Anayedai kufanya kazi za uwakili bila sifa, akutwa na kesi ya kujibu

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imemkuta na kesi ya kujibu mshtakiwa Baraka Mukama, anayekabiliwa na mashtaka ya kufanya kazi ya uwakili bila kuwa na sifa.

Hivyo, mshtakiwa huyo anatakiwa kuanza kujitetea mahakamani hapo kesho Jumatano Septemba 18, 2024.

Uamuzi huo umetolewa leo na Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swallo, baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wao wa mashahidi watano na Mahakama kumkuta na kesi ya kujibu.

Mukama anakabiliwa na mashtaka ya kufanya kazi ya uwakili bila kuwa na sifa na kuzuia watumishi wa umma kufanya kazi yao.

Mshtakiwa huyo anadaiwa kujitambulisha mahakamani hapo kuwa yeye ni wakili wa utetezi kisha kuwatetea washtakiwa katika kesi ya jinai namba 99 ya mwaka 2019 wakati akijua hana sifa hizo.

Hakimu Swallo amesema Mahakama imepitia ushahidi wa mashahidi watano wa upande wa mashtaka pamoja na vielelezo, hivyo kumkuta mshtakiwa ana kesi ya kujibu.

Hata hivyo, Mukama amedai atajitetea kwa kiapo na anatarajia kuwa na mashahidi watano pamoja na vielelezo kadhaa.

Mshtakiwa baada ya kueleza hayo, Hakimu Swallo aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 18, 2024 shauri hilo litkapoitwa kwa ajili ya mshtakiwa kuanza kujitetea.

Awali, wakili wa Serikali Asiat Mzamiru amedai shauri hilo liliitwa kwa ajili ya usikilizwaji na upande wa mashtaka wamefunga ushahidi wao.

Tayari mashahidi watano wa upande wa mashtaka wameshatoa ushahidi wao dhidi ya mshtakiwa huyo.

Miongoni mwa mashahidi hao ni Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashkata(NPS) Mkoa wa Dar es Salaam,  Faraji Ngukah (40) ambaye aliieleza Mahakama hiyo, namna mshtakiwa alivyomuita na kumwambia kuwa amsaidie ili askari Polisi wasimpeleke Kituo cha Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, kwani itakuwa shida kubwa kwa sababu yeye sio wakili bali ni kishoka.

Ngukah amedai Mkama alimwambia yeye ni kishoka na anatumia jina la Baraka Mukami ambaye ni daktari na mhadhiri wa Chuo cha Dodoma, hivyo aliomba asipelekwe Polisi.

Ngukah, ambaye ni shahidi wa tatu katika kesi hiyo ya jinai namba 177 ya mwaka 2023, alitoa maelezo hayo Julai 26, 2024, wakati akitoa ushahidi wake dhidi ya mshtakiwa huyo.

Ngukah alidai Mei 23, 2023, asubuhi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati akiendesha kesi ya Jinai namba 99/2019 inayokuwa inamkabili mshtakiwa Khalid Somole (54) na wenzake watatu, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Romuli Mbuya, mshtakiwa alijitambulisha kuwa ana wawakilisha mshtakiwa wa pili na watatu katika kesi hiyo.

Ngukah amedai katika kesi hiyo, washtakiwa walikuwa wanakabiliwa na mashtaka 16 yakiwamo ya kughushi stika za dawa zilizoisha muda wake na shtaka moja ni la kula njama ya kutenda makosa ya kughushi.

Alidai mbali na Somoe, ambaye ni mkazi wa Keko Mwanga; wengine ni Raphael Lyimo(40), mkazi wa Kimara Bonyokwa; Betty Mwakikusye(41) mkazi wa Chanika Msumbiji na Abdiel Mshana(57) mkazi wa Msasani Ubalozini, wote ni wakiwa ni wafanyabiashara.

“Washtakiwa hao wanne walikuwa na uwakilishi ambapo mshtakiwa wa kwanza na wanne walikuwa wanatetewa na wakili Agatha Fabian, wakati mshtakiwa wa pili na wa tatu wao walikuwa wanatetewa na mshtakiwa ambaye alijitambulisha kuwa ni Wakili Baraka Mukami,” amedai Ngukah.

Ameendelea kudai siku hiyo, kesi iliitwa kwa ajili ya kuendelea na ushahidi, lakini aligundua mshtakiwa wa tatu hakuwepo mahakamani na wala hakuwa ametoa taarifa ya kutokuwepo kwake mahakamani hapo kwa upande wa mashtaka.

“Katika kesi hiyo, nilikuwa mimi na mwenzangu Agness Mahinga na upande wa mashtaka siku hiyo hatukuwa na shahidi, hivyo tuliomba kuahirisha kesi hiyo na kuiomba Mahakama itoa hati ya kumwita mshtakiwa wa tatu ili aje aeleze zababu za kushindwa kufika mahakamani kusikiliza shauri lake,” amedai Ngukah.

