JUMAPILI ilipowadia Amina akanipigia simu kunikumbusha juu ya ile ahadi yetu. Nikamwambia kuwa ninaikumbuka.
“Tutakapokuwa wote nitakupigia,” nikamwambia nilimaanisha nitakapokuwa na mchumba wangu Musa nitampigia ili aje.
Saa moja usiku Musa akanipigia simu kunijulisha kuwa ameshafika hapo hotelini. Hapakuwa mbali sana na nyumbani kwetu. Na mimi nikampigia Amina.
Nikamwambia nikutane naye hapo hotelini. Baada ya kumueleza hivyo nikaanza mwendo wa miguu kuelekea huko hotelini. Nikiwa njiani nilimpigia tena Musa kumjulisha kuwa nitakuwa na rafiki yangu.
“Humjui, ndio nataka nikutambulishe naye.”
“Uliwahi kunitajia jina lake lakini sijawahi kukutana naye.”
“Ndio nataka leo umuone mfahamiane.”
“Sawa. Ninawasubiri.”
Wakati nafika hotelini nikakutana na Amina kwenye mlango.
“Eh! Shoga umekuja na bodaboda nini?” Nikamuuliza kwa mshangao.
“Kwanini?” Akaniuliza.
“Jinsi ulivyowahi ni kama uliyekuja na usafiri.”
“Hapana nimekuja kwa miguu tu.” Amina aliniambia kisha akacheka.
“Au ni hamu ya kumuona shemeji yako?” Nikamuuliza kwa mzaha.
Amina akaendelea kucheka.
Aliponiambia hivyo tukacheka sote.
“Wala usiumie shoga, shemeji yako utamuona leo tena yeye ameshafika,” nikamwambia.
“Twenzetu nikamuone.’
Tukaingia ndani ya hoteli. Tulimkuta Musa akiwa amekaa kwenye meza ya peke yake akitusubiri. Nilimuona akitafuna tafuna, nikajua alikuwa anatafuna mirungi kisirisiri. Mezani kwake kulikuwa na chupa ya CocaCola na chupa ya maji safi.
Alipotuona alijifuta midomo yake kwa kitambaa kisha akakaa vizuri.
“Vipi unasaga?” Nikamuuliza.
“Si nimekuona unatafuna halafu umeweka chupa ya maji na Cocacola.”
“Nilikuwa namalizia miti yangu ya mchana. Sijui hii tasnima yangu nitaiweka wapi?”
Nikavuta kiti na kuketi. Amina naye akaketi.
“Hili tonge la mirungi lililoko mdomoni.” Musa akanijubu.
“Ndio linaitwa tasnima?”
“Na ninyi mna maneno ya ajabu ajabu, eti tasnima!” Nikamtazama Amina kisha nikacheka.
Nilijua Amina pia alitaka kucheka lakini alijikaza kwa kumuona aibu shemeji yake.
“Amina shemeji yako huyo, umuone umjue umfahamu,” nikamwambia Amina.
“Shemeji habari za siku?” Amina akamsalimia Musa huku akimpa mkono.
“Musa huyo ni rafiki yangu kipenzi anaitwa Amina,” nikamwambia Musa.
“Oh nimefurahi kumfahamu, karibu shemeji.”
“Sasa hilo tasnima lako si uende ukalitupe msalani,” nikamwambia Musa.
“Hili halitupwi, linahifadhiwa tu kisha baadaye ninalirudisha midomoni.”
“Mh! Nasikia kinyaa. Watu wa mirungi mna mambo yenu,” nikasema kasha nikamgeukia Amina: “Umemsikia huyu anachosema?”
“Lakini si uliniambia hata wewe unakula.” Amina akanisusuwaza.
“Nakula lakini sio kivile.”
“Hebu nisaidie shemeji yangu, asinisakame mimi kumbe na yeye pia yumo.” Musa akasema.
“Hebu kalitupe bwana…” Nikamwambia Musa baada ya kucheka.
“Naona mnapendana sana.” Amina akaniambia.
Mhudumu akatufuata na kukatiza mazungumzo yetu. Alitupa menyu. Nikaangalia orodha ya vyakula kisha nikamwambia.
“Ngoja bwana mkubwa aje.”
Musa aliporudi nikamuuliza.
“Kila mtu atakula anachopenda.”
“Mimi nataka chipsi kuku,” nikasema kisha nikamtazama Amina.
“Utakula nini Amina?” Nikamuuliza
“Nitakula hizo hizo chipsi kuku.”
Nikampungia mkono muhudumu kumuita. Mhudumu alipofika sote tuliagiza chipsi kuku na juisi.
Wakati tunasubiri chakula tulichoagiza tukaanza kupiga stori.
“Shemeji, shoga yangu ameniambia mnakaribia kufunga ndoa. Je, ni kweli?” Amina akamuuliza Musa.
Lilikuwa swali ambalo kwa mtu mwingine lisingependeza lakini kutokana na ukaribu wetu mimi na Amina sikujali.
“Kama amekuambia hivyo ni kweli.” Musa akamjibu.
“Sawa. Sasa kuna mambo yanayohitajika mojawapo ni kumfanyia shopping kwa ajili ya sanduku la harusi…”
“Amina umesema kweli,” nikamuunga mkono Amina kisha nikamwambia Musa.
“Shopping tutafanya.” Musa akasema.
