Miili miwili yaopolewa ajali ya mtumbwi Ziwa Victoria

Bunda. Miili miwili kati ya mitano iliyohofiwa kufa maji baada ya mtumbwi kuzama Ziwa Victoria imeopolewa na kufanya idadi ya miili iliyopatikana kufikia mitatu.

Mwili mmoja ulipatikana muda mfupi baada ya ajali kutokea.

Miili hiyo ya mwanamke na mwanamume imeopolewa leo Septemba 17, 2024 asubuhi ikiwa ni siku ya tatu tangu kuzama ziwani humo baada ya mtumbwi waliokuwa wakisafiria kupasuka na kujaa maji kisha kuzama kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kuzidiwa uzito.

Kaimu Kamanda wa Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mara, Agostino Magere amesema miili hiyo imeopolewa kati ya saa 12 hadi saa mbili asubuhi ya leo huku kazi ya kutafuta mingine ikiendelea hadi sasa.

Ametaja miili iliyoopolewa kuwa ni wa Nyanchugu Lazaro (39) na Machumu Machumu (32).

Amesema licha ya uwepo wa changamoto ya tope na giza ndani ya ziwa, kazi ya utafutaji wa miili hiyo bado inaendelea baada ya kuongezewa nguvu ya askari na vifaa kutoka Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mwanza.

“Hii miili ambayo tayari imeopolewa sasa hivi  inafanyiwa taratibu za kiserikali kisha itakabidhiwa kwa familia kwaajili ya shughuli za mazishi” amesema Magere.

Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dk Vicent Naano amesema kazi ya utafutaji wa miili mingine bado inaendelea kwa kushirikisha wenyeji wa maeneo hayo pamoja na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.

Naano amesema Serikali itagharamia usafiri pamoja na majeneza kwa ajili ya mazishi ya watu hao ambao hata hivyo kwa mujibu wa mila na desturi za wakazi wa kijiji hicho, watu waliofariki majini hawazikwi kwa kutumia majeneza.

“Nimeambiwa watu waliokufa maji  hawazikwi kwa majeneza kwa mila na desturi za huku, lakini kwa vile tulikuwa tumeandaa pesa kwa ajili ya majeneza basi familia husika itakabidhiwa pesa taslimu ambayo tunaamaini itasaidia katika shughuli zingine za msiba badala ya kununua jeneza, pia Serikali itasafirisha miili ya marehemu hadi pale familia inatarajia kuzika,” amesema.

Amesema bado wanaendelea kumsaka mmiliki wa mtumbwi uliosababisha maafa hayo.

“Mtumbwi ulikuwa na uwezo wa kubeba watu watano tu lakini badala yake ukabeba watu 20 hii haikubaliki, hawa wameshapewa elimu na mamlaka husika kuhusu aina ya chombo kinachotakiwa kubeba abiria lakini mimi pia niliwahi kupiga marufuku mitumbwi ya uvuvi kutumika kubeba abiria,” amesema Dk Naano.

Septemba 15,2024 saa moja usiku,  mtumbwi huo uliokuwa umebeba watu wakitoka kwenye harusi katika Kijiji cha Mwiruruma ulizama ziwani ukiwa unaelekea Kitongoji cha Bulomba Kijiji cha Igundu.

Watu hao ambao walikuwa ndugu, jamaa  na marafiki wa bwana harusi walikuwa wakirejea nyumbani kwa ajili ya maandalizi ya harusi kwa upande wa bwana harusi sherehe iliyopangwa kufanyika Septemba 16,2024 kijijini Igundu.

Mtumbwi huo uliopigwa na wimbi na kupasuka kisha maji kujaa ndani kabla ya kubinuliwa na kuwamwaga watu  ziwani, ulikumbwa na hali hiyo takriban kilomita 1.5 kabla ya kufika katika ufukwe wa Kijiji cha Igundu.

Hili ni tukio la pili kutokea ndani ya miezi 14,  Julai 30,2023 mitumbwi miwili ilizama na kuua watoto 14 wakiwamo wanafunzi 13 wa Shule ya Msingi Bulomba.

Related Posts