu wetu kama wananchi”

Amesema hayo leo (Jumatatu, Septemba 16, 2024) alipomwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Baraza la Maulid Kitaifa lililofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Nyankumbu, Mkoani Geita.

Amesema kuwa viongozi wa dini wana jukumu la kutoa mwongozo na malezi ya kiroho kwa waumini kwa kuwa wana nguvu kubwa ya kuhamasisha maadili na tabia nzuri.

“Wazazi, ninyi mna jukumu la msingi katika kulea watoto wenu kuanzia katika ngazi ya familia ili kujenga tabia njema, na tukifanya hivyo matendo na hovyo hayatakuwepo, lazima tuwe macho katika matendo haya ambayo yanaweza kuleta hofu kwa jamii yetu”

Sambamba na msisitizo katika maadili, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa kila mmoja ashiriki katika kulinda Taifa kwa kutambua matendo yote yanayoashiria uvunjifu wa amani ili nchi iendelee kuwa imara “suala la ulinzi na usalama ni letu sote watanzania, ndivyo tulivyofanya tangu Tanzania ipate uhuru”

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amewataka waumini wa dini ya kiislam kutumia sherehe za Maulid kwa kuonesha kwa vitendo namna ya kuishi kwa upendo, heshima, maadili, huruma na uadilifu.

“Kwa kuenzi maisha ya Mtume Muhammad (S.A.W), tutumie sherehe za Maulid kuwa chanzo cha mabadiliko chanya katika maisha ya waumini. Sote tutumie nafasi hii kuhamasika na kujitahidi kuishi kwa maadili ya Mtume, ambayo yanajumuisha tabia nzuri, uadilifu, na huruma”

Kwa Upande wake, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Dkt. Abubakary Zubeir Ally amewataka waislam na Watanzania kushikiri katika ujenzi wa uchumi wa nchi ikiwemo ujenzi wa miundombinu mbalimbali katika sekta za elimu na afya. “Waislam tujenge na tuulinde uchumi wetu, tusomeshe watoto ndani na nje ya nchi”

Pia ametoa wito kwa Watanzania kuwa wazalendo na kulinda nchi yao “kufanya hivyo ni wajibu wa kila mmoja, tuichunge na tuipende nchi yetu pia ni muhimu kwa kila mtanzania kushiriki katika kuzuia mmomonyoko wa maadili”

Naye Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Alhaj Nuhu Jabiri Mruma ametoa wito kwa Waislam

na watanzania kwa ujumla kujitokeza kushiriki katika uboreshaji wa daftari la kudumu la Wapiga Kura pamoja na kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Aidha ametoa wito kwa vyombo vinavyosimamia uchaguzi kutenda haki na kufuata taratibu zote za uchaguzi “Vyama vya siasa pia epukeni rushwa kwani itasababisha kutokuwepo kwa haki”

Related Posts