Zaidi ya watu 12 wamethibitishwa kufariki katika mataifa ya Austria, Poland, Jamhuri ya Czech na Romania kutokana na mafuriko yaliyoikumbia nchi hizo mwishoni mwa wiki huku idadi ya vifo ikitarajiwa kuongezeka.
Sehemu kubwa ya barabara na baadhi ya nyumba katika mataifa yalioathirika na mafuriko zimefunikwa na maji huku mito ikivunja kingo zake.
Soma pia: Zaidi ya watu 500 wafariki kufuatia mvua na mafuriko mabaya kanda ya Afrika Magharibi na Kati
Nchini Poland, mamlaka zimesema kuwa wanaume watatu na mwanamke mmoja wamepoteza maisha katika maeneo tofauti yaliokumbwa na mafuriko.
Mafuriko hayo yamemshurutisha meya wa mji wa Nysa nchini Poland Kordian Kolbiarz kuwataka watu katika mji huo kuhama mara moja.
Meya huyo amewahimiza watu kuelekea maeneo salama ya nyanda za juu, akitaja kitisho cha mto ulioko karibu na mji huo kuvunja kingo zake.
Huyu ni mmoja wa waliothirika na mafuriko, “Nilipoamka, kulikuwa kumejaa maji kila mahali. Tulisubiri kuona kitakachotokea, na walikuwa wakatuokoa.”
Soma pia: Idadi ya waliokufa kwa kimbunga yafikia watu 200
Tayari watu saba wamefariki dunia nchini Romania kutokana na mafuriko hayo. Vifo pia vimeripotiwa nchini Austria, Jamhuri ya Czech na Poland.
Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk amesema serikali yake imetenga kiasi euro milioni 197 kuwasaidia wahanga wa mafuriko nchini humo na kwamba nchi hiyo itatuma maombi ya msaada zaidi wa kifedha kutoka Umoja wa Ulaya. Aidha Poland imetangaza mafuriko hayo kuwa janga la kitaifa.
Kwengineko, mito kadhaa nchini Jamhuri ya Czech inaripotiwa kufurika huku mto Danube ukivunja kingo zake nchini Slovakia na Hungary.
Maeneo ya mpakani mwa Jamhuri ya Czech na Poland pia yameshuhudia mafuriko makubwa mwishoni mwa wiki huku madaraja yakivunjika na baadhi ya nyumba zikisombwa na maji.
Mvua kubwa imenyesha nchini Jamhuri ya Czech. Katika mji wa kaskazini mashariki wa Jesenik, kiwango cha mvua milimita 473 imenyesha tangu Alhamisi, kiwango hicho cha mvua kikiwa mara tano zaidi ya wastani.
Soma pia: Scholz kutembelea maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko Bavaria
Huduma ya zima moto nchini humo imepeleka misaada kwa baadhi ya watu waliokwama vijijini huku miito ikitolewa kwa watu kutokunywa maji yanayotoka moja kwa moja kwenye mabomba au visima kutokana na uwezekano wa maji hayo kutokuwa salama kwa afya.
Idara za utabiri wa hali ya hewa zimetabiri kuwa mvua zaidi zinatarajiwa kunyesha leo nchini Austria, Jamhuri ya Czech na kusini mashariki mwa Ujerumani ambapo viwango vya mvua vinatarajiwa kupindukia milimita 100.