TRA SHINYANGA:LIPENI KODI MLIZOKADIRIWA PAMOJA NA MALIMBIKIZO YOTE KABLA YA SEPTEMBA 30,2024

Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Shinyanga, Josephat Mwaipaja akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Septemba 17,2024

Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Shinyanga imewahimiza Walipa Kodi wote kulipa kodi walizokadiriwa pamoja na malimbikizo yote kabla ya Septemba 30,2024 ili kuepuka riba baada ya kipindi hicho.

Rai hiyo imetolewa leo Jumanne Septemba 17,2024 na Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Shinyanga, Josephat Mwaipaja wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu Uwasilishwaji wa Ritani na Malipo ya Kodi ya Mapato awamu ya tatu.

 

“Mwezi Septemba ni mwezi muhimu katika makusanyo ya kodi kwani ni mwezi wa malipo ya kodi kwa awamu ya tatu kwa mwaka huu wa 2024/2025. Ni kipindi ambacho kodi nyingi zinapaswa kulipwa, anayechelewa kulipa kodi atalazimika kulipa riba kuanzia mwezi Oktoba hivyo nichukue nafasi hii kuwahimiza wafanyabiashara wote kuhakikisha wanatimiza wajibu waowa kulipa kodi ya awamu ya tatu pamoja na malimbikizo yote ya kodi wanayodaiwa kabla ya tarehe 30.09.2024”,amesema Mwaipaja.

Katika hatua nyingine amewataka wafanyabiashara kutunza kumbukumbu za biashara ili kupata makadirio sahihi ya kodi na kupunguza malalamiko ya makadirio ya kodi.

“Tunaendelea kuwakumbusha walipakodi kuhakikisha wanatoa risiti za EFD wanapouza bidhaa au huduma na pia wanunuzi wa bidhaa au huduma wahakikishe wanadai risiti zenye thamani sawa na pesa waliyotoa wakati wa kununua bidhaa au huduma”,ameeleza Mwaipaja.

Mwaipaja amesema TRA Mkoa wa Shinyanga imeendelea kufikia malengo ya ukusanyaji kodi ambapo kwa kipindi cha 2023/2024 imefanikiwa kukusanya kodi kwa asilimia 124.

Katika hatua nyingine amebainisha kuwa, Kampeni mbalimbali za mlango kwa mlango zimekuwa na manufaa makubwa katika ukusanyaji mapato ya serikali ambapo TRA imejenga ukaribu na walipakodi, imezijua biashara zao, imetoa elimu kwa walipa kodi kulingana na aina za biashara, imetoa huduma za makadirio, kupokea mrejesho juu ya huduma za TRA pamoja na kuongeza mapato kwa serikali.

Aidha amesema TRA imetenga siku ya Alhamisi kwa ajili ya kuwasikiliza walipa kodi ili kupokea kero,malalamiko na maoni mbalimbali huku akizitaja namba za mawasiliano ya TRA Mkoa wa Shinyanga kuwa ni 0677050546, 0677050545 au 0677050544.

Kodi ni mchango wa lazima ambapo mtu, taasisi au kampuni ambayo ni raia au siyo raia hupaswa kulipa kwa serikali kwa mujibu wa sharia bila kutarajia kupata bidhaa au huduma inayolingana na fedha inayolipwa.

Kodi huipatia uwezo serikali kutekeleza miradi iliyopangwa kwa ajili ya wananchi kama vile shule,hospitali, huduma za kiuchumi, umeme, barabara, huduma za ulinzi na usalama na huduma za kiutawala.

Ukadiriaji wa kodi ni shughuli inayofanya mlipakodi kufahamu kiasi cha kodi kulingana na kumbukumbu za mlipakodi zilizopo ambapo Malipo ya kodi yalikadiriwa hufanyika kwa awamu nne (Machi, Juni, Septemba, Desemba).

Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Shinyanga, Josephat Mwaipaja akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Septemba 17,2024. Picha na Kadama Malunde – Malunde 1 blog

Related Posts