Kundi la itikadi kali ladai kuhusika na mashambulizi, Mali – DW – 18.09.2024

Mashambulizi hayo katika maeneo kadhaa mjini Bamako ni tukio la nadra la machafuko kufikia mji huo baada ya miaka kadhaa ya vita katika maeneo ya mbali na mji kati ya vikosi vya serikali na waasi wa itikadi kali.

Baada ya makabiliano hayo ya risasi kupungua, mji huo ulikabiliwa na hali ya wasiwasi huku makundi ya vijana yakishika doria mitaani.

Soma pia:Jeshi la Mali ladhbiti hali Bamako kufuatia shambulizi

Shirika la habari la Reuters liliripoti kuona mabaki ya mwili wa mtu mmoja ulioungua. Mashuhuda wanasema mwili huo ulikuwa wa muuzaji mmoja wa sigara aliyechomwa na vijana kwa sababu alikuwa amevaa mkanda wa risasi na kuwafanya vijana hao kumshuku kuwa mshambuliaji.

Video za matukio mbalimbali zasambazwa

Video zilisambazwa mtandaoni zikionyesha mwanamgambo mmoja aliyekuwa amejihami kwa silaha akiwasha moto injini moja ya ndege.

Ndege hiyo ilionekana kuwa na maandishi yaliosoma ”Jamhuri ya Mali”.

Soma pia:Raia wa Mali wakabiliana na maisha magumu tangu mapinduzi

Video nyingine ilionesha mtu aliyekuwa na bunduki akifyatua risasi dhidi ya ukumbi mmoja mtupu wa uwanja wa ndege .

Moshi wafuka kutoka uwanja wa ndege wa kimataifa mjini Bamako baada ya shambulizi la waasi mnamo Septemba 17, 2024
Moshi wafuka kutoka uwanja wa ndege wa kimataifa mjini Bamako baada ya shambulizi la waasiPicha: Social Media/via REUTERS

Video ya tatu ilionesha moshi kutoka kwenye jengo moja kubwa zinakoegeshwa ndege pamoja na kuhifadhiwa vifaa vingine.

Hata hivyo, Reuters haikuweza kuthibitisha uhalali wa video hizo.

Shughuli za uwanja wa ndege zazuiwa kwa muda 

Wizara ya uchukuzi nchini humo imesema kuwa shughuli za uwanja wa ndege zilizuiwa kwa muda ili kuepusha kutokea kwa hatari zozote, huku ikiwataka watu kudumisha utulivu. Kizuizi hicho kiliondolewa baadaye.

Jeshi lasema hali mjini Bamako imedhibitiwa

Katika taarifa, jeshi la nchi hiyo limesema kuwa mapema leo, kundi la magaidi lilijaribu kuingia katika shule hiyo ya mafunzo ya kijeshi ya Faladie na kwamba operesheni za kuwasaka zinaendelea kwa sasa.

Mkuu wa jeshi, Jenerali Oumar Diarra, alitembelea shule hiyo baada ya tukio hilo na kuwaambia waandishi habari kwamba shambulio hilo tata sasa limedhibitiwa na wavamizi kukabiliwa.

Soma pia:Kituo cha mafunzo ya kijeshi Mali chashambuliwa

Jioni ya jana, jeshi hilo lilisema kupitia taarifa kwamba shambulio hilo lilisababisha vifo kadhaa ikiwa ni pamoja na maafisa wa jeshi wa shule hiyo ya Faladie. Hata hivyo, halikutoa idadi kamili.

Afisa wa usalama ambaye hakutaka kutambulishwa, alisema shambulizi hilo lilianza mwendo wa saa tisa alasiri na anashuku kuwa washambuliaji walikuwa wametumia fursa iliyojitokeza ya sikukuu ya Waislamu siku ya Jumatatu ambayo iliwafanya waumini wengi kufika mjini humo.

 

 

Related Posts