Fei Toto amtaka tena Aziz Ki

KIUNGO Mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’ amesema anatamani bato yake na Stephane Aziz Ki liendelee tena msimu huu kwani inamuongezea ubora kutokana na kumfuatilia mpinzani wake kwa kujifunza vitu.

Wawili hao msimu uliopita walikuwa wanawania kiatu cha ufungaji bora hadi mechi ya mwisho ya msimu ambapo Aziz Ki aliibuka mfungaji bora baada ya kupachika mabao 21 akimuacha Fei Toto kwa mabao mawili baada ya kupachika 19 kambini.

Akizungumza na Mwanaspoti, Fei Toto amesema licha ya kuwa sio mshambuliaji halisia lakini anafurahia kufunga kila anapopata nafasi na ushindani wake na Aziz Ki umekuwa chachu ya kuendelea kuimarika kwake kwani anajifunza vitu vingi kutoka kwa aliyekuwa mshindani wake msimu ulioisha.

“Ukiachana na bato iliyokuwepo kati yangu na Aziz Ki mimi namkubali sana huyu mchezaji anajua mpira na nimekuwa nikimfuatilia ata wakati tunashindana siku timu yake ikicheza nilikuwa namuangalia na akifunga alikuwa ananipa hasira ya kupambana ili na mimi nifunge,” amesema na kuongeza:

“Hivyo mbali na ushindani mimi nilikuwa nanufaika kwa kujifunza vitu kutoka kwake na kunipa hasira za mimi kupambana ili nifanye kama alichokifanya, natamani bato hilo liendelee tena msimu huu kwani linanijenga linanitoa sehemu moja kwenda nyingine.”

Fei Toto alisema vita yake anaiendeleza alipoishia huku akikiri kuwa msimu ulioisha ulikuwa bora kwake sasa anapambana kuhakikisha anaendeleza ubora wake kwa kuipambania timu hiyo iweze kufikia malengo ambayo ni kutwaa mataji.

“Hakuna kinachoshindikana natamani kuipa mataji timu yangu ya sasa baada ya kuyabeba nikiwa nje ya Azam FC ndoto yangu kubwa ni kuona natwaa taji la ligi au Kombe la Shirikosho (FA) lakini pia ikitokea tukabena yote itanijengea heshima kubwa na naamini hilo linawezekana kama sio msimu huu basi ata ujao.”

Akizungumzia msimu huu kwa ujumla Fei Toto alisema ni msimu mgumu lakini hawatarajii kutoka kwenye malengo ya kufanya vizuri huku akikiri kuwa mwanzo mbaya kwao hauwezi kuwakatisha tamaa kwani bado wana mechi nyingi.

“Mpira una matokeo matatu hivyo tuliyoyapa kwenye mechi za mwanzo ni sehemu ya mchezo tunaachana nayo sasa akılı zote tunaelekeza kwenye mchezo unaofuata ambao hatutarajii kufanya makosa kwani tunahitaji kuendeleza tulipoishia.”

Azam FC wamekusanya pointi mbili kwenye mechi mbili walizocheza baada ya kuambulia sare dhidi ya JKT Tanzania ugenini na nyumbani walikubali suluhu dhidi ya Pamba timu iliyopanda daraja msimu huu.

Related Posts