Nilipoona mazungumzo yake hayaingii kichwani mwangu nikajidai kumuuliza.
“Bidhaa tu za Wahindi.”
“Mkifika Dar, kesho mnaondoka tena?’
“Kupatikana kwa mzigo, kama mzigo upo tunaondoka tena.”
“Sasa nyinyi mnalala muda gani? Au ndio mnakula mirungi usiku na mchana?”
“Tunalala. Kama tunafika hii alfajiri tunasubiri kuche, tunashusha mzigo wa watu halafu narudisha gari, tunakwenda kulala. Kama kuna safari nyingine tunaweza kuondoka usiku au asubuhi ya kesho kutwa.”
“Wewe ndio unaona tuna kazi lakini sisi wenyewe tumeshazoea.”
Baada ya kumkatisha yale mazungumzo yake ya kunidadisi maisha yangu nikawa nimemchanganya kidogo, hakunidadisi tena mpaka tuliposimamishwa na polisi wa usalama barabarani.
Walikuwa polisi wanne waliokuwa wameegesha gari lao pembeni na kusimama kando ya barabara. Nikaogopa.
“Wakikuuliza wewe nani, waambie ni mke wangu. Usiseme ni abiria. Haturuhusiwi kuchukua abiria.” Dereva Musa akaniambia.
“Ficha hiyo mirungi.”
Nikaificha chini ya siti. Ile iliyokuwa midomoni nikaitema haraka. Dereva naye alifanya hivyo hivyo.
Polisi mmoja akaja kwenye dirisha la upande wa dereva.
“Poa.” Dereva akamjibu na kumuuliza.
Kabla ya dereva kumjibu kitu, polisi akauliza.
Macho yake yalikuwa yakiangaza angaza ndani ya gari kama yaliyokuwa yakitafuta kitu.
“Tunatoka Kigoma.” Dereva akamjibu.
“Umemuona wapi abiria?”Dereva akamuuliza.
“Si huyo msichana umekaa naye”
“Hapana. Huyu si abiria, ni mke wangu. Natoka naye Kigoma. Alikuwa amekwenda kwao. Nilivyokwenda Kigoma juzi nimeamua nirudi naye.”
“Sasa si ameshakuwa abiria?”
“Hapana. Ni sisi wenyewe tu. Abiria ni yule anayelipa nauli. Huyu anasaidia kunizuia na michepuko ya njiani.”
Polisi huyo akacheka na kumuita mwenzake.
“Angalia huyu dereva eti anasema amemchukua mke wake amzuie na michepuko,” akamwambia.
Polisi aliyeitwa naye akatuchungulia.
“Lakini ni mke wake kweli?”
“Jamani ni mume wangu, tumeamua kuja pamoja,” nikasema.
“Tumetoka Kigoma,” nikajibu mimi.
“Kuna bidhaa za kawaida tu,” alijibu dereva.
“Hebu lete risiti zake tuone kama zimelipiwa kodi.”
Dereva akachukua mkoba wake aliokuwa ameuweka pembeni mwa mlango wa gari akatoa stakabadhi mbalimbali na kumpa polisi huyo.
“Hebu shuka utueleze.” Polisi aliyepokea stakabadhi hizo alimwambia.
Dereva akashuka. Walikwenda nyuma ya gari wakazungumza. Baada ya robo saa hivi dereva akarudi peke yake akiwa na stakabadhi zake mkononi.
Alizitia kwenye mkoba wake kisha akaliwasha gari, tukaondoka.
“Umewapa ngapi?’ Taniboi wake akamuuliza.
“Nimewapa elfu tano tu.”
“Umewapa za nini?” Nikauliza mimi.
“Kawaida tu. Maswali yote yale walikuwa wanataka hela tu.”
“Wameangalia huo mzigo?” Nikamuuliza.
“Hawakuangalia chochote.”
Nikacheka. Dereva akatoa mirungi yake na kuanza kutafuna.
Na mimi nikatoa yangu tukaendelea kusaga.
Baada ya muda kidogo nilianza kukihisi kile kitu wanachokiita ‘handas’. Nilijiona nimechangamka na kuwa na maneno mengi. Sasa msemaji nikawa ni mimi. Nilikuwa nikieleza kila kitu mpaka nilivyokuwa mtoro shuleni na kuishia darasa la saba.
Wakati tunaingia jijini Dar kulikuwa kumeshaanza kupambazuka. Saa ya ndani ya gari ilionyesha kuwa ilikuwa saa kumi na moja na dakika arobaini.
“Sasa mtanipeleka nyumbani?” Nikamuuliza dereva.
“Nitakupa nauli upande daladala. Sisi tutaishia hapa hapa Kimara.” Dereva akaniambia.
Alilisimamisha lori pembeni mwa barabara akafungua mlango na kushuka kisha akaniita. Nikashuka kwenye gari. Kichwa kilikuwa kizito kwa mirungi. Uchovu wote wa usingizi ulikuwa umenitoka.
Niliposhuka, dereva aliniita nyuma ya gari akanipa shilingi elfu arobani.
“Zinakutosha?” Akaniuliza.
“Kwa nauli tu zinatosha kabisa. Nashukuru,” nikamwambia.
“Naomba namba yako,” akaniambia.
