Dar es Salaam. Kutokana na kuongezeka kwa mwamko wa abiria kutumia usafiri wa treni ya umeme (SGR), wamiliki wa mabasi nchini Tanzania wamekuja na mikakati mipya kuhakikisha wanaendelea kuwa sokoni bila biashara zao kuathirika.
Tangu kuanza kwa usafiri huo, wamiliki wa mabasi wamekuwa wakilalamikia changamoto katika soko na tayari wengine wameanzisha safari mpya katika njia zisizo na reli ya kisasa.
Kampuni kama Kimbinyiko, BM Coach, Abood na Shabiby tayari zimeanza kupanua huduma katika maeneo mapya, ikiwemo Sumbawanga, Bukoba, Musoma na hata nchi jirani ya Kenya.
Hatua hizi zinalenga kurejesha sehemu ya soko na kudumisha shughuli zao za usafirishaji, licha ya mabadiliko makubwa katika sekta ya usafiri.
SGR, iliyoanza kutoa huduma hivi karibuni, imevutia wananchi zaidi, ikiwa na zaidi ya abiria 7,000 wanaosafiri kwa siku kati ya Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma.
Ufanisi na mvuto wa mtandao huo wa reli umesababisha kupungua kwa abiria wanaotumia usafiri wa mabasi kwa njia ya barabara.
Hata hivyo, wamiliki wa mabasi wamesema, licha ya treni kuchukua soko katika njia zilizozoeleka, haitakuwa shida kwao kwa kuwa Tanzania ni kubwa.
Tanzania ina eneo la kilomita za mraba 945,087 ikiwa ni kubwa zaidi kuliko Kenya, Uganda, Burundi na Rwanda kwa pamoja.
Eneo la nchi hizo nne lina ukubwa wa kilomita za mraba 877,852, huku Kenya na Uganda zikichukua sehemu kubwa zaidi ya kilomita za mraba 582,646 na 241,038, mtawalia.
Kuwepo kwa mipaka na nchi saba, ambapo nchi mbili kati ya hizo hazina bahari na zinategemea Bandari za Tanzania kwa biashara za kimataifa, kunatoa fursa kwa wamiliki wa mabasi kutumia fursa hiyo.
Agosti mosi, 2024, akizindua treni ya SGR, Rais Samia Suluhu Hassan alisema licha ya athari zilizoanza kujitokeza kwa wamiliki wa mabasi na malori, bado Tanzania ina fursa nyingi za wasafirishaji hao kunufaika.
Pamoja na athari hizo, Rais Samia alisema bado wasafirishaji hao wana fursa ya kunufaika, hasa katika njia nyingine ambazo mradi huo haujafika.
Hata hivyo, alisema kupungua kwa mabasi barabarani inaweza kuwa athari mbaya kwa wafanyabiashara, lakini nzuri kwa Serikali kwa kuwa itapunguza ajali.
“Hasara moja ambayo imeanza kuonekana ni kupungua kwa mabasi barabarani, kwa wafanyabiashara ni mbaya lakini kwa nchi ni nzuri kwa sababu inapunguza ajali pia na sasa usafiri barabarani unadhibitiwa vizuri,” alisema.
Hata hivyo, alieleza bado wasafirishaji hao hawataathirika kwa kuwa kuna njia nyingine treni hiyo haijafika na hivyo wana nafasi ya kupeleka mabasi huko.
Akizungumza na The Citizen, Mkurugenzi wa Kampuni ya Mabasi ya Kimbinyiko, Ferdinand Mabumo amesema tayari kampuni yake ilishaanzisha njia nne mpya, ili kuendana na soko linalobadilika.
“Tumepunguza safari kati ya Dar es Salaam na Dodoma kutoka safari 10 hadi nne kwa siku,” amesema.
Njia mpya sasa ni Dodoma-Arusha, Arusha-Mbeya, Dodoma-Njombe na Moshi-Mbeya. Mipango ya baadaye ya kampuni hiyo ni kupanua huduma hadi Nairobi, nchini Kenya.
Meneja wa Kampuni ya Mabasi ya Shabiby, Edward Magawa amesisitiza umuhimu wa kupanua maeneo ya huduma.
“Tanzania ni kubwa ingawa bado kuna mahitaji ya safari kati ya Dar es Salaam na Dodoma, tumejikita katika njia mpya kama vile Dodoma-Sumbawanga, Dodoma-Bukoba na Dodoma-Musoma,” amesema.
Shabiby pia imeagiza mabasi mapya yanayotarajiwa kufika katikati ya Oktoba 2024, ili kutumika katika njia hizo mpya.
BM Coach imeanzisha huduma za kuvuka mipaka, ikizindua njia mpya kati ya Dar es Salaam na Nairobi, tangu Septemba 4, 2024.
“Kwa sasa tupo kwenye majaribio na tuna mipango ya kupanua hadi Kampala (Uganga) na Rwanda,” amesema Meneja wa Operesheni wa BM Coach, Gabriel Makundi.
Kampuni hiyo itaendesha safari nne kwa siku kwenye njia hiyo na inafikiria kuongeza njia ya Dar es Salaam-Tunduma hivi karibuni.
Kabla ya kuanza kwa SGR, BM Coach ilikuwa ikiendesha hadi mabasi 22 kwa siku kwenye njia ya Dar es Salaam-Morogoro na mabasi 10 kati ya Dar es Salaam na Dodoma.
Hata hivyo, kutokana na kuongezeka kwa usafiri wa reli, sasa ni mabasi sita tu yanayofanya safari kati ya Dar es Salaam na Morogoro na manne kati ya Dar es Salaam na Dodoma.
Licha ya changamoto zinazotokana na SGR, wamiliki wa mabasi nchini wanatumia uwezo wao wa kubadilika na kupanua njia zao, ili kuhakikisha wanaendelea kuwa sehemu muhimu ya mtandao wa usafiri nchini.
