Kiini ndoa kuvunjika mapema hiki hapa 

Dar es Salaam. Wadau wa masuala ya saikolojia, wanasheria, wanazuoni na wanajamii wamebainisha sababu kadhaa zinazochangia ndoa kuvunjika mapema baada ya kufungwa, hususan mijini.

Wameeleza hayo walipochangia mjadala wa Mwananchi X Space leo Jumatano Septemba 18, 2024 ulioongozwa na mada isemayo: ‘Nini kinachochea ndoa zinazofungwa mijini kuvunjika mapema?’

Mada katika mjadala huo ulioandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) inatokana na ripoti ya hivi karibuni ya Chama cha Wanasheria wa Familia inayoeleza ndoa zinazofungwa mijini kwa asilimia 40 zinavunjika chini ya miaka mitano ya kwanza. 

Mwanachama wa Chama cha Wanasaikolojia Tanzania (Tapa), Jesusa Charles amesema miongoni mwa yanayochangia ndoa kuvunjika mapema ni utandawazi.

“Utandawazi umesababisha dunia kuwa kijiji na kuna mambo mengi yanayoendelea na yanatuzidi, kadri yanavyotuzidi ndoa zinakuwa haziko salama. Watu wanashidana na kuondoka katika uhalisia wao.

“Unaweza kujikuta upo kwenye mahusiano mtu anaangalia mtu mwingine anafanya nini, mtindo huo unapoendelea ina maana mtu unaanza kujikataa na kumuona mwenza wako hafai sababu tu umeangalia mambo fulani katika mtandao,” amesema.

Mbali ya hilo, amesema mambo wanayopitia watu yanaacha hisia, lakini vidonda hivyo huwa havionekani, akitaja mfano wa unyanyasaji.

“Wengi wanahisi wakiingia kwenye ndoa vitapona na wengi wanafanya hivyo wakiwa na lengo la kujiweka sehemu salama, lakini unakuta kadri muda unavyoenda lengo linashindwa kutimizwa mwisho wa siku mtu anakata tamaa,” amesema.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Mjege Kinyota amesema matatizo ya ndoa kama vile vipigo na usaliti si kwamba hayakuwepo zamani, bali kulikuwa na uvumilivu na kuficha mambo yanayowakabili wanandoa.

Amesema suala la kuachika lilikuwa aibu, tofauti na ilivyo sasa.

Dk Kinyota amesema matarajio ya sasa kama vile mwenza wako akupatie kila kitu ni miongoni mwa sababu za ugomvi katika ndoa.

“Una mume au mke unataka kila kitu akupatie, na yeye unakuta yuko ‘bize’ anatafuta maisha kwa hiyo lazima ugomvi uanze,” amesema.

Amesema msingi wa ndoa unajengwa na mapenzi ya dhati kama ilivyokuwa zamani, lakini siku hizi watu wanaoa na kuolewa kwa sababu ya kipato na mali na si msingi wa mapenzi ya kweli.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (Tawla), Tike Mwambipile amesema sheria ya ndoa inaelekeza mwanamume akiwa ameoa lazima awajibike kumtunza mke.

Hata hivyo, inapotokea sababu maalumu kama kuumwa au hana kazi, basi mkewe ana wajibu wa kisheria kumtunza mume wake.

Amesema kwa sasa wanawake wana vipato kutokana na masuala ya usawa wa kijinsia na wakati mwingine mke ana kipato kumzidi mume wake, lakini changamoto hutokea kutokana na kutokuwa na uelewa kati yao.

“Suala lililopo ni kutafakari kwa namna gani tunaweza kusaidiana katika hili. Lakini kikubwa mwanaume ili apate heshima yake vizuri, basi anapaswa atunze familia hata kama mkewe ana kipato,” amesema.

Tamaduni zisizotoa usawa kwa wanawake na wanaume imeelezwa huchangia ndoa kuvunjika.

Joseph Wasira, akichangia mjadala huo amesema katika baadhi ya maeneo ya Kanda ya Ziwa ndoa kuvunjika huchangiwa na tamaduni kandamizi zisizotoa usawa kwa mwanamke na mwanaume.

“Wanawake wa maeneo hayo wameanza kupata mwanga kwa kutambua walikuwa wanapata mateso, wanaamua kuacha ndoa kwenda kutafuta maisha mapya kwa sababu tu ya kukosekana uwiano wa usawa,” amesema.

Wasira amesema ukilinganisha ukubwa wa tatizo hilo, vijijini ni kubwa zaidi kuliko mijini na taasisi za kiraia zimekuwa zikienda maeneo hayo kutoa elimu.

Amesema usasa pia unaathiri taasisi ya ndoa, akisema maadili yameporomoka, hivyo watu hawaoni umuhimu wa kuwa ndani ya ndoa kama ilivyokuwa zamani.

Wasira amesema pia ndoa za mijini huvunjika kutokana na familia kutokuwaanda vijana katika malezi.

