Mahakama Kuu yatupa tena shauri dhidi ya mawakili wa ‘waliotumwa na afande’

Dodoma. Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma imetupilia mbali kwa mara nyingine shauri la mapitio ya mwenendo wa kesi ya jinai inayowakabili washitakiwa wanne wanaodaiwa kumbaka kwa kundi na kumwingilia kinyume cha maumbile binti, mkazi wa Yombo Dovya jijini Dar es Salaam.

Uamuzi huo umefikiwa baada ya Mahakama kujiridhisha kuwa shauri hilo halina mashiko kisheria.

Shauri hilo namba 24889 la mwaka 2024 ambalo lilikuwa mbele ya Jaji Steven Kakolaki lilifunguliwa na wakili Leonard Mashabara kwa mara ya pili, baada ya Mahakama hiyo kulitupilia mbali kutokana na kuwapo kasoro za kisheria.

Mahakama ililitupa shauri la awali baada ya Mashabara kuwaingiza watu ambao hawahusiki kwenye kesi ya msingi inayoendelea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma kuwa wajibu maombi.

Uamuzi wa kwanza ulitolewa na Jaji Suleiman Hassan Agosti 29, 2024 kutokana na pingamizi lililowekwa na wajibu maombi wakieleza baadhi yao hawahusiki katika kesi ya msingi.

Waombaji ambao hawahusiki na kesi ya msingi ni Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Mwanasheria Mkuu wa Serikali na mawakili wanne wanaowatetea washitakiwa kwenye kesi ya msingi.

Baada ya uamuzi huo wa Mahakama, Mashabara kupitia wakili wake Emmanuel Anthony walifungua shauri lingine mahakamani hapo dhidi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali na washitakiwa wanne wanaoshitakiwa kwenye kesi ya msingi iliyopo Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma.

Baada ya Mahakama Kuu kusikiliza hoja za pande zote mbili, leo Septemba 17, 2024 imetoa uamuzi wa kutupilia mbali shauri hilo.

Mahakama imesema kwa mujibu wa sheria kila mtu ana haki ya kuwakilishwa na kusikilizwa mahakamani.

Mashabara alifungua maombi akiiomba Mahakama kupitia uhalali wa washitakiwa katika shauri la jinai namba 23476 la mwaka 2024 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma kuwakilishwa na mawakili kutoka TLS.

Alidai TLS walitoa tamko lenye viashiria vyenye mgongano wa masilahi, hivyo kufanya mawakili wote ambao ni wanachama wa chama hicho kukosa sifa za kuwatetea washitakiwa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Septemba 17, nje ya jengo la Mahakama, wakili Anthony amesema Jaji Kakolaki katika uamuzi amesema TLS haibanwi na kanuni za utendaji za mawakili kwani wakili mmojammoja anawajibika kwa mteja wake moja kwa moja.

Amesema hoja nyingine ambayo Jaji ameitoa ni kwamba, washitakiwa wana haki ya kuwakilishwa mahakamani ambayo ni ya msingi.

Washitakiwa katika kesi hiyo ni askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), MT 140105 Clinton Damas, maarufu Nyundo, askari Magereza C.1693 Praygod Mushi, Nickson Jackson ‘Machuche’ na Amin Lema anayejulikana pia kwa jina la Kindamba ambao kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka ya kumbaka kwa kikundi na kumwingilia kinyume cha maumbile binti huyo anayetambulishwa mahakamani kwa jina la XY.

“Baada ya uamuzi huo basi mteja wangu ameona kuna haja ya kwenda Mahakama ya Rufani, tunaona si rahisi kutenganisha TLS na shughuli zao hasa pale chama kinaposimama kama chombo cha utendaji,” amesema. Amesema wameshawasilisha notisi ya rufaa ambayo imepewa namba 6430684 ya mwaka 2024 ambayo imesajiliwa kwa njia ya mtandao.

Wakili wa washitakiwa katika kesi ya msingi, Robert Owino amesema Mahakama Kuu imelitupilia mbali shauri hilo kwa sababu kila mtu ana haki ya kuwakilishwa na kusikilizwa mahakamani, hivyo washitakiwa wana haki ya kuwakilishwa na mawakili ambao ni wanachama wa TLS kwa sababu sheria inayotumika mahakamani na kanuni zake ni ya mawakili na siyo za TLS.

“Unajua sheria inasema kila mtu ana haki ya kuwakilishwa na kusikilizwa mahakamani na mwenye dhamana ya kumwakilisha mtu mahakamani ni wakili, sasa endapo Mahakama itazuia watu wasiwakilishwe kwa sababu chama cha wanasheria kimesema kitasababisha taharuki kwa wananchi kwa sababu itakuwa chama kikitoa tamko kuhusu kesi yoyote basi wanasheria hawatawawakilisha watu hao, hivyo wengi watakosa uwakilishi ambao ni haki yao ya msingi wawapo mahakamani,” amesema Owino.

Amesema baada ya Mahakama Kuu kutupilia mbali shauri hilo, kesi itaendelea kusikilizwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma kwa tarehe itakayopangwa.

Related Posts