YANGA inaondoka saa 3:00 asubuhi ya kesho Alhamisi na itatumia masaa mawili tu kufika Unguja, Zanzibar tayari kwa mchezo wa marudiano wa raundio ya pili wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya CBE ya Ethiopia, lakini kuna mazoezi flani wameyafanya ndani ya siku mbili yamemfanya kocha Miguel Gamondi kusema sasa mabao yatafungwa.
Kama ulifika mazoezini Yanga ndani ya siku mbili jana na juzi kuna kitu kilikuwa kimekomaliwa na makocha wa timu hiyo ni umakini wa kuzuia, lakini zaidi ni mazoezi mengi ya kufunga yakiambatana na vikao mbalimbali.
Mazoezi ya kufunga yamefanyika kwa washambuliaji na hata viungo kila mmoja akiongezewa mbinu za kufunga mabao, timu hiyo ikifanyia kazi kwa umakini makosa ambayo yamewanyima ushindi mnono ugenini wikiendi iliyopita.
Kwenye mezoezi hayo washambulaiji Prince Dube, Clement Mzize na Jean Baleke walifanya makubwa kila mmoja akifunga mabao yasiyopungua matatu kwa kila kipindi cha mazoezi.
Achana na mazoezi hayo, kocha Gamondi na msaidizi wake Mussa N’dew aliyekuwa mshambuliaji hatari wa zamani, walikuwa na vikao tofauti vya washambuliaji hao wakiwatuliza presha kwa kuwajenga kisaikolojia.
Yanga itakuwa na dakika 90 za nyumbani dhidi ya CBE ili kuamua nani atinge makundi, huku wenyeji wakihitajika kupata japo sare tu au ushindi mkubwa kukata tiketi hiyo.
Baada ya ratiba hiyo ya mazoezi ya Yanga, Gamondi aliliambia Mwanaspoti kuwa baada ya maandalizi hayo sasa ana imani kwamba wachezaji watakuwa ba dakika 90 bora zitakazoenda kuwafurahisha mashabiki.
Gamondi alisema viwango vilivyonyeshwa na wachezaji, huku wengine wakiomba radhi kwa kile kilichotokea Ethiopia katika mchezo wa kwanza Yanga ambao Yanga ilishinda 1-0 wakiahidi mechi ya nyumbani itakuwa boza zaidi.
“Sote hatukufurahia kile kilichotokea Ethiopia, ilitakiwa kushinda kwa kiwango kikubwa lakini mambo haya yanatokea kwenye soka, ninachofurahia kila mchezaji anajutia lile,” alisema Gamondi.
“Tumefanya mazoezi ya kutosha ya kufunga mabao, naweza kusema kila kilichofanywa na washambuliaji na wachezaji wa nafasi zingine kimenivutia sana naamini tutakwenda kuwa na dakika 90 nzuri nyumbani mbele ya mashabiki wetu.