ZAIDI YA SHILINGI BILIONI 830 KUKABILIANA NA ATHARI ZA EL – NINO

Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema Serikali imetoa zaidi ya shilingi Bilioni 830 kwa ajili ya kujenga upya na kwa ubora barabara na madaraja yalioathiriwa na mvua za El -Nino na kimbunga Hidaya nchini kote.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri huyo, Septemba 15, 2024 alipokagua ujenzi wa barabara ya Nyamwage – Utete (Km 33.7) kwa kiwango cha lami inayojengwa na mkandarasi M/s China Railway Seventh Group (CRSG), na kuhimiza umuhimu wa ujenzi huo kuwiana na thamani ya fedha na kukamilika kwa wakati ili wananchi wanufaike na mradi huo mapema iwezekanavyo.

“Niwahakikishie Mhe. Rais ameshatoa fedha hizi, kazi iko kwetu Wizara ya Ujenzi na TANROADS kuhakikisha wakandarasi makini wanapatika kujenga miundombinu hii iliyoathiriwa na mvua”, amesema Kasekenya.

Aidha, Kasekenya amesisitiza umakini na kasi katika ujenzi wa daraja la Mbambe lenye urefu wa mita 81 linalounganisha mji wa Ikwiriri na Mkongo pamoja na barabara ya Nyamwage – Utete (Km 33.7) kwa kiwango cha lami ili zikamilike haraka na kuchochea shughuli za usafiri na usafirishaji wilayani Rufiji.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri huyo amewahakikishia wakazi wa Kilwa, mkoani Lindi kuwa barabara ya Tingi-Kipatimu itajengwa kwa lami kwa awamu huku madaraja katika barabara hiyo ujenzi wake unatarajiwa kuanza mapema mwezi Oktoba, 2024.

Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Brabara (TANROADS), Mkoa wa Pwani, Mhandisi Baraka Mwambage amesema ujenzi wa barabara hiyo una jumla ya makalvati 109 ambapo kati ya hayo mawili yamekamilka na ujenzi wa kalvati moja unaendelea.

Naibu Waziri Kasekenya anaendelea na ziara yake katika Mikoa ya Lindi, Mtwara na Pwani kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara na madaraja hususan yalioathiriwa na mvua za El-Nino na kimbunga Hidaya.

Related Posts