Morogoro yaja na maonesho ya kilimo biashara

Morogoro. Mkoa wa Morogoro umeanzisha maonyesho ya kilimo biashara yatakayotambulika kama Samia Kilimo Biashara Expo, lengo likiwa ni kuhamasisha uzalishaji wa mazao ya chakula na lishe hapa nchini.

Morogoro ni moja kati ya mikoa inayotegemewa katika kufikia lengo la kuwa na usalama wa chakula na lishe hali, hilo limeufanya uongozi wa mkoa huo kuandaa maonyeshao hayo yatakayowakutanisha wadau mbalimbali.

Maonyesho hayo yatakayoanza Oktoba 6 hadi 12, 2024 katika Wilaya ya Gairo mkoani humo, yatakuwa ni ya msimu wa tatu na yanatarajia kuwatanisha wadau mbalimbali katika mnyororo wa thamani wa sekta ya kilimo, mifugo na mazingira.

Wadau wanaotarajiwa kushiriki ni wakulima, wafugaji, wauzaji na wazalishaji wa pembejeo za kilimo na mifugo, taasisi za utafiti wa kilimo na mifugo pamoja na taasisi za fedha.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Jabir Makame ameeleza lengo la maonesho hayo ni kutekeleza maono ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo na mifugo kupitia mkakati unaolenga kuongeza tija katika sekta ya kilimo kufikia asilimia 10 kutoka asilimia 4.2 ya mwaka 2023.

Makame ameeleza kuwa maonyesho hayo yatasaidia wakulima kupata huduma na kujifunza teknolojia ili kuleta tija katika sekta ya kilimo na mifugo.

“Dira na mikakati ya mkoa kwa Wilaya ya Gairo ni kuwasaidia wakulima kulima na kufuga kwa tija kupitia mazao yao ya asili ambayo wamekuwa wakilima kwa muda mrefu sambamba na mazao mapya ya kimkakati yakiwamo parachichi, viazi mviringo na tumbaku, ikiwa ni nyenzo muhimu ya kukuza pato la mkulima mmoja mmoja ili kuondoa na kukuza uchumi wa wilaya na kuongeza ukusanyaji wa mapato,” amesema Makame.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima ameeleza kupitia maonyesho hayo, huu ni wakati wa wakulima na wafugaji kufanya shughuli zao kwa tija ili kuendelea kuongeza kipato chao na kuinua sekta hiyo kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuweka mipango itakayosaidia kubadilisha kilimo kuwa biashara.

Malima ameeleza kuwa kuna umuhimu wa wadau wa kilimo kushirikiana na wakulima na wafugaji ili kuboresha mazingira ya sekta ya kilimo na mifugo pamoja na kudhibiti uharibifu wa mazingira ili mazingira yaweze kutoa mazao yenye tija.

“Mara nyingi watu wanafikiri tunaposema kilimo biashara tunamaanisha yale mazao ya biashara, lakini maana yake ni kilimo anacholima mtu kikutoshe kwanza kufidia mahitaji yako ya msingi ya kila siku halafu unabakia na ziada,” amesema Malima.

Maonesho ya Samia Kilimo Biashara Expo 2024 yatabeba ajenda kuu tano ikiwamo ushiriki wa wananchi katika uchaguzi wa Serikali za mitaa, kilimo na ufugaji wa kibiashara, nishati safi ya kupikia,  fursa ya biashara ya kaboni (hewa ukaa), afya, lishe pamoja na ushirika wa mfumo wa stakabadhi ghalani.

Related Posts