Silinde ataja BBT inavyowabeba vijana

Mbeya. Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau kuwekeza kwenye sekta ya kilimo kupitia miradi ya kimkakati chini ya Programu ya Kujenga Kesho iliyo Bora (BBT).

Pamoja na hayo, Silinde amewataka wadau wa kilimo kuongeza juhudi za kuwafikia vijana wengi zaidi katika maeneo ambayo imewekeza ya mashamba makubwa kwa ajili ya kutekeleza programu hiyo ya BBT.

Silinde ametoa kauli hiyo leo Jumanne, Septemba 17, 2024, alipokuwa akikabidhi vifaa kwa vijana 105 wanaojihusisha na kilimo kupitia mradi wa kuimarisha sekta binafsi unaotekelezwa na Kampuni ya Kibanza kwa ufadhili wa Shirika la Watu wa Marekani (USAID) katika wilaya za Mbeya, Mbarali na Chunya.

“Jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta binafsi zimeleta mafanikio makubwa katika kuongeza thamani ya mazao, sambamba na ushiriki wa USAID kupitia mradi wa Feed the Future,” amesema Silinde.

Aidha, amewahamasisha vijana kutumia fursa zinazotolewa na sekta ya kilimo, akisisitiza kuwa mikoa ya Mbeya na Songwe imekuwa kitovu cha Wizara ya Kilimo katika uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.

“Serikali imewekeza katika mashamba makubwa kupitia mradi wa BBT, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya, imetenga hekari 57,000 kwa ajili ya kilimo,” amesema naibu waziri huyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Kibanza, Jumanne Sanga amesema vijana 502 wamepewa mafunzo ya usindikaji wa bidhaa pamoja na elimu juu ya mabadiliko ya tabianchi na matumizi bora ya unyevu kwenye uzalishaji.

Amesema lengo ni kuwawezesha vijana kuongeza thamani ya mazao yao na kutumia mbinu mbalimbali za kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

Imeelezwa kuwa vijana 30,000 tayari wamefikiwa na mradi huo katika mikoa mbalimbali, ikiwamo Mbeya, Iringa na Morogoro, huku vijana 15,000 wakipata ajira. Aidha, vijana 3,000 wanatarajiwa kunufaika na mkopo wa Sh4.6 bilioni kupitia mradi wa Feed the Future ifikapo mwaka 2027.

Mnufaika wa mradi huo, Mariam Mkisi anayejishughulisha na usindikaji wa pilipili, amesema mradi huo umemsaidia kuunganishwa na masoko makubwa ya ndani na nje ya nchi kwa ajili ya usambazaji wa bidhaa zake.

Related Posts