Chini ya mti wa mwembe amekaa Rose Daniel akiwa ameshika simu ya mkononi, akiangalia ujumbe mfupi wa maneno aliotumiwa na mwalimu wa mwanawe.
Lakini kwa kuwa hafahamu kusoma na kuandika, inambidi amsubiri mwanawe huyo aje amsomee ujumbe huo, ambao hajui umeandikwa na nani wala unazungumza nini.
Rose ni miongoni mwa maelfu ya Watanzania wasiojua kusoma na kuandika kwa kuwa wao hawana uelewa huo.
Ripoti iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco), inaonyesha kuwa watu wazima milioni 754 hawajui kusoma wala kuandika, huku changamoto ikionekana zaidi katika nchi za Kusini mwa bara la Asia na Kusini mwa jangwa la Sahara.
Kwa upande wa Tanzania, takwimu za sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), zinaonyesha kuwa asilimia 17 ya Watanzania hawajui kusoma wala kuandika, huku Mkoa wa Tabora ukiwa na idadi kubwa ya watu wasiojua kusoma na kuandika.
Takwimu hizo zinaonyesha mikoa mitano inayoshika nafasi ya mwisho ni Tabora yenye asilimia 32 ya watu wasiojua kusoma na kuandika, ikifuatiwa na Katavi (29.6), Rukwa (25.9), Simiyu (25) na Dodoma (24).
Kwa upande wa vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24, takwimu hizo zinaonyesha wapo milioni 10.45 hukua asilimia 11.7 wakiwa mbumbumbu.
Lakini kwa upande wa mikoa inayoongoza kuwa na idadi ndogo ya watu wazima (miaka 15 na kuendelea) wasiojua kusoma na kuandika ni Dar es Salaam yenye asilimia 2.5, Mjini Magharibi (3.8), Kilimanjaro (5.8), Kusini Unguja (6.1) na Njombe (10).
Hata hivyo, sensa hiyo inaonyesha kuwa kiwango cha watu kutojua kusoma na kuandika kwa watu wazima kimepungua kutoka asilimia 21.9 mwaka 2012 hadi asilimia 17 mwaka 2022.
Takwimu hizo zinaonyesha kuwa kiwango cha kujua kusoma na kuandika ni kikubwa na kiko kwa asilimia 86.8 kwa wanaume ikilinganishwa na wanawake ambao ni asilimia 79.5.
Mwalimu wa Shule ya Msingi Kongwa Wilayani Kongwa, Mkoa wa Dodoma, Pendo Benjamin anasema kutokujua kuandika na kusoma, kunawafanya watu walio wengi kushindwa kujikomboa kifkra na kiuchumi.
kwa sababu wanalazimika kuwatumia wengine kuwasaidia kusoma na kuandika, anasema inawanyima faragha ya kuwa na mawasiliano yao wenyewe.
“Hapo inambidi mtu kusomewa na kuandikiwa na mtu mwingine, hapo hakuna faragha tena. Kila kitu kinakuwa wazi kwa mtu wa tatu. Na hili linawanyima fursa pia ya kujifunza mambo mengine kwa kusoma,”anasema.
Anasema mtu anapokuwa hajui mambo hayo kunawafanya kuwa wajinga na wanakuwa kama watu waliopo kwenye giza nene.
“Huelewi kuwa dunia inaenda wapi, wenzako wanafanya nini. Hata uwezo wa ushiriki wako katika mambo mbalimbali katika maendeleo na hata kwenye soko la ajira unakuwa ni mdogo,”anasema.
Anasema kutokujua kusoma na kuandika kuna athari hasi katika masuala mengine ya kiafya, malezi na maendeleo.
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Dk Lutengano Mwinuka anasema kwa karne ya sasa watu wengi wanamiliki simu za mkononi ambazo wanazitumia kutumiana ujumbe na taarifa mbalimbali za kibiashara na masoko.
“Mtu anapojua kusoma anaweza kuelewa hiki ni nini. Kwa maana kuna watu wengine wanaweza wasikwambie jambo kwa kuongea lakini wakakutumia kwa njia ya ujumbe mfupi wa maneno (SMS), kama unajua inaweza kukusaidia kutafsiri na kuchukua ujumbe,”anasema.
Anasema kwa kujua kusoma na kuandika ina maana kubwa duniani katika kuhudumiwa, kujihudumia na hata katika masuala ya maendeleo kwa sababu vyote hivi vinategemeana kwenye kufanya maisha yasonge mbele.
Kinachosababisha mbumbumbu na dawa yake
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) Dk Paul Loisulie anasema miongoni mwa sababu za watu kutojua kusoma na kuandika, ni ama wakiwa wadogo kutopata fursa ya kwenda shule au walipata lakini hawakujifunza.
Anasema ndio maana inatokea wanafunzi wanamaliza darasa la saba bila kujua kusoma wala kuandika.
“Wapo ambao hawakuhangaika na fursa ya elimu ya watu wazima iliyopo ili angalau wajue kusoma na kuandika. Lakini wengi wasiojua kusoma na kuandika ni wale ambao hawakwenda shule,”anasema.
Anasema kinachotakiwa ni kutatua changamoto hizo kuanzia chini kwa kutoa msisitizo mkubwa kwa watoto kupelekwa shuleni kwa wakati mwafaka.
Anasema hiyo itasaidia miaka inayokuja Tanzania, kutoendelea kuwa na idadi kubwa ya watu wasiojua kusoma na kuandika.