“Lini? Si unaona siku zimekaribia.”
“Wewe ungependa lini?”
“Ningependa iwe kesho kwa sababu leo ni usiku. Ningetamani hata iwe leo.”
Musa akafikiri kidogo kisha akasema.
“Kwa hiyo kesho utakwenda kunifanyia shopping.”
“Nataka iwe shopping kamili, nipate gauni la harusi, nguo zangu za kuvaa, pochi viatu na dhahabu.”
Vyakula vyetu vikaletwa. Tukanawishwa mikono kisha tukaanza kula.
“Sasa tutakutana wapi?” Nikamuuliza Musa.
“Nitakapokuwa tayari nitakupigia simu.”
“Hapana, niambie kabisa ili niweze kujiandaa, tena nitakuwa na shoga yangu Amina.’
“Ndio tutakuwa pamoja.” Amina akanikubalia.
“Nimekwambia nitakapokuwa tayari nitakupigia simu, sasa hapo nikikupigia ndio utajiandaa.”
“Kwa hiyo nikae tu nisubiri simu yako ambayo sijui utanipigia saa ngapi?”
“Itategemea nitakapoondoka kazini.”
“Niambie muda bwana.”
“Basi tuweke saa sita. Yaani nitakupigia simu saa sita kukujulisha kuwa ninakuja.”
“Amina kesho saa sita uje nyumbani. “
“Tutanunua sanduku huko huko, si unajua harusi za Kiswahili nguo ni mpaka zisasambuliwe.”
“Tutanunua kila kitu.”
“Msisahau na doti za khanga jamani.”
“Khanga lazima, tena nataka khanga zile zenye maneno ya kukera.”
“Kumbe Mishi nawe umo!” Akaniambia na kunipiga kwenye bega langu.
Tuliendelea kula na kuzungumza hadi tukamaliza mlo wetu. Sote tulikuwa tumeshiba vizuri.
Tukatoka hotelini na kutembea kwa miguu kumsindikiza Musa barabarani akapande daladala.
Tulipofika kwenye kituo tulisubiri daladala. Daladala ilipofika Musa akaondoka. Mimi na Amina tukarudi.
“Shoga umepata bonge la bwana!” Amina akaniambia wakati tunarudi.
Maneno yake yalinifurahisha, nikamuuliza.
“Kwanini unasema hivyo?’
“Ni muelewa. Kila unachomuambia lake yeye ni hewala tu. Hampingani?”
“Si kuna kitu anataka. Akishakipata anaweza kubadilika.”
“Kwani hajakipata tu?”
“Hicho kitu unachosema wewe.”
“Umekijua ni kitu gani?
“Kwani wewe ulikusudia kitu gani?”
“Ndoa. Si anataka kuniweka ndani ili aweze kunimiliki vizuri. Kwa sasa atakubali kila kitu nitakachomwambia.”
“Unadhani atakuja kubadilika? Hawezi kubadilika.”
“Usiseme hivyo Amina, yamewakuta wengi.”
“Watu hawajui. Kinachommbadili mume ni tabia zako mwenyewe.”
“Wakati mwingine unajiona wewe ndiye mke peke yake, unaanza kumdengulia. Kila kitu unamchukulia poa tu. Yale mapenzi ya mwanzo humuonyeshi tena. Ndio hapo mwenzako anapoanza kubadilika.”
“Keshokutwa mwenzako napelekwa kwa kungwi. Nitakwenda fundwa huko huko. Mbinu za kumdhibiti atakaponioa nitazipata huko huko.”
Nilipomwambia hivyo Amina, tukacheka.
“Lakini Amina tuache utani, Musa nimempenda sana. Ni mpole na ananisikiliza sana. Mwache anioe,” nikamwambia Amina baada ya kicheko.
“Sio unampenda, mnapendana. Nimegundua hata yeye anakupenda, vinginevyo asingekuwa anakusikiliza.”
“Basi ndio hivyo shoga. Nilitaka umpitishe uniambie kuwa anafaa au vipi.”
“Nimeshampitisha anafaa.”
“Basi poa, kesho utatupeleka madukani.”
Siku ya pili yake Musa akanipigia simu saa nne asubuhi akaniambia kuwa anakuja Ilala.
“Unisubiri pale pale kwenye kituo cha daladala, nitakuja na teksi.”
“Hivi sasa ni saa nne, njoo saa tano,” nikamwambia.
Baada ya kuzungumza na Musa nikampigia simu Amina.
“Amina jitayarishe, jamaa amenipigia simu,” nikamwambia.
“Amekwambia anakuja?”
“Alitaka aje muda huu lakini nimemwambia aje saa tano, hivyo jitayarishe uje hapa kabla ya saa tano.”
“Sawa shoga, ninajitayarisha.”
Nikakata simu na kwenda kuoga. Nilipomaliza nilichagua nguo nikavaa. Nilitumia kama dakika tano kujipodoa mbele ya kioo kisha nikakaa kumsubiri Amina.
Ilipofika saa tano kasorobo Amina akanipigia simu.
“Nikukute wapi?” Akaniuliza.
“Ungekuja hapa nyumbani tuondoke pamoja,” nikamwambia.
“Basi nisubiri hapo nje, mimi ndio nakuja.”
Nikamuaga shangazi na kutoka nje. Sikusubiri kwa muda mrefu Amina akatokea.