Aliyemuua rafiki kwa kumzunguka kwa mkewe, atupwa jela miaka miwili

Sumbawanga. Mkazi wa Migazini, Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi, Mohamed Habibu amehukumiwa kifungo cha miaka miwili jela, baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumuua bila kukusudia rafiki yake, Rashid Makopa.

Kiini cha mauaji hayo yaliyotokea Aprili 16, 2024 ni kitendo cha mshtakiwa kurudi nyumbani na kumkuta rafiki yake huyo aliyekwenda nyumbani kwake kumtembelea, akiwa chumbani kwake na mkewe, huku marehemu akiwa ameshusha suruali.

Hukumu dhidi ya mshtakiwa ambaye ni maarufu kwa jina la Master Mood ilitolewa Septemba 13, 2024 na Jaji Abubakar Mrisha wa Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga na nakala yake kuwekwa jana katika mtandao wa Mahakama.

Awali, mshtakiwa huyo alikuwa akikabiliwa na kosa la kuua kwa kukusudia, lakini baadaye shtaka hilo lilibadilishwa na kuwa kuua bila kukusudia kutokana na ombi la mshtakiwa mwenyewe kupitia wakili wake, Eliud Ngao.

Ombi hilo halikupingwa na upande wa mashtaka ukiongozwa na wakili mwandamizi wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Kalistus Kapinga aliyekuwa akiwakilisha upande wa Jamhuri na Habib akakiri kosa hilo.

Kulingana na maelezo ya kosa yaliyosomwa mahakamani baada ya mshtakiwa kukiri kosa hilo, yanaeleza tukio hilo la mauaji lilitokea Aprili 16, 2024 eneo la Migazini, Wilaya ya Mpanda katika nyumba ya mshtakiwa.

Kabla ya umauti, marehemu alikuwa akiishi Kijiji cha Tuombe Mungu kilichopo Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora na kwamba marehemu na mshtakiwa walikuwa wakifahamiana na walikuwa na tabia ya kutembeleana katika nyumba ya Habib.

Siku ya tukio, marehemu alifika nyumbani kwa mshtakiwa na kumkuta mke wa rafiki yake, Shamsa Masigati na waliingia wote hadi chumbani na wakiwa huko, ghafla mshtakiwa alirejea nyumbani na kuwakuta chumbani.

Kwa mujibu wa maelezo hayo, marehemu alikuwa katika hatua za mwisho kushusha suruali yake kutokea eneo la magoti na mshtakiwa alimshambulia marehemu maeneo mbalimbali ya mwili na kumsukuma na kuanguka.

Alipoangua, aliangukia kipande cha chuma ambacho kilimjeruhi na kusababisha atokwe na damu nyingi na baadaye kupoteza maisha na mshtakiwa aliamua kwenda mwenyewe kituo cha Polisi Mpanda kutoa taarifa.

Aprili 19, 2024, mtuhumiwa alipelekwa kwa mlinzi wa amani, Theresia Masha ambapo alikiri na kufafanua kilichotokea na kwamba hakuwa na nia ovu ya kusababisha mauaji hayo.

Baada ya maelezo hayo kusomwa, mshtakiwa aliithibitishia Mahakama kuwa yalikuwa sahihi na kwamba ndivyo tukio lilivyotokea, hivyo Mahakama kumtia hatiani kwa kosa hilo kutokana na kukiri kwa kinywa chake kutenda kosa hilo.

Akiwasilisha maombolezo (mitigation) kwa niaba ya mteja wake, wakili Ngao aliomba apewe adhabu ndogo kwa sababu mbali na ukweli kuwa alikiri kosa hilo dogo na kuokoa muda wa Mahakama, alishakaa mahabusu miezi 12.

Wakili huyo alisema katika muda aliokaa gerezani ametubu na anajutia kosa hilo na kwamba mbali na hoja hiyo, lakini ana watoto 12 wanaomtegemea na hakuwa na nia ovu kusababisha kifo kama mazingira yanavyojieleza.

Hivyo, wakili huyo akasema mteja wake anastahili adhabu ndogo ili arudi nyumbani na kuendelea kuisaidia familia yake ambapo Jaji alisema hakuna ubishi kuwa mshtakiwa ndiye aliyehusika kusababisha kifo cha rafiki yake huyo.

“Kwa msingi huo hakuna namna anaweza kukwepa kupewa adhabu kutokana na kukiri mwenyewe kuwa na hatia. Hata hivyo, kwa kuzingatia maombolezo aliyoyatoa, na kwa sababu ni mkosaji wa kwanza ninatilia manani hoja zake,” amsema.

Jaji Mrisha aliendelea kusema kuwa kosa hilo lilitendeka katika mazingira ambayo lisingetendeka kama marehemu asingechangia kutendeka kwa kosa hilo, baada ya kukutwa akiwa ndani ya chumba cha mshtakiwa akiwa na mke wake.

Kulingana na Jaji, mshtakiwa anastahili adhabu ndogo hasa ikizingatiwa pia kuwa alishakaa mahabusu kwa miezi mitano ambayo ni sawa na kifungo cha gerezani, hivyo kutokana na sababu hizo, anamhukumu kifungo cha miaka miwili jela.

Jaji alisema anaamini akimaliza adhabu hiyo, atakuwa raia mwema katika jamii na kuwa balozi mzuri wa kuhamasisha wanajamii wengine juu ya umuhimu wa kuheshimu sheria za nchi na kutambua madhara ya kujichukulia sheria mkononi.

Related Posts