Kyerwa. Ni tukio la kushangaza. Ndivyo unavyoweza kuelezea kile kilichotokea katika familia ya Venant Zabron (52), Mkazi wa Kahinga, Kata Bugomola, wilayani Kyerwa, Mkoa wa Kagera baada ya kaburi la mjukuu wake kufukuliwa na watu wasiojulikana.
Mbali na kufukuliwa kwa kaburi hilo, watu hao walichukua jeneza lilokuwa na mwili wa mtoto huyo, Faston Innocent (1) na kulitekeleza mlangoni mwa nyumba ya Zabron. Tukio hilo lililotokea jana Jumanne, Septemba 17, 2024 limeibua taharuki kijijini hapo.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatano Septemba 18, 2024, Zabron amesema jana saa 12 asubuhi akiwa ndani ya nyumba yake, alisikia kelele za majirani waliokuwa wakipita kwake, lakini hawakubaini chanzo.
Amesema walipotoka nje waliona jeneza hilo liliokuwa na mwili wa marehemu mjukuu wake waliyemzika siku chache zilizopita likiwa nimefunuliwa mlangoni, huku mashuka na msalaba vikiwa eneo hilo.
“Mwili ulikuwa ndani ya jeneza likiwa limefunuliwa, watu walinishangaa, hata sisi familia hatukuelewa mashuka na msalaba vilikuwepo maeneo hayo,” amesema Zabron.
Amesema waliujulisha uongozi wa kijiji, kuangalia kaburi la mjukuu wake lilikuwa limefukuliwa na hawajajua aliyehusika, hivyo kuuachia uongozi ufanye uchunguzi.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Magoma, Venance Nicholas amesema alipata taarifa saa 12:30 asubuhi kutoka kwa familia hiyo kuwa wamekuta mwili wa mtoto aliyezikwa Septemba 12, 2024 jeneza lake limekutwa mlangoni.
Amesema baada ya taarifa hiyo, aliwasiliana na uongozi wa wilaya, jeshi la polisi na kata, mwili uliamuliwa ukazikwe upya, huku jeshi la polisi likiendelea na ufuatiliaji wa tuykio hilo. Mwili huo ulizikwa tena jana Jumanne katika kaburi la awali.
“Sisi kama viongozi imetushtua na tukio hilo maana haijawahi kutokea maeneo haya, tunaomba Serikali itusaidie tubaini nani kahusika hata kama ni nguvu za kishirikina tujue,” amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa, Zaituni Msofe amesema amepokea taarifa za awali kuhusu tukio hilo na anafuatilia na baadaye atalizungumzia baada ya kupokea taarifa kamili.
“Ni tukio baya kwenye jamii na kuogopesha, ila nalifuatilia baadaye nitalizungumzia baada ya kupokea taarifa kamili,” amesema mkuu huyo wa wilaya
Taarifa ambazo Mwananchi limepata kuna baadhi ya watu wanashikiliwa kuhusu tukio hilo.
Endelea kufuatilia Mwananchi