KLABU YA ROTARY YA DAR E SLAAAM YAZIPATIA MADAWATI MENGINE SHULE ZENYE UHITAJI.

Dar es Salaam, 15th Septemba 2024

Klabu ya Rotary ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na Klabu ya Rotary ya Vancouver, chini ya utaratibu wa Rotary Global Grants, imepiga hatua kubwa katika kuimarisha miundombinu ya elimu jijini Dar es Salaam baada ya kutoa msaada wa madawati mengine 138 kwa shule ya msingi Kunduchi, iliyopo Wilaya ya Kinondoni.

Jumla ya madawati 3,708 yenye thamani ya Tsh. 470,916,000/- zimetolewa na Klabu ya Rotary ya Dar es Salaam kwa shule zenye uhitaji kwenye mji wa Dar es Salaam hadi sasa.

Hii ni hatua kubwa katika juhudi zinazoendelea za Klabu ya Rotary ya Dar es Salaam za kukabiliana na uhaba wa madawati katika shule za msingi jijini Dar es Salaam.

Kwa huu mchango wa jumla wa madawati 3,708 hadi sasa, wanachama wa Rotary na wafadhili wake, kupitia Klabu ya Rotary ya Dar es Salaam, wamewainua zaidi ya wanafunzi 10,000 wa shule ya msingi kutoka sakafuni.

Hii ni taswira ya wazi ya dhamira ya Klabu katika kuboresha mazingira ya elimu kwa watoto nchini Tanzania.

Akizungumza kwa niaba ya Shule ya Msingi ya Kunduchi, Mwalimu Mkuu, Emmanuel Munisi alisema kwamba msaada huo kutoka kwa Rotary unatatua moja ya matatizo makubwa yanayoikabili shule yao.

Mwalimu Mkuu alisema madawati hayo yatasaidia kwa kiasi kikubwa katika utoaji wa elimu kwani sasa wanafunzi wataweza kusoma kwa raha. Bw. Munisi aliishukuru Rotary kwa msaada huo mkubwa na aliahidi kwamba shule itatunza vizuri madawati ili kuhakikisha yanadumu kwa muda mrefu na kuwahudumia wanafunzi zaidi katika miaka ijayo.

Utafiti wa muda mrefu unasisitiza umuhimu wa mazingira mazuri ya kujifunza katika kukuza maendeleo ya kitaaluma kwa watoto. Kwa kuzingatia hili, madawati yaliyotolewa yameundwa kwa muundo wa chuma na mbao ngumu zilizotibiwa ili kuhakikisha uimara wa madawati.

Akizungumzia mpango huo, Rais wa Klabu ya Rotay ya Dar es Salaam, Manisha Tanna, alisisitiza mbinu jumuishi iliyochukuliwa na klabu hiyo, ya utoaji wa madawati, sambamba na kujenga uwezo kwa Waalimu, pamoja na kupanda miti ili kuhifadhi mazingira.

Mbali na madawati 3,708 yaliyotolewa, Klabu imepanda miti 7140 katika maeneo mbalimbali pamoja na kutoa mafunzo kwa Walimu 80 wa Shule za Msingi kuhusu TEHAMA katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT).

Wakati Klabu ya Rotary ya Dar es salaam ikiendelea kushirikiana na wadau mbalimbali, klabu inasisitiza dhamira yake ya kuweka mazingira wezeshi ya elimu, ambapo kila mtoto ana fursa ya kustawi.


Related Posts