Uchimbaji madini ya kinywe waiva Mahenge, Sh790 bilioni kutumika

Dar es Salaam. Hatimaye mchakato wa kuchimbwa madini ya kinywe yanayotumika kutengeneza betri umefikia pazuri, baada ya Sh790 bilioni kupatikana kwa ajili ya utekelezaji wa kazi hiyo katika awamu ya kwanza ya mradi.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya kukamilika kwa utiaji saini makubaliano ya kuanza mradi kati ya Benki ya CRDB, Kampuni ya Faru Graphite Corporation, Benki ya Maendeleo ya Afrika Kusini (DBSA) na Shirika la Maendeleo la Viwanda la Afrika Kusini (IDC).

Mradi huo wa uchimbaji madini utakaofanyika Mhenge wilayani Kilombero katika Mkoa wa Morogoro, unatarajiwa kutekelezwa na Kampuni ya Faru Graphite Corporation.

Akizungumza wakati wa hafla ya kusaini makubiano ya utekelezaji wa mradi huo Septemba 16, 2024, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema kati ya Sh790 bilioni, benki hiyo imetoa Sh66 milioni katika awamu ya kwanza.

Sambamba na kutoa fedha hiyo, amesema imepewa jukumu la kusimamia uwezeshaji wa kifedha, akaunti kuu ya mradi na dhamana zote.

Amesema mradi huo mbali na kuwezesha kutoa madini muhimu, pia utazalisha ajira, kuimarisha miundombinu na fursa ya biashara.

Ameeleza ushiriki wa CRDB ni ishara ya uwezo wa benki za ndani kufanikisha miradi mikubwa inayotekelezwa nchini, uimara wa ushirikiano na taasisi nyingine za fedha Afrika na kimataifa.

Mbali na benki hiyo, mradi huo unahusisha pia Benki ya Maendeleo ya Afrika Kusini (DBSA) itakayochangia Dola 59.6 milioni na Shirika la Maendeleo la Viwanda (IDC) la Afrika Kusini litatoa Dola 53.4milioni.

Akizungumza hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Blackrock inayomiliki asilimia 86 ya hisa za Kampuni ya Faru Graphite Corporation, John de Vries alisema hiyo ni hatua kubwa.

“Kukamilika kwa mchakato huu ni hatua kubwa kuelekea uendelezaji wake kwa manufaa ya wadau wote,” amesema.

Amesema mradi huo, unatarajiwa kuwa wa aina yake kwa kuleta manufaa ya kiuchumi na kimazingira kwa Tanzania na dunia nzima.

Hilo linatokana na kile alichoeleza, aina ya madini yatakayochimbwa yatatoa malighafi muhimu ya utegenezaji wa betri jambo litakalosaidia kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa duniani.

Mradi huo unatarajiwa kuzalisha fursa za ajira 500, kadhalika kuchochea ujenzi wa njia ya umeme yenye kilovolti 220 kutoka Kituo cha Umeme cha Ifakara hadi eneo la Mahenge.

Umeme huo utagawiwa kwa vijiji vya karibu katika wilaya za Mahenge, Ulanga na kutoa fursa za biashara kwa wasambazaji wa ndani, watoa huduma na makandarasi mkoani Morogoro na nchini kote.

Related Posts