Nikampa. Na yeye akanipa yake.
“Umesema unaishi Ilala?”
“Basi nitakupigia mchana tuzungumze.”
“Nenda kapande daladala uende au wataka nikuongeze mirungi?’
“Imetosha. Siwezi kula mingi, kumeshakucha.”
Dereva akacheka kisha tukaagana. Nikaenda kupanda daladala.
Nilipofika nyumbani, walikuwa bado wamelala. Nikamuamsha shangazi niliyekuwa ninaishi naye. Nikamuamkia na kumwambia kwamba nimerudi.
“Umekuja kwa basi gani asubuhi hii?” Akaniuliza.
“Nilipata lifti ya lori, nimekuja bure na pesa ya kupanda daladala pia nimepewa.”
“Una bahati mwanangu.”
“Basi nililopanda kwanza liliharibika njiani, ningefika tangu jana jioni.”
Baada ya kuzungumza kidogo na shangazi niliingia chumbani kwangu. Niliweka mkoba wangu nikavua mavazi niliyokuwa nimevaa na kujifunga khanga na taulo. Nikaenda kuoga.
Niliporudi nilitaka nilale lakini usingizi ulikuwa umeniruka. Nikawasha TV na kukaa kwenye kochi. Niliangalia matangazo ya magazeti asubuhi ile huku nikimuwaza yule dereva Musa aliyenipa mirungi iliyorusha usingizi wangu.
Nikajiambia kama si yeye huenda muda ule bado ningekuwa njiani, sijafika Dar.
Licha ya kuoga maji baridi nilikuwa nikiona joto kwani mwili ulinichemka sana. Ilipofika saa tatu asubuhi wakati nakunywa chai, dereva Musa alinipigia simu, nikaipokea.
“Hello Musa, vipi huko?” Nikamuuliza.
“Huku poa tu, uko wapi?”
“Na wewe unajifanya kama hujui, nataka tukutane.”
“Popote tu tutakapopanga.”
Musa alisita kabla ya kunijibu.
“Mazungumzo tu.” Sauti yake ilikuwa imenywea.
“Yapi sasa, yasiyoongeleka kwenye simu?” Nikamuuliza.
“Mbona una maswali mengi?” Ilikuwa sauti ya kubembeleza.
“Lazima nikuulize niweze kukuelewa.”
Alipoona nimembana akabadili mada.
“Unajua kesho asubuhi naondoka.”
“Unakwenda wapi?” Nikamuuliza.
“Naenda Burundi. Kuna mzigo napeleka.”
“Ahaa kesho unakwenda Burundi?”
“Ndiyo, nitaondoka saa kumi na mbili asubuhi.”
“Yoyote tu utakayopenda.”
“Nitakuletea japokuwa hukutaka kukutana na mimi leo.”
“Sijakataa isipokuwa sitakuwa na nafasi kwa leo.”
Pakapita ukimya mfupi kabla ya Musa kuniambia.
“Sawa, basi tutakutana hapo nitakaporudi.”
“Unatarajia kurudi lini?”
“Sijui lakini safari zeu zinachukua wiki tatu mpaka nne.”
“Tunachelewa zaidi kwenye mipaka. Kunakuwa na foleni ndefu za magari.”
“Nakuombea Mungu uende salama na urejee, tukutane.”
“Nashukuru. Nitakupigia kabla sijaondoka.”
Nilipomaliza kunywa chai ndipo nilipoanza kuhisi usingizi. Nikaingia chumbani. Nilijitupa kitandani nikalala hapo hapo.
Nilikuja kuamshwa saa saba mchana. Aliniamsha shangazi akaniambia.
“Amka uje ule, chakula tayari.”
Usingizi ulikuwa umenikolea. Sikutaka kuamka.
“Kula tu shangazi, mimi naendelea kulala.”
“Kwani umepika nini?”
“Nimepika pure (kande).”
Nikaendelea kulala hadi saa nane na nusu nilipoamka na kwenda kuoga.
Niliporudi chumbani mwangu, shoga yangu Amina akanipigia simu. Alikuwa msichana wa Kirangi mwenyeji wa Kondoa Irangi. Tulifahamiana nilipokuwa shule. Yeye alianzia darasa la nne akitokea Kondoa.
“Niambie Amina…” nikamwambia mara tu nilipopokea simu yake.
“Mimi mzima shoga. Mbona kimya sana?”
“Si ndio nimekukumbuka shoga yangu.”
“Halafu unajua ndio nimerudi kutoka Kigoma.”
“Kumbe ulikwenda Kigoma?”
“Nilikuwa Kigoma tangu juzi. Mwenzangu basi liliharibika njiani. Nimekuja na lori. Tumefika alfajiri. Nimechoka, sina hamu.”
“Tukutane basi tupige stori.”
“Nitakuja nyumbani. Hivi sasa naenda kula chakula. Nikitoka hapo nakuja.”
“Unakwenda kula wapi?”
“Hapo Afrique Restaurant.”
Nikavaa kisha nikamuaga shangazi na kutoka. Afrique Restaurant ilikuwa mtaa wa tatu kutoka mtaa niliokuwa nikiishi, hivyo kwamba niliweza kwenda kwa miguu kwani hapakuwa mbali sana.