Tanzania kuzindua nembo ya asali kuvutia soko la kimataifa

Dar es Salaam. Tanzania ipo mbioni kuzindua nembo ya asali zinazozalishwa nchini, ili kuitambulisha bidhaa hiyo muhimu katika soko la kimataifa.

Uzinduzi huo mbali ya kuitambulisha asali ya Tanzania katika soko la kimataifa, umetajwa pia kuwa uthibitisho wa ubora wa asali na nta zinazozalishwa hapa nchini.

Mpango huo utazinduliwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Pindi Chana Oktoba 4, 2024 mkoani Tabora katika Taasisi ya Mafunzo ya Ufugaji Nyuki.

Mpango huo unafadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) na kutekelezwa kwa pamoja na Shirika la Maendeleo la Ubelgiji (Enabel) na Kituo cha Biashara cha Kimataifa (ITC).

Aidha, uzinduzi huo utaenda sambamba na uwekaji wa jiwe la msingi kwa ajili ya hosteli ya wanawake katika taasisi hiyo ya ufugaji nyuki.

Akizungumzia uzinduzi huo leo Jumanne Septemba 17, 2024, Meneja wa mradi, Stephen Paul amesema:”Uzinduzi wa nembo, mbali ya kuitambulisha asali ya Tanzania katika soko la kimataifa, ni uthibitisho wa ubora wa asali na nta zinazozalishwa hapa nchini.

“Mbali na kutengeneza nembo hii ya kuaminika ya ubora, pia tunaboresha soko la bidhaa zetu za asali na kusaidia maisha ya maelfu ya wafugaji nyuki na wafanyabiashara nchini kote,” amesema.

Paul amesema nembo hiyo inasimamia na inawakilisha ubora wa hali ya juu wa asali ya Tanzania katika masoko ya ndani na ya kimataifa.

Amesema kama taasisi ya Serikali yenye jukumu la kuendeleza biashara ya bidhaa zote za Tanzania, Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara ya Tanzania (Tantrade) inasimamia nembo hiyo inayomilikiwa na Serikali ya Tanzania, ili kuitangaza asali yetu kimataifa.

“Hii itakuwa ni ishara ya asali yenye ubora na viwango vya juu kwa watumiaji wanaotafuta bidhaa za asali za Tanzania,” amesema.

Kwa upande wake, Latifa Khamis, Mkurugenzi Mkuu wa Tantrade, amesema umuhimu wa mpango huo kwa ukuaji wa kiuchumi wa Tanzania: “Tantrade imedhamiria kuunga mkono wazalishaji wetu wa ndani na kuhakikisha asali ya Tanzania inatambuliwa na kuthaminiwa duniani kote.

“Kupitia nembo hii, tunatoa fursa mpya kwa wafugaji nyuki wetu na kuchangia katika malengo ya kukuza uchumi na upanuzi wa masoko,” amesema.

Katika kuelekea uzinduzi huo hadi sasa maandalizi kwa ajili ya mpango huo yamekamilika, ikiwa ni hatua muhimu pia kukuza hatua zote muhimu za mnyororo wa thamani ya ufugaji nyuki kupitia (Bevac- Beeking Value Chain).

Mpaka sasa, wanufaika 4151 wakiwemo  wafanyabiashara 38, wafugaji nyuki 4113 na wauzaji wa nje wengi wamepata msaada, ikiwa ni pamoja na rasilimali na uunganishaji wa masoko, kuwasaidia kustawi katika masoko ya ndani na ya kimataifa.

Related Posts