Mbali ya hayo, imeelezwa umaskini wa fikra na uwepo wa matatizo ya afya ya akili kutokana na mfumo wa maisha uliopo mijini, kulinganisha na vijijini ni miongoni mwa sababu za kuvunjika mapema kwa ndoa za mijini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Akili Platform Tanzania, Roghat Robert amesema mengine yanayochangia kuvunjika ndoa za mijini ni umbea, kusambaza uvumi, taarifa zisizo za kweli, makundi na mtazamo uliopo kwa baadhi ya watu kwamba mtu akishapata pesa anabadilika.

“Tulifanya dodoso tukagundua ukichukua wadada 10 ukiwauliza wanasema wanatamani kuzaa, lakini hawataki kuwa chini ya mwanaume, hivyo unagundua wengi wanajikuta wakikata tamaa kutokana na mfumo wa maisha na matukio yanayotokea,” amesema.

Ni nini kifanyike, amesema lazima watu waandaliwe mapema kabla ya kuingia kwenye ndoa, ili watakapoingia wajue majukumu yao na kuvumilia upungufu wa kila mmoja.

Kenny Mmari akichangia mjadala huo amesema matarajio makubwa yasiyokuwa na uhalisia ni chanzo cha ndoa kuvunjika mapema.

Amesema, “watu wanachukulia wanavyoviona kwenye vyombo vya habari na katika filamu, wanaingia na matarajio hayo, sasa wakiingia wakikutana na mambo tofauti wanaachana.

“Mijini ni mfano mzuri wa utandawazi kuliko vijijini, yanayotokea kwenye miji ya Tanzania na Afrika na sehemu zingine duniani ni kiashiria ya kile kinachotokea maeneo yote.”

Mmari ametaja sababu nyingine ni mabadiliko ya wajibu wa kijinsia akisema, “zamani tamadani zetu zilikuwa zinamfanya mwanamke kuwa na watoto na kuwa mtu wa nyumbani, lakini leo wana uhuru zaidi si jambo baya lakini inasababisha migogoro ya kuvunjika ndoa.”

Amesema kadri ustaarabu wa binadamu unavyopiga hatua unasababisha kila mtu kutafuta utimilifu wa haki yake na kupata furaha itakayomfanya afurahie maisha.

“Mahitaji hayo yanapoongezeka yanasababisha mgongano wa masilahi na ilivyo mjini watu wengi wamebadilika na kuzoea utamaduni wa kidunia zaidi kuliko wa vijijini,” amesema.

Ndoa zinazojengwa katika misingi ya mali badala ya upendo pia zimetajwa kuvunjika mapema.

“Ustawi wa Taifa unategemea ustawi wa mahusiano ya ndoa na familia kwa ujumla, kukosekana kwa msingi mzuri wengi wanapuuza. Miaka ya nyuma vijijini msingi wa ndoa ilikuwa watu kukutana na kupendana na kuamua kuoana.

“Mapenzi yalikuwa msingi wenyewe, mambo yanavyobadilika watu wanakengeuka, ule utaratibu wa zamani mfano mtu anaweza kuwa na mtu wake anampenda lakini akaona bado anapambana na maisha anamfuata aliyefanikiwa kimaisha,” amesema Hemed Tawa akichangia mjadala huo.

Amesema vijana wengi wanaangalia mtu aliyefanikiwa au kuwa na kazi wakiamini hata kuwa mzigo katika maisha yake bila kujali kama anampenda.

“Matokeo yake tunatoka kwenye msingi halisia ambao ungeisimamisha ndoa na kustawi. Kwa hiyo mnakuwa matapeli wawili mmekutana kila mmoja kaja na sababu yake lakini wanashindwa kuambiana,” amesema.

Awali, akichokoza mada, Mhariri wa Gazeti la Mwananchi, Kalunde Jamal amesema kukosa elimu ya ndao kwa walio wengi nchini ni sababu ya nyingi zinazofungwa kuvunjika ndani ya muda mfupi.

“Tatizo liko maeneo yote mijini na vijijini, inaweza kuwa mijini hali imezidi. Nilichokigundua hakuna elimu ya ndoa, walio wengi wanaingia kama fasheni, hawajui wanaenda kukutana na nini kwa wanaume na wanawake,” amesema.

Amesema tatizo lingine ni usasa, akieleza kutokana na mabadiliko ya teknolojia mtu anakuwa na uwanja mpana wa kujifunza mambo kwa kusikiliza wanachozungumza wengine kupitia mitandao ya kijamii.

Ripoti ya matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 inaonyesha takwimu za watu kupeana talaka zimeongezeka zaidi ya mara nne ikilinganisha na sensa ya mwaka 2012.

Mkuu wa Dawati la Takwimu katika Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Halili Letea amesema, “kiwango cha talaka kwa mwaka 2022 ilikuwa asilimia 3.7 ikilinganishwa na asilimia 0.9 mwaka 2012. Hivyo kuna ongezeko la wanaoachana. Pia wapo waliotengana bila talaka walikuwa asilimia 1.8 mwaka 2022 tofauti na asilimia 2.9 mwaka 2012.”

Related Posts