Mamia ya vifaa vya mawasiliano vinavyotumika na kundi linaloungwa mkono na Iran nchini Lebanon, Hezbollah, vimeripuka na kusababisha vifo vya watu tisa na wengine 2,800 kujeruhiwa. Waziri wa Afya wa Lebanon, Firass Abiad, amesema kati ya watu hao waliojeruhiwa watu mia mbili wako katika hali mahututi.
“Kama tulivyosema jana, watu waliojeruhiwa wanakaribia 3000. Wengi wamejerhiwa usoni, machoni na mikononi. Visa hivi vinatathiminiwa kujua iwapo majeruhi watahitaji kuhamishiwa kwengine na iwapo tutawapeleka wagonjwa wengine katika hospitali maalum nchini Iraq ama mataifa mengine ili wapate matibabu wanayoyahitaji.”
Hezbollah imedai Israel ndiyo iliyofanya shambulizi hilo na kuapa kuiadhibu vikali, ingawa maafisa wa Israel bado hawajatoa tamko lolote juu ya tukio hilo.
Shambulizi la Lebanon limetokea saa chache baada ya Israel kutangaza kutanua vita vyake na Hamas kwa kulijumuisha kundi la Hezbollah katika maeneo ya mpaka wake na taifa hilo jirani.
Iran, ambayo moja kwa moja pia imeilaumu Israel kwa mauaji ya wengi, imepeleka timu ya madaktari nchini humo kusaidia kuwatibu waliojeruhiwa.