Wamiliki wa mabasi wamesema wako tayari kuwekeza kwenye mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT), endapo maboresho yatafanywa katika ukusanyaji wa nauli na mikataba ya uendeshaji.
Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa) kinahimiza ushiriki zaidi katika mfumo wa BRT, ili kuendeleza biashara zao huku mtandao wa reli ukiendelea kubadilisha sekta ya usafiri.
Katibu Mkuu wa Taboa, Priscus Joseph akizungumza na The Citizen amesema mazungumzo na Wakala wa Usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (Dart) yalifanyika mwaka 2022.
Katika mazungumzo hayo, wamiliki wa mabasi walipendekeza kununua mabasi ya kuendesha ndani ya mfumo wa BRT, lakini bado hawajapata mrejesho.
“Tulipendekeza turuhusiwe kuwekeza kwenye mabasi huku Serikali ikibaki na miundombinu, lakini bado hatujapata majibu,” amesema.
Mradi wa BRT, unaotekelezwa kwa awamu sita, umekumbwa na changamoto za kimuundo.
Awamu ya Kwanza ya BRT, iliyoanza mwaka 2016, ilikusudiwa kuendeshwa kwa mabasi 305, lakini kwa sasa yanafanya kazi mabasi 210 tu, huku mengi yakiwa yameharibika.
Awamu ya Pili ya BRT, iliyokamilika Oktoba 2023, inasubiri kuwasili kwa mabasi mapya.
Septemba 2, 2024, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa aliitaka Dart na Udart kushirikiana kuwaingiza waendeshaji wa mabasi ya mikoani kwenye mfumo wa BRT, ili kuboresha huduma za abiria badala ya kusubiri wawekezaji kutoka nje.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kadi na mageti ya kisasa kwenye vituo vya BRT Dar es Salaam, Mchengerwa alisema kuanza kwa huduma za treni za umeme kwenye SGR kumeathiri baadhi ya waendeshaji wa mabasi ya mikoani., hivyo ingefaa kuangalia uwezekano wa mabasi hayo kufanya kazi ndani ya mfumo wa BRT.
“Kumekuwa na mjadala wa muda mrefu kuhusu suala la mabasi. Awamu ya Kwanza ya BRT bado inahitaji mabasi 170 ili ifanye kazi kwa ufanisi, na mabasi 500 yanahitajika ili kuanza kazi kwa Awamu ya Pili ya BRT kwenye njia ya Mbagala. Hakikisheni mabasi yananunuliwa kufikia Desemba mwaka huu,” alisema.
Mchengerwa alisema: “Wamiliki wa mabasi ya mikoani, ambao wamekuwa wakisafirisha abiria kwa miaka mingi, wanaweza kufanya kazi kwa ufanisi katika njia za BRT. Kwa hivyo, wito unatolewa kwa waendeshaji wa ndani kuwekeza kwenye BRT badala ya kusubiri wawekezaji wa kigeni.”
Kwa upande wake, Meneja wa Operesheni wa BM Coach, Gabriel Makundi alisema ingawa wamiliki wa mabasi wako tayari na wanataka kutumia fursa hiyo, kuna haja ya uwazi zaidi kwenye mchakato wa zabuni kwa ajili ya uendeshaji wa mabasi ya BRT.
“Tangazo rasmi la zabuni linapaswa kutolewa ili kuainisha vigezo vinavyohitajika kwa mabasi ya mikoani kushiriki kwenye mfumo wa BRT,” alisisitiza.
Magawa wa Shabiby alisema kampuni yake iko tayari kuwekeza kwenye BRT lakini akatoa wito wa kufanyika mapitio ya nauli na mazingira bora ya uwekezaji.
Mkurugenzi Mtendaji wa Dart, Dk Athumani Kihamia alikiri kufanyika mazungumzo ya mwaka 2022 na wamiliki wa mabasi lakini alieleza kuwa hawakuafikiana.
“Tuna mpango wa kushirikisha waendeshaji zaidi ili kuelezea maendeleo yetu na kushughulikia masuala yanayowakabili,” alisema.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Taboa, Mustapha Mwalango alibainisha kupungua kwa idadi ya abiria na kuongezeka kwa mabasi yasiyo na kazi.
“SGR imeathiri shughuli zetu kuliko tulivyotarajia awali,” alisema.
Mkuu wa Mawasiliano wa Latra, Salum Pazzy ameshauri wamiliki wa mabasi kuiona SGR kama fursa badala ya tishio.
Alibainisha SGR ikitumika vema, kutakuwa na ongezeko la mahitaji ya mabasi kusafirisha abiria kutoka Dodoma kwenda mikoa mingine.
Mkurugenzi wa Usafiri wa Barabara wa Latra, Johansen Kahatano alithibitisha kupungua kwa huduma za mabasi.
“Tafiti zetu zinaonyesha kupungua kwa safari za mabasi na idadi ya abiria tangu SGR ilipoanza. Tunafanyia kazi kutatua athari hizi,” alisema.
Kutokana na hali hiyo, Latra inapanga kuandaa mkutano wa wadau wa usafiri, waendeshaji wa mabasi na Shirika la Reli Tanzania (TRC) ili kuchunguza njia za kuboresha muunganiko wa usafiri na kupunguza gharama za nauli kwa abiria.
Mkutano huo utalenga kutafuta suluhisho na kuboresha ushirikiano kati ya huduma za mabasi na treni, hususan karibu na vituo vya SGR.
Kadri sekta ya usafiri inavyoendelea kubadilika, wamiliki wa mabasi wana matumaini kwamba ushirikiano zaidi na mipango madhubuti itawezesha kuendelea kutoa huduma