Madina, Wanyeche, OLomi kuwania ubingwa Afrika

Madina Iddi wa Arusha ndiye kinara wa orodha ya wachezaji nyota waliochaguliwa kuunda timu ya taifa ya wanawake ya gofu itakayoshiriki mashindano ya ubingwa wa Afrika nchini Morocco mwisho wa mwaka.

Wengine waliochaguliwa ni Hawa Wanyeche wa Dar es Salaam na Neema Olomi  wa Arusha ambao kwa mujibu wa Rais wa Chama cha Gofu ya Wanawake (TLGU), Queen Siraki wamechaguliwa baada ya kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali makubwa ndani na nje ya nchi.

“Mashindano yaliyomalizika hivi karibuni jijini Arusha ya Tanzania Ladies  Open yalikuwa mtihani wa mwisho kwa wachezaji wanaowania kupata nafasi ya kuliwakilisha taifa nchini Morocco. Kwa hiyo wote waliochaguliwa wana sifa zinazostahili kuichezea timu yetu ya taifa katika mashindano haya,” alisema.

Queen alisema kila mwanagofu alitegemea wachezaji hao kuitwa timu ya taifa kwa sababu mafanikio yao ndani na nje ya nchi yaliwekwa wazi kupitia vyombo vya habari.

Katika mtihani wa mwisho ambao ni mashindano ya Tanzania Ladies Open, Madina alimaliza nafasi ya pili akiwa na wastani wa mikwaju +19 nyuma ya Mkenya Mercy Nyanchama aliyeongoza akiwa na wastani wa mikwaju +17. Hawa Wanyeche alimaliza nafasi ya tatu akiwa na wastani wa mikwaju +25 wakati Olomi alimaliza nafasi ya nne na mikwaju +32.

Mbali ya kufanya vizuri jijini Arusha, wachezaji hao pia walifanya vizuri katika mashindano ya nje yaliyofanyika Ghana, Zambia, Kenya na Uganda. Madina Iddi ndiye bora katika orodha  na ni tegemeo kubwa la ushindi baada ya kushinda mataji manne Ghana, Zambia na Uganda ambako alishinda mawili. Wanyeche alimaliza nafasi ya pili katika mashindano ya John Walker Uganda Open ambayo Olomi alimaliza katika nafasi ya tatu. Olomi pia alifanya vizuri katika mashindano ya viwanja vitano Pwani, Kenya ambako alikuwa wa pili.

Related Posts