Pia Dk Loisulia anataka walimu kujitahidi kuwafundisha wanafunzi ili wajue kusoma na kuandika na jamii iendelee kusisitiza umuhimu wa elimu ya watu wazima kwa waliokosa fursa wakiwa wadogo.
Mwalimu Ancetilius Lumo anasema hatua ya kwanza ni kuwabaini wote wasiojua kusoma wala kuandika na kisha kurejesha kisomo cha watu wazima kama ilivyokuwa wakati wa Serikali ya awamu ya kwanza.
“Kwa kuwa sasa hivi kuwapata inakuwa ni vigumu, njia itakayosaidia ni kuhakikisha watoto wote wanaanza shule kwa wakati na kumaliza wote. Hii ya kutojua kusoma na kuandika, inatokea kwa kuwa kuna mdondoko hapa kati kuna baadhi wanafunzi hawamalizi shule kulingana na changamoto mbalimbali za maisha,”anasema.
Anazitaja changamoto hizo zinazosababisha mdondoko na kusababisha wasiojua kusoma na kuandika ni wazazi kuachana, ukosefu wa chakula, usimamizi wa upande mmoja wa wazazi, watoto kutelekezwa na wazazi wao na kukosa huduma za chakula shuleni na za kielimu.
Kuhusu mtoto wa kidato cha pili kutojua kusoma na kuandika, Lumo anasema watoto wanaokatiza masomo wakiwa madarasa ya chini na kukosa mwendelezo mzuri, baada ya miaka 10 ama 15, wanashindwa kusoma wala kuandika.
“Akishakaa muda huo, matokeo yake anakwenda katika uchaguzi hawezi kupiga kura hadi asaidiwe. Watoto wakisimamiwa vizuri wakabaki shule, jamii ikawezesha watoto kupata chakula na mahitaji yao vizuri, na tukawa na walimu wa kutosha tutaepukana na changamoto hii,”anasema.
Anasema sasa hivi Serikali imewezesha ujenzi wa miundombinu mizuri ya elimu kwa kiasi kikubwa, hivyo changamoto ipo kwa jamii kutoa msukumo kwa watoto kwenda shuleni.
Lumo anasema sababu nyingine ni wanafunzi kutumia Kiswahili kujifunza hivyo wanapofika katika shule za sekondari na kukutana na kingereza wanashindwa kusoma.
Aidha, anasema misingi ya elimu haikuwa mizuri, hivyo kuzalisha baadhi ya watu wasiojua kusoma na kuandika, lakini kwa sasa anaamini baada ya miaka minne ijayo, wanafunzi watakapoenda kuishia darasa la sita mambo hayo yatabadilika.
Kwa upande wake, Mwalimu Shule ya Msingi Mayamaya Rahma Said anasema wengine wanashindwa kujua kusoma na kuandika kutokana na kuathiriwa na lugha mama, hivyo ni vyema kukafanyika utafiti katika maeneo yanayoonekana kuwa yana idadi kubwa ya watu wasiojua kusoma na kuandika.
Anasema baada ya utafiti huo Serikali itajua ni sababu zipi kama ni kuathiriwa kwa lugha mama basi watumike wakalimani wanaotokana na makabila yao, watakaowasaidia kuwafundisha ili wafahamu kusoma na kuandika.
“Pia sio mbaya kama watawapa fursa ya kutembelea maeneo mengine ili kujifunza wenzao waliofanikiwa kuwa na idadi kubwa ya watu wanaojua kusoma na kuandika. Hili litawatia hamasa ya kujifunza zaidi ili nao waweze kujua,”anasema.
Septemba 4, 2024, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga alisema wataanzisha madarasa ya watu wasiojua kusoma na kuandika ili kuondoa changamoto hiyo.
Kipanga alisema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu Shally Raymond bungeni jijini Dodoma, ambaye aliuliza kuhusu wanafunzi wanaomaliza darasa la saba lakini hawajui kusoma wala kuandika.
“Kwa kuwa hilo ni takwa maalumu katika nchi yetu. Je Serikali iko tayari sasa kurejesha ule mpango wa kutoa elimu na madarasa ya jioni kwa watu wazima ambao hawakufanikiwa kujifunza kusoma na kuandika katika shule ya msingi,”alihoji mbunge huyo.
Akijibu swali hilo, Kipanga alisema katika matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, sasa hivi idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika nchini ni asilimia 17.
Alisema kuwa asilimia hiyo imeshuka kutoka asilimia 22 ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012.
“Lakini tunasema kuwa asilimia hii kuwa bado ipo kubwa kulingana na maisha ya sasa hivi na karne ya sasa hivi. Lakini naomba nimuondoe hofu mbunge kuwa katika maboresho ya Sera ya Elimu pamoja na mitalaa tuliyoifanya mwaka jana jambo hili limezingatiwa,”alisema.
Alisema katika halmashauri zote wameanzisha idara pamoja na vitengo vya elimu ya watu wazima, kwa maana ya elimu ya msingi na sekondari na kuteua maofisa elimu katika maeneo hayo.
Alisema wanatarajia kuanzisha madarasa katika kata na vijiji vyote, huku maofisa hao wakiwa wasimamizi wa elimu hiyo.
Nyongeza na Johnson James
Kama una maoni kuhusu habari hii tuandikie kupitia Whatsapp 0765864917.