Dar es Salaam. Jeshi la Polisi limemwita Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika kwa ajili ya kumhoji kuhusu mauaji ya kada wa chama hicho, Ali Kibao.
Kada huyo alitekwa na watu wasiojulikana Septemba 6, 2024 akiwa safarini kutoka Dar es Salaam kuelekea mkoani Tanga kwa basi la Tashriff na Septemba 8 alikutwa akiwa ameuawa eneo la Ununio.
Mnyika akizungumza na waandishi wa habari Septemba 7, katika ofisi za makao makuu ya chama hicho, alisema taarifa za kutekwa kwa Kibao zilianza kusambaa Septemba 6, 2024 kupitia mitandao ya kijamii ikidaiwa saa 12.00 jioni.
Alisema kada huyo alichukuliwa na watu wasiojulikana waliokuja na magari mawili yaliyosimamisha basi la Tashriff eneo la Tegeta Dar es Salaam.
Siku hiyo hiyo, Msemaji wa Jeshi la Polisi David Misime alisema wanalifuatilia suala hilo.
Barua ya polisi iliyotolewa jana Septemba 16, 2024 na Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kinondoni, Davis Msangi yenye kichwa cha ‘wito wa kufika polisi’ imetaja kosa la mauaji ya marehemu Ali Kibao.
Barua imesema wito huo ni kwa mujibu wa kifungu cha 10(2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai sura ya 20 R.E 2022 na kifungu cha 32 cha Sheria ya Jeshi la Polisi na Polisi Wasaidizi Sura ya 322.
“Ili kukamilisha uchunguzi nimelazimika kukuita kwa ajili ya mahojiano, kwani kuna masuala ambayo wewe unayafahamu yanayoweza kusaidia katika upelelezi wa shauri hili.
“Fika ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa makosa ya jinai Mkoa wa Kipolisi Kinondoni tarehe 18/09/2024 saa nne asubuhi bila kukosa,” inaeleza barua hiyo.
Taarifa za kuitwa kwa Mnyika zilithibitishwa na Wakili wa Chadema, Hekima Mwasipu Septemba 12, 2024 akisema waliletewa taarifa na polisi za wito huo