LHRC yataka uchunguzi mauaji Dodoma

Dodoma. Kufuatia mauaji ya watu watatu wakiwamo watoto wawili wa familia moja, yaliyotokea usiku wa kuamkia jana Jumatatu ya Septemba 16, 2024, Kata ya Nala jijini Dodoma, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimelaani tukio hilo na kutaka vyombo vya ulinzi na usalama kubaini chanzo cha mauaji hayo.

Watoto hao miili yao inadaiwa kukutwa imeungua huku mwili wa mfanyakazi wa ndani ukiwa na majeraha kichwani.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Anania Amo akizungumza na Mwananchi usiku wa jana Jumatatu Septemba 16, 2024 amesema watu watatu walikutwa wamefariki dunia.

Amesema mama mwenye nyumba alikutwa amejeruhiwa na amepelekwa hospitali kwa ajili ya matibabu.

Leo Jumanne Septemba 17, 2024, LHRC imetoa taarifa ya kulaani tukio hilo. Mkurugenzi mtendaji wa kituo hicho, Dk Anna Henga amesema hivi karibuni kumekuwepo ongezeko kubwa la matukio ya kikatili nchini hususani ya mauaji, watu kupotea na kutekwa.

Amesema matukio hayo yanaongeza hofu kubwa kwa wananchi kwa kuwa yanatishia usalama wao na jamii nzima na kwamba ongezeko la matukio hayo yanazidisha hofu.

Kituo hicho kimetoa rai kwa mamlaka za ulinzi na usalama kuchunguza kwa kina tukio hilo ili kubaini chanzo cha mauaji hayo na kuhakikisha wahusika wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria kwa mujibu wa sheria za nchi.

Pia, amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuimarisha ulinzi wa raia kwa kuchukua hatua za haraka.

“Jamii nzima iheshimu sheria na kuepuka kujichukulia sheria mkononi… badala ya kulipa visasi na kufanya matukio ya kikatili watafute suluhu za kisheria katika kutatua migogoro,” amesema Henga.

Viongozi wa dini na jamii wametakiwa kuendelea kuhubiri amani na kutii sheria ili kuzuia vitendo vya ukatili na kujichukulia sheria mkononi.

“Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kinasisitiza umuhimu wa kuendeleza utulivu, haki na usalama wa raia kwa kushirikiana na vyombo vya dol ana kuheshimu misingi ya haki za binadamu,” amesema Henga.

Related Posts