Dk Biteko aungana na waombolezaji maziko ya Askofu Sendoro Mwanga 

Mwanga. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amewasili katika Kanisa Kuu la Mwanga kuungana na mamia ya waombolezaji katika ibada ya  maziko ya aliyekuwa Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mwanga, Askofu Chediel Sendoro.

Maziko ya Askofu Sendoro, yanafanyika leo, Septemba 17, 2024, katika Kanisa Kuu, Mwanga, mkoani Kilimanjaro na yamehudhuriwa na mamia ya wachungaji na maaskofu takribani 30.

Katika ibada hiyo inayoongozwa na mkuu wa KKKT, Dk Alex Malasusa, vilio na simanzi vimetawala, huku baadhi ya waumini na waombolezaji wakiwamo watoto na wanafunzi wakishindwa kujizuia kutokwa na machozi.

Viongozi wengine walioshiriki ibada hiyo ni Cleopa Msuya ambaye ni Waziri Mkuu mstaafu,  Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Jerry Silaa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uwekezaji), Profesa Kitila Mkumbo, Mbunge wa Mwanga, Joseph Tadayo na viongozi wengine wa serikali.

Wameshiriki pia wakuu wa taasisi za Serikali na binafsi kutoka Wilaya ya Mwanga alikokuwa akihudumu Askofu Sendoro pamoja na waimbaji wa kwaya kutoka sharika za Mwanga na Dayosisi ya Mashariki na Pwani.

Katika ibada hiyo rangi zilizotawala ni nyeusi na nyeupe, huku wakuu wa majimbo na maaskofu wakivaa mavazi ya rangi nyekundu  na baadhi yao zambarau.

Askofu Sendoro alifariki dunia Septemba 9, 2024 kwa ajali iliyotokea eneo la Kisangiro, Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro saa 1:30 usiku, baada ya gari alilokuwa akiliendesha aina ya Toyota Prado, akitokea Kileo kuelekea nyumbani Mwanga, kugongana uso kwa uso na lori.

Sendoro ndiye askofu wa kwanza wa Dayosisi ya Mwanga aliyeingia kazini Jumapili ya Novemba 6, 2016 baada ya kuzaliwa kwa dayosisi hiyo iliyotokana na kugawanywa kwa dayosisi mama ya Pare.

Related Posts