KUSHINDWA kwa mabosi wa KenGold kutoa mkwanja wa maana dirisha lililopita la usajili inaelezwa kuwa ni miongoni mwa mambo yaliyomuangusha aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Fikiri Elias ambaye ameamua kukaa pembeni kutokana na mwenendo wa chama hilo.
Jana Jumatatu Fikiri alifanya uamuzi huo sambamba na msaidizi wake, Luhaga Makunja mara baada ya KenGold ya Mbeya kupoteza katika mchezo wake wa tatu wa ligi wakiwa ugenini jiji Dar dhidi ya KMC kwa bao 1-0, kikiwa ni kipigo chao cha tutu mfululizo tangu kuanza kwa ligi msimu huu.
Mtu wa karibu wa kocha huyo, alilieza Mwanaspoti kwamba: “Yapo mapendekezo ambayo kocha aliyawasilisha mwanzoni kabisa mwa msimu lakini ilishindikana kutekelezwa na viongozi, pamoja na hilo alijitahidi kufanya kile anachoweza ili kulingana na wachezaji waliopo ingawa hakuona kama wanaweza kufikia lengo.”
Chanzo hicho kiliendelea kusema: “Alichofanya ni uwajibikaji, viongozi wanatakiwa na wao kujitathimini, wajaribu kutafuta namna bora ya kuinusuru timu ili ifanye vizuri katika michezo iliyopo mbele yao, daraja la kwanza na ligi kuu ni vitu viwili tofauti, hili wanatakiwa kutambua.”
Kwa upande wake, Fikiri alisimamia kile alichosema baada ya kupoteza mchezo wao wa tatu katika ligi hakutaka kueleza kiundani nini kipo nyuma ya matokeo hayo akisema: “Nimewajibika kama kocha kwa kukaa pembeni kutokana na mwenendo wa timu.”
Mtendaji Mkuu wa KenGold, Benson Mkocha, alibainisha kwamba Fikiri kuondoka kwake kikosini hapo ni kutokana na kuomba mwenyewe na wao wameridhia hilo wala hakuna mambo mengine zaidi.
Kung’atuka kwa Fikiri kumeufanya uongozi wa KenGold kumteua Jumanne Charles kuwa kocha wa muda wakati mchakato wa kutafuta mkufunzi mpya kwenye kikosi hicho chenye maskani yake Mbeya ukiendelea.
Kituo kinachofuata kwa KenGold ni Bukoba ambako watakuwa wageni wa Kagera Sugar ambao nao watakuwa wakisaka ushindi wao wa kwanza katika ligi baada ya hapo watarejea tena Dar kukabiliana na Yanga.