Dk Biteko kuongoza waombolezaji maziko ya Askofu Sendoro

Mwanga. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko anaongoza mamia ya waombolezaji kwenye maziko ya aliyekuwa Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mwanga, Askofu Chediel Sendoro yanayofanyika leo, Septemba 17, 2024, katika Kanisa Kuu, Mwanga, mkoani Kilimanjaro.

Askofu Sendoro alifariki dunia Septemba 9, 2024 kwa ajali iliyotokea eneo la Kisangiro, Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro saa 1:30 usiku, baada ya gari alilokuwa akiendesha aina ya Toyota Prado, akitokea Kileo kuelekea nyumbani Mwanga, kugongana uso kwa uso na lori.

Sendoro ndiye askofu wa kwanza wa Dayosisi ya Mwanga  na aliingizwa kazini Jumapili Novemba 6, 2016 baada ya kuzaliwa kwa dayosisi hiyo iliyotokana na kugawanywa kwa dayosisi mama ya Pare.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Septemba 17, 2024, Katibu Mkuu wa Dayosisi ya Mwanga, Mathias Msemo amesema katika ibada hiyo ya maziko itakayoongozwa na Mkuu wa KKKT, Dk Alex Malasusa, pia itahudhuriwa na Biteko.

Amesema mbali na kiongozi huyo, pia watahudhuria maaskofu wa KKKT na makanisa mengine, viongozi wa dini mbalimbali na wa  Serikali.

Akizungumzia ratiba ya leo, Msemo amesema kuanzia saa 12:00-3:30 asubuhi waombolezaji wataendelea kutoa heshima za mwisho na saa 4:00 asubuhi ibada ya maziko itaanza.

“Mwili wa baba askofu umelala hapa kanisani, na kuanzia saa 12:00 asubuhi watu wameendelea na utaratibu wa kutoa heshima za mwisho ratiba itakayomalizika saa 3:30 asubuhi na saa 4:00 ibada itaanza ambayo itaenda mpaka saa 7:00 mchana, pia tutasikia salamu kutoka kwa kiongozi wa Serikali na kanisa,” amesema Msemo.

Related Posts