Baada ya kuwasilisha ombi hilo kwa hakimu, Mukama alipinga maombi hayo na badala yake aliomba Mahakama ifute kesi hiyo kwa kuwa upande wa mashtaka wameshindwa kuleta shahidi.

Mukama aliomba Mahakama iwafutie wateja wake kesi hiyo chini ya kifungu 225(5) cha Sheria ya Mwenendo wa Jinai (CPA).

“Upande wa mashtaka tulipinga maombi ya Mukama ya kufutiwa kesi washtakiwa na badala yake, tuliomba Mahakama itupe muda ili tuweze kufanya maamuzi,” amedai wakili Ngukah.

Hata hivyo, Nguka amedai wakati wote wanaendelea na shauri hilo, mshtakiwa huyo alikuwa anajitambulika kama Wakili Baraka Mukami.

Aliendelea kudai kuwa baada ya muda, hakimu Mbuya alitoa uamuzi na kueleza kuwa anakubaliana na maombi ya Mukama na kuifuta kesi hiyo kupitia kifungu hicho.

Alidai baada ya washtakiwa hao kufutiwa kesi hiyo, upande wa mashtaka ulielekeza askari polisi waliokuwepo mahakamani hapo kuwashikilia washtakiwa hao ili waweze kukata rufaa ya kupinga uamuzi uliotolewa na mahakama hiyo.

Aliendelea kudai kuwa baada ya upande wa mashtaka kutoa maelekezo hayo, askari Mubaraka alitoka chumba cha Mahakama na kuwenda kuwaita wenzake ili kuongeza nguvu.

“Wakiwa katika zoezi la ukamataji washtakiwa hao, Mukama aliwafuata askari hao ambao ukamataji huo ulikuwa unafanyika katika lango (geti) la kuingia Mahakama ya Kisutu na kisha kumkaba mmoja wapo,” amedai.

Mshtakiwa alifika getini hapo na kuanza kuwasukuma askari huku akiwaambia wawaachie wateja wake na kumjeruhi askari Mubaraka upande wa kiwiko cha mkono wa kushoto na upande wa kulia kupata michubuko.

Wakati Mukama ana mkaba askari, Wakili Agatha yeye hakuwepo eneo hilo.

Amedai baada ya kupata taarifa kuwa kuna wakili anapimana ubavu na askari, alitoka chumba cha Mahakama na kwenda kuangalia nini kinaendelea katika geti la kuingia mahakamani hapo.

Amedai kutokana na vurugu aliyofanya mshtakiwa huyo ilisababisha mshtakiwa mmoja kukimbia, huku wengine wakikamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi.

“Baada ya kupata taarifa ya mshtakiwa mmoja kukimbia, niliagiza Mukama akamatwe na awekwe maabusu wakati hatua nyingine zinafanyika,” amedai na Ngukah 

Amedai akiwa bado mahakamani, Askari Mubaraka alimfuata Ngukah ofisi ya waendesha mashtaka na kumwambia kuwa yule waliyemkamata anaomba anonane na wakili aliyekuwa anaendesha kesi iliyofutwa.

 “Nilienda na kumkuta Mukama amewekwa chini ya ulinzi wa polisi, na aliniambia kuwa anaomba nimsaidie askari polisi wasimpeleke kituo cha polisi kwani itakuwa shida kubwa kwake maana yeye sio wakili bali ni kishoka na jina alilokuwa anatumia mahakamani ni Baraka Mukami la daktari ambaye ni wakili na mhadhiri wa Chuo cha Dodoma na hapo tulikuwa tunaongea wawili tu yaani mimi na yeye,” amedai Nguka.

Alidai Mei 30, 2023, akiwa mahakamani anaendesha kesi, alifuatwa na askari aitwaye Stephano na kuelezwa kuwa anatakiwa kuchukuliwa maelezo.

Shtaka la kwanza, mshtakiwa anadaiwa kwa makusudi alimzuia Askari Polisi mwenye namba J 515 PC Mubaraka Abdallah, asimkamate Harid Rajabu maarufu kama Somole, ambaye alifutuwa kesi ya jinai namba 99/2019.

Shtaka la pili ni kufanya kazi ya uwakili bila kuwa na sifa, tukio analodaiwa kulitenda Mei 23, 2023 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Mshtakiwa anadaiwa siku hiyo, akiwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Romuli Mbuya, mshtakiwa alijiwakilisha kama wakili wa kijitegemea mwenye namba ya usajili 4696, wakati akijua ni uongo na yeye sio wakili.

Mshtakiwa huyo alijiwakilisha kama wakili katika kesi ya jinai namba 99/2019 ambayo alikuwa anawatetea washtakiwa wawili kati ya wanne waliokuwa wanakabiliwa na mashtaka ya kughushi nyaraka na stika mbalimbali za dawa.

Kwa mara ya kwanza, mshtakiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo Oktoba 2, 2023 na kusomewa mashtaka yake katika kesi ya jinai namba 177/2023.

Related Posts