Kamisheni ya Ardhi yalalamikiwa ucheleweshaji wa hatimiliki

Unguja. Baadhi ya wananchi wameiomba Kamisheni ya Ardhi kubadilika kutokana na mzunguko mrefu uliopo kwa watu wanaotafuta hatimiliki za ardhi za kilimo.

Akizungumza leo Septemba 18, 2024 katika uzinduzi wa utoaji hati hizo, Aziza Ibrahim Ahmed, mkazi wa Kwa Goa amesema ni mwaka wa sita sasa amekuwa akihangaika kutafuta hati hiyo.

Amesema alikata tamaa ya kuipata hadi na hata leo ameipata ni jambo ambalo hakulitarajia.

“Nina mwaka wa sita sasa natafuta hati hii, jana (Septemba 17) nimepigiwa simu ili nije nichukue. Naiomba Kamisheni wabadilike ili kutupunguzia mzigo wananchi,” amesema Aziza.

Ramadhan Hassan Suluhu, amesema japokuwa mchakato ni mrefu, amefarijika kuona sasa amepata hatimiliki.

Amesema kwa kadri ya mchakato ulivyokuwa ukichelewa walielezwa sababu jambo lililompatia faraja na kumfanya kuwa mvumilivu.

Ramadhan ametoa wito kwa Kamisheni ya Ardhi inapokwenda kupima viwanja bikoni zinazoonyesha mipaka ziweke vizuri kuepusha mivutano.

Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi Zanzibar, Rahma Kassim Ali amesema ucheleweshwaji wa utoaji wa hati hizo ulitokana na ubadilishaji wa mkataba wa eneo la ekari tatu ambao haukuwa na ramani ya mipaka.

“Naiagiza Kamisheni kutengeneza utaratibu rafiki wa kutoa hati kwa wananchi bila ya kucheleweshewa,” ameagiza. Jumla ya hati 32 zimetolewa katika uzinduzi huo.

Hata hivyo, amewataka wananchi kuacha tabia ya kuvamia maeneo na kukata vipande, akieleza ardhi ya Serikali si ya mtu binafsi hivyo haipaswi kuuzwa.

Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Ardhi, Mussa Kombo Bakari amesema kwa miaka mitatu hawakutoa nyaraka yoyote kwa wanaotumia mashamba ya Serikali kwa sababu ya masharti yaliyomo kwenye sheria ya ardhi.

Kutokana na umuhimu wa ardhi, amesema wananchi wanapaswa kusimamia vizuri mashamba hayo ili kuepuka migogoro.

Related Posts