Uturuki. Mamlaka ya Kukabiliana na Maafa na Dharura (AFAD), imetuma meli kutoka nchini Uturuki ambayo imebeba tani 2,995 za misaada ya kibinadamu kuelekea Sudan kunakoendelea mapigano ya wenyewe kwa wenyewe kwa muda mrefu sasa.
Makamu wa Rais wa Afad, Hamza Tasdelen amesema tani 2,955 za misaada hiyo ya chakula, malazi, vifaa vya afya, jenereta pamoja na mahema, vimeshapakiwa kwenye meli hiyo na tayari ipo safarini.
“Tumekusanyika hapa kutuma karibu tani 3,000 za msaada. Hii ni pamoja na mahema 18,500, mablanketi zaidi ya 17,000 na vifaa mbalimbali vya makazi, tani 1,000 za unga na karibu tani 500 za paket za chakula,” amesema.
Tasdelen ameeleza meli ya kwanza kutoka Mersin Uturuki iliwasili Sudan Julai 19 ikiwa na tani 2,500 za msaada na hii ikiwa ni meli ya pili kuelekea nchi hiyo.
“Nchi yetu inaendelea kusimama pamoja na wanadamu wote, bila kujali dini, lugha, au rangi, duniani kote,” ameongeza.
Akiangazia juhudi zinazofanywa kusaidia Sudan amesema kuna matatizo katika eneo karibu na uturuki, ikiwa ni pamoja na migogoro ya ndani inayoendelea, ukame na mvua nyingi.
Tasdelen amesisitiza si mara ya kwanza kutoa msaada kwa kuwa ni misaada muhimu ilitumwa Misri kwa ajili ya kupelekwa Gaza ambapo ilitumwa jumla ya tani 75,000.
Chini ya uongozi wa Rais Recep Erdogan na maagizo ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Ali Yerlikaya, uamuzi umefanywa wa kufikisha tani 30,000 za unga huko Gaza.
“Tunatanguliza shukrani zetu za dhati kwa mashirika yetu yasiyo ya kiserikali na Hilali nyekundu ya Uturuki kwa pamoja tuliandaa maudhui ya misaada,” amesema Tasdelen.
Hafla ya kuaga meli hiyo katika Bandari ya Mersin ilifanyika Jumatatu, ikiwa ni meli ya pili ya msaada kuelekea Sudan.
Nchini Sudan mapigano yameendelea katika nchi hiyo ya kaskazini mashariki mwa Afrika tangu katikati ya Aprili 2023, wakati mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan na naibu wake wa zamani Mohamed Hamdan Daglo, ambaye anaongoza kikosi cha wanamgambo wa Rapid Support Forces walipoanza kuzozana
Imeandaliwa kwa msaada wa mtandao