MKUU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Alex Malasusa, amelaani matukio ya utekaji na mauaji ya raia na kusema kanisa halitaki kusikia uhalifu huo tena. Anaripoti Restuta James, Kilimanjaro … (endelea).
Ameyasema hayo leo Septemba 17, 2024, mbele ya Naibu Waziri Mkuu, Dk. Dotto Biteko, wakati wa ibada ya maziko ya aliyekuwa Askofu wa Mwanga, Dk. Chediel Sendoro, iliyofanyika katika Kanisa Kuu, Mwanga, mkoani Kilimanjaro.
“Hili jambo lisitokee tena, tusisikie tena mahali popote na tutakapoomba Mungu atawadhihirisha wote wanaofanya kazi hiyo ya uovu,” amesema.
Ametahadharisha kwamba damu inayomwagwa inasababisha laana kwenye nchi na kutaka ‘ifike mwisho’ wa matukio hayo.
“Naibu Waziri Mkuu, ninaomba fursa ya kutamka mahuzuniko yetu tuliyonayo na hasa kwa hali inayoendelea katika nchi yetu kusikia habari ambazo si nzuri za vifo, sasa tumesikia ajali nyingi sana katika barabara zinazotuunganisha katika nchi yetu, nina hakika sisi sote tukichukua wajibu wetu huenda tukazifuta kabisa au tukazipungumza.”
“Lakini sambamba na hilo masikio yetu na wengine wameshuhudia jinsi ambavyo kumekuwa na matukio ambayo hayakuzoeleka katika nchi yetu. Hasa kutekwa au kutoweka kwa Watanzania, nafikiri tuseme ifike mwisho,” amesema.
Ametahadharisha kwamba Biblia inaonya kuhusu mauaji akieleza nchi inalaaniwa damu inapomwagika.
“Hatutaki laana hii iingine katika nchi yetu. Tuombe kila mwenye kujua maana ya maombi kuliombea jambo hili, najua wanasiasa wamekuwa wakilizungumza, hebu tulisogeze pia hili kama haja yetu mbele za Mungu,” amesema.
Katika maziko hayo ambayo yamehudhuriwa na viongozi wa serikali na wa kidini, Askofu Malasusa alitoa maelekezo ya maombi kwa maaskofu na wachungaji wa KKKT nchi nzima kufanya maombi maalumu kwa ajili ya watekaji, watesaji na wauaji.
“Tumefika kipindi ambacho Watanzania wamekuwa na hofu ambayo ipo katika watu ambao wameshuhudia kabisa. Kanisa liingine kwenye maombi, tusiache kulichukulia jambo hilo kiroho,”
ameiomba pia serikali kuandaa meza ya majadiliano ili kutafuta suluhu ya pamoja.