Dar es Salaam. Kukua kwa idadi ya watu kusikoendana na kuwapo kwa ongezeko la shughuli za kujiingizia kipato, kumetajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazochochea ongezeko la matukio ya uhalifu visiwani Zanzibar.
Pia wadau wanaeleza huenda matukio hayo yanaonekana kuongezeka kutokana na uelewa wa watu kukua katika kuripoti, badala ya kuamua kubaki nayo wenywe.
Hayo yanaelezwa wakati ambao Ripoti ya Zanzibar Abstract ya mwaka 2023 iliyotolewa na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali (OCGS) 2023 kuonyesha kuwapo kwa ongezeko la matukio ya uhalifu dhidi ya mali na yale yaliyofanywa dhidi ya watu.
Ripoti hiyo inaonyeshamatukio uhalifu dhidi ya mali ndani ya mwaka mmoja yameongezeka kutoka 1,947 mwaka 2022 hadi kufikia matukio 9,345 mwaka 2023, wakati ambao uhalifu dhidi ya watu ukiongezeka kutoka matukio 1,421 hadi 2,049, mtawaliwa.
Katika matukio dhidi ya mali matukio ya wizi ndiyo yanaoongoza kwa kuripotiwa kuongezeka kutoka 344 mwaka 2022 hadi matukio 7,075 mwaka 2023. Wizi wa mazao nao uliripotiwa kuongezeka kutoka matukio 267 hadi 702 mwaka jana.
Matukio ya wizi wa pikipiki nao ulifikia 334 kutoka matukio 176 yaliyokuwapo mwaka juzi.
Katika matukio dhidi ya watu yanaoongoza kwa kuripotiwa, ni ubakaji kwa wasichana wenye umri chini ya miaka 18 ambapo matukio yaliyoripotiwa yalitoka 585 hadi kufikia 824 mwaka jana. Mashambulizi yakitoka matukio 125 hadi 376 yaliyoripotiwa.
Akizungumzia suala hilo, mtaalamu wa uchumi, Oscar Mkude amesema wakati mwingine ongezeko la matukio ya uhalifu hushuhudia kutokana na kiwango cha uelewa wa watu kutoa taarifa polisi kukua.
Hiyo inatokana na wao kujifunza kwa njia mbalimbali, ikiwemo elimu inayotolewa na Jeshi la Polisi na hata vyombo vya habari.
“Lakini pia huenda hali hii ikachochewa na ukuaji wa jamii, ukuaji ambao wakati mwingine hauendani na ukuaji wa shughuli za kiuchumi na ukizingatia hiki ni kipindi ambacho watu walio katika umri wa kufanya kazi ndiyo wanaongoza kuwa wengi kwa mujibu wa sensa,” amesema.
Amesema kukosekana kwa shughuli za kiuchumi huenda ikawa sababu ya watu kuamua kujiingiza katika matukio ya uhalifu.
Uwepo wa matukio haya hasa yanayohusisha wizi wa mali, kwa mujibu wa Mkude yamekuwa yakiwarudisha watu nyuma katika maendeleo ya mtu mmoja mmoja, kwani badala ya kuwekeza fedha zake katika shughuli nyingine analazimika kununua kitu kilichoibiwa kwa ajili ya matumizi yake.
Wakati Mkude akisema hayo, hata ripoti ya hali ya uhalifu Tanzania ya mwaka 2023 inayonyesha ongezeko la matukio ya uhalifu upande wa Tanzana Bara na visiwani.
Ripoti hiyo kwa ujumla inataja kukosekana kwa shughuli rasmi za kujiingizia kipato kuwa sababu za kuwapo kwa matukio hayo.
Jeshi la polisi Tanzania katika ripoti hiyo ilitaja pia hali duni za kiuchumi, kukosa maadili, ukuaji wa miji, utandawazi, tofauti kubwa ya hali ya maisha kati ya walionacho na wasionacho na ukosefu wa ajira.
Kwa vijana, tamaa ya kumiliki mali kuwa sababu za kuwapo kwa matukio kama wizi, wizi wa mali mbalimbali na hata uvunjaji.
“Katika kushughulikia hili Jeshi la Polisi linaendelea kuhamasisha jamii hususan vijana kushiriki katika shughuli halali za ujasiriamali na uchumi, ili kujipatia kipato sambamba na kuzishawishi taasisi za fedha zipunguze urasimu wa upatikanaji wa mikopo nafuu na kupunguza riba kubwa zinazotozwa katika mikopo hiyo,” imeeleza mikakati ya jeshi hilo.
Kuwepo na mipango endelevu ya utoaji elimu kwa umma hususan elimu ya ujasiriamali, kuhamasisha jamii ijenge utamaduni na utaratibu wa kutoa taarifa kwa wakati kwenye vyombo vya dola wanapobaini viashiria vya uhalifu.
“Pia kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuibua fursa kwa vijana, ili kujipatia kipato na kuepukana na vishawishi vya kujiingiza kwenye uhalifu,” imeeleza ripoti hiyo.
Katika matukio dhidi ya watu, ikiwemo ubakaji na ulawiti, Jeshi la Polisi limeainisha kuwa litaendelea kushirikisha na taasisi za kidini na wadau mbalimbali katika kuhamasisha jamii ili kuachana naimani potofu za kishirikina.
“Katika hili Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi Na Teknolojia pamoja na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalumu, kutenga muda maalumu shuleni wa kutoa elimu ya ulinzi wa fikra kwa watoto, ili watambue viashiria vya watu wenye nia mbaya,” imeeleza ripoti hiyo.
Katika hili, mchambuzi wa uchumi, Dk Balozi Morwa amesema kukosekana kwa usimamizi mzuri wa utawala wa sheria, kusimamia masuala ya rushwa na uhalifu huenda ikawa moja ya sababu ya kuwapo kwa matukio haya.
Amesema kuendelea kuwapo kwake kunapunguza uzalishaji mali hali inayofanya kupungua kwa ukuaji wa uchumi, kwani hakuna bidhaa inayoingia sokoni kwa ajili ya kuuzwa.
“Kama unashindwa kuzalisha sokoni hakuna kitu kinachozalishwa na hakuna ukuaji wa uchumi,” amesema Dk Morwa.
Ili kushughulikia hilo, ameshauri ni muhimu kuendelea kuweka msisitizo juu ya mpango wa uzazi, ili kila mtu atambue wajibu wa malezi aliyonayo kwa watoto anaowaleta duniani.