Wagombea saba akiwamo mwanamke kutoka Afrika, wamejitosa katika kinyang’anyiro cha kukalia kiti cha rais wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki, (OIC), nafasi inayotajwa kuwa bora zaidi katika ulimwengu wa michezo. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa … (endelea).
OIC imetangaza majina ya wagombea hao jana Jumatatu na uchaguzi wa kura ya siri utafanyika Machi mwakani.
Atakayeibuka kidedea atachukua nafasi ya wakili Thomas Bach, wa Ujerumani ambaye atahitimisha ngwe yake ya miaka 12 ya uongozi Juni mwakani.
Inaelezwa kuwa Rais wa 10 wa IOC anaweza kuwa kwa mara ya kwanza mwanamke na kutokana na walioomba kugombea kiti hicho, bosi mpya atotekea Afrika, Asia au Uingereza.
Kirsty Coventry ni mwanamke pekee kutoka Zimbabwe, aliyeingia kwenye kinyang’anyiro cha kuongoza shirika hilo ambalo limekuwa na marais wanaume pekee katika historia yake ya miaka 130. Marais wanane kati ya hao walitoka Ulaya na mmoja kutoka Marekani.
Wanaochuana na Kirsty ni Sebastian Coe anayepewa nafasi kubwa ya kuibuka kidedea, Mwanamfalme Feisal al Hussein wa Jordan, Juan Antonio Samaranch, David Lappartient, Morinari Watanabe na Johan Eliasch.
Pamoja na kwamba Coe anapewa nafasi ya kukalia kiti hicho, ushindani mkali anaupata kutoka kwa mwanamama Kirsty Coventry, ambaye rekodi zinaonesha ameshinda medali nyingi zaidi za Olimpiki kuliko muogeleaji yeyote wa kike katika historia.
Anatajwa pia ndiye mwanariadha aliyefanikiwa zaidi wa Olimpiki barani Afrika. Katika Olimpiki ya Majira ya 2004 huko Athens, Coventry alishinda medali ya dhahabu, fedha na shaba; mashindano ya Olimpiki ya majira ya joto ya 2008 yaliyofanyika jijini Beijing, alishinda medali za dhahabu na tatu za fedha.
Pia ameshikilia rekodi tano za dunia. Yeye ni mwanachama wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) na mapema 2018, alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa Tume ya Wanariadha wa IOC, chombo kinachowakilisha wanariadha wote wa Olimpiki ulimwenguni.
Tangu Septemba 2018, Coventry ni Waziri wa Vijana, Michezo, Sanaa na Burudani katika Baraza la Mawaziri la Zimbabwe.