Arusha. Uongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) umetoa msaada wa vifaa vya maabara vyenye thamani ya Euro2.6 milioni (Sh6.9 bilioni) kwa nchi wanachama ili kuimarisha uwezo wa kupambana na magonjwa ya milipuko ukiwamo wa Homa ya Nyani (Mpox).
Imeelezwa kuwa vifaa hivyo ni sehemu ya mpango mpana wa EAC, unaolenga kutoa msaada wa ziada wa Dola 12 milioni za Marekani (Sh31.2 bilioni) kwa ajili ya kuboresha mtandao wa maabara za rufaa katika ukanda huo, pamoja na kuanzisha kituo cha umahiri cha kikanda kwa uchunguzi wa virusi vya magonjwa hayo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne, Septemba 17, 2024, Naibu Katibu Mkuu wa EAC, Andrea Ariiki amesema msaada huo utasaidia kuimarisha uwezo wa nchi wanachama kugundua magonjwa ya mlipuko haraka, vimelea na kudhibiti usambaaji wa magonjwa hayo kabla hayajaleta madhara makubwa.
“Mpox kwa sasa ni tishio kubwa, umeshaathiri zaidi ya watu 17,541 na kusababisha vifo 517; na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ina na zaidi ya visa 16,800 na vifo 500,” amesema Ariiki.
Amesema nchi nyingine zilizoathiriwa na Mpox ni Burundi (visa 150 na vifo 10), Kenya (visa 20 na vifo viwili), Rwanda (visa 10 na kifo kimoja), na Uganda (visa vitano na vifo vinne).
“Vifaa hivi vinavyojumuisha maabara inayotembea iliyotolewa kwa DRC, vimefadhiliwa na Serikali ya Ujerumani kwa ushirikiano na Taasisi ya Bernhard Notch ya Tiba ya Kitropiki kutoka Hamburg, Ujerumani,” amesema.
Ariiki amesema vifaa hivyo vitazisaidia nchi wanachama kugundua magonjwa haraka zaidi kutokana na uwezo wake wa kufanya uchunguzi wa vinasaba vya virusi na bakteria.
Pia, amesema vifaa hivyo vitasaidia pia kufuatilia magonjwa yanayoibuka na kurudi katika ukanda wa EAC kwa ajili ya kuchukua hatua mapema. Hivyo, amesisitiza kuwa hatua hizo zinalenga kuzuia athari mbaya kwa sekta za biashara, uchumi na maendeleo ya kijamii katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Mtaalamu wa afya kutoka Taasisi ya Bernhard Notch, Muna Affara amesema taasisi yao inajikita katika kushughulikia milipuko ya magonjwa yenye uwezo wa kusambaa mipakani katika eneo la EAC.
“Tumeanzisha mtandao wa maabara tisa za simu, zimejikita kushughulikia magonjwa mbalimbali ya milipuko kama Mpox, Marburg, Ebola, homa ya manjano na COVID-19,” amesema.
Affara amesema maabara inayotembea iliyotolewa kwa DRC itaongeza uwezo wa nchi hiyo sio tu kukabiliana na Mpox, bali pia magonjwa mengine ya milipuko yanayoikumba.