Arusha. Baadhi ya wazazi katika jamii ya kifugaji wilayani Longido, Mkoa wa Arusha, wanadaiwa kubadili mbinu za kukeketa watoto wadogo na sasa wanatumia sherehe za ubatizo kama kificho cha kutekeleza ukeketaji.
Aidha, inasemekana baadhi ya wazazi huzimaliza kesi hizo nyumbani, hali inayosababisha wahusika kushindwa kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Serikali imetoa onyo kwa yeyote anayeendelea kutekeleza ukatili huo, itachukua hatua kali za kisheria dhidi yao.
Hayo yameelezwa leo Jumanne, Septemba 17, 2024, na Ofisa Maendeleo wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Rashid Hussein alipokuwa akizindua mradi wa kupaza sauti kupinga ukeketaji na vitendo vya ukatili, unaotekelezwa na Shirika la Wanahabari la MAIPAC kwa ufadhili wa Shirika la Cultural Survival.
Hussein amesema baada ya Serikali kuimarisha msako wa wanaotekeleza ukeketaji, mbinu mpya zimeibuka na wamebaini hivi sasa watoto wanakeketwa kwa siri katika sherehe za ubatizo.
“Katika jamii hizi za kifugaji, ukeketaji bado ni tatizo. Tunaendelea kupambana kutokomeza vitendo hivi, lakini wahusika wanatumia mbinu mpya kila siku ili kukwepa sheria. Hivi sasa mtoto anakeketwa akiwa na miezi miwili au hata wiki moja katika sherehe za ubatizo,” amesema Hussein.
Amesema wameelekeza viongozi wa vitongoji kuhakikisha wanatoa taarifa pindi wanapobaini vitendo hivyo kwenye sherehe hizo.
Kuhusu utoaji wa taarifa, Hussein amesema baadhi ya viongozi huzimaliza kesi hizo nyumbani, hali inayoathiri juhudi za kisheria. “Serikali imeshaweka vikao na viongozi hao na kuonya kuwa watachukuliwa hatua kali iwapo watafumbia macho vitendo hivyo,” amesema ofisa huyo.
Kwa upended wake, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Longido, Dk Mathew Majani amesema wanawake wengi wa jamii ya kifugaji huwa dhaifu wanapofikishwa hospitalini kujifungua kutokana na kutopewa chakula sahihi.
“Kwa kuwa asilimia kubwa ya wanawake wa jamii hiyo wamekeketwa, wanazuiwa kula vyakula fulani ili wasipate changamoto kubwa wakati wa kujifungua, jambo ambalo ni hatari kwa afya zao,” amesema.
Dk Majani amesema ukeketaji husababisha vifo vya wanawake na watoto kutokana na kutokwa na damu nyingi pamoja na kukosa nguvu za kujifungua salama.
Mkurugenzi wa Shirika la MAIPAC, Mussa Juma amesema mradi huo umeanzishwa baada ya utafiti uliofanyika mwaka huu kubaini ukeketaji bado unaendelea katika wilaya hiyo.
“Licha ya juhudi zinazofanywa na Serikali na wadau kutaka kutokomeza mila hii potofu, lakini bado hali inaendelea. Shirika hili linatarajia kutoa elimu na kuunda kamati za vijiji kupinga ukeketaji,” amesema Juma.
Mmoja wa waathirika wa ukeketaji, Merikinoi Orkesyanye aliyeathirika na fistula kutokana na ukeketaji, ametoa wito kwa Serikali na viongozi wa mila kusitisha mila hiyo hatari kwa afya ya wanawake.
Mary Laizer, aliyekeketwa akiwa mdogo, amesema amefanikiwa kumkinga binti yake dhidi ya ukeketaji, akitoa wito wa elimu zaidi kuhusu athari za kitendo hicho.