Dar es Salaam. Mahakama Kuu, Masjala ndogo ya Dar es Salaam, imewapa siku tano wakulima 24 wa Kilombero, mkoani Morogoro ili wawasilishe majibu yao ya nyongeza katika kesi ya Kikatiba waliyoifungua dhidi ya Waziri wa Kilimo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Uamuzi huo umetolewa leo Jumatano, Septemba 18, 2024 na Msajili wa Mahakama hiyo, Hussein Mushi wakati shauri hilo lilipoitwa kwa ajili ya usikilizwaji.
Hatua hiyo, inatokana na wakulima hao kuomba muda wa nyongeza kuwasilisha majibu yao.
Mushi amewaongezea muda huo kutoka na wakulima hao kuwasilisha ombi mahakamani hapo, wakiomba waongezewe muda ili wapate nyaraka walizopewa na wajibu maombi ambazo wamedai zinahitaji muda kuzipitia na kisha kuwasilisha mahakamni hapo majibu ya nyongeza.
Kesi hiyo ya kikatiba imefunguliwa na George Mzigowandevu na wenzake 23, dhidi ya Waziri wa Kilimo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
George na wenzake hao kwa niaba ya wakulima wenzao 11,000, wa miwa kutoka Bonde la Kilombero, walifungua kesi hiyo Mahakamani hapo wakipinga kuondolewa kwa kinga ya uingizwaji wa sukari baada ya kufanyika mabadiliko ya sheria yaliyofanywa na Bunge la Jamhuri ya Muungano.
Mzigowandevu katika maombi yake anapinga, mabadiliko ya sheria Na 6 ya fedha 2024 ambapo kulifanyika mabadiliko ya kifungu cha 14 cha sheria ya sukari.
Hata hivyo, shauri hilo ambalo linasikikizwa na Jaji Dk Angelo Rumisha, limesikilizwa kwa Msajili Mahakama hiyo, baada ya Jaji Rumisha kuwa na udhuru.
Awali, wakili wa Serikali Mkuu, Hangi Chang’a ambaye anawakilisha wajibu maombi katika shauri hilo, ambao ni Waziri wa Kilimo na Mwanasheri Mkuu wa Serikali, alidia kuwa shauri hilo limeitwa kwa ajili ya usikilizwaji na wao tayari wameshawasilisha majibu yao tangu Septemba 10, 2024.
“Kama ambavyo Mahakama ilituelekeza tulete majibu yetu kwa wakati, tumefanya hivyo na tumewapatia wenzetu majibu yetu na shauri hili lilipangwa leo kwa ajili ya usikilozwaji,” amedai wakili Chang’a.
Chang’a baada ya kueleza hayo, kiongozi wa jopo la mawakili sita wanao wanatetewa wakulima hao, Dk Rugemeleza Nshala amedai nyaraka hizo wao zimewafikia Septemba 12, 2024.
Dk Nshala amedai kutoka na muda kuwa mdogo walishindwa kuwapata kwa wakati wakulima hao kwa kuwa wapo Kilombero.
Dk Nshala amedai baada ya kupema majibu ya maombi hayo wameona kuna vitu katika maombi hayo ambayo wanatakiwa kujibiwa, hivyo wanaona wapewe muda ili waweze kuandaa majibu na kuwasilisha majibu yao.
“Mheshimwa Msajili, kama unavyoona wateja wetu wapo Kilombero, hivyo ilikuwa ni ngumu kuwapata hadi leo hii labda tunaweza kuwaeleza haya majibu waliyotupa wenzetu, hivyo kutokana na hali hii tuaomba mahakama ituongezee siku tano mbele ili tuweze kuleta majibu,” amedai Dk Nshala.
Baada ya kuwasilisha maombi hayo, Msajili Mushi amewauliza wajibu maombi kuhusiana na ombi lililowasilishwa na Dk Nshala.
Hata hivyo, wakili Chang’a alidai kuwa hana pingamizi dhidi ya ombi hilo.
“Mheshimiwa Msajili, kwa ajili ya kutenda haki, sisi hatuna pingamizi juu ya ombi hilo,” amedai Chang’a.
Msajili Mushi baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 23, 2024, saa 3:30 asubuhi kwa ajili ya usikilizwaji na amewataka upande wa waleta maombi wawe wamewasilisha majibu ya nyongeza.
Siku hiyo, shauri hilo litaitwa kwa ajili ya usikilizwaji iwapo shauri hilo lina uhalali na halina dosari za kiseria au laa.
Baada ya kusikilizwa shauri hilo kama litakuwa halina dosari za kisheria, jalada hilo litahamia kwa Jaji Kiongozi na kisha kupangiwa majaji watatu ambao wataanza kulisikiliza.
Mbali na Dk Nshala, ambaye ni rais mstaafu wa TLS, mawakili wengine wanawatetea wakulima hao ni Mpale Mpoki, John Seka ambaye pia mi rais mstaafu wa TLS, rais wa sasa wa TLS, Boniface Mwabukusi, Ferdinand Makore na Edson Kilatu na Paul Kisabo.
Katika maombi hayo, wakulima hao wanapinga mabadiliko yaliyofanywa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye kifungu cha anadai kifungu hicho kinabadili Mamlaka ya kuagiza sukari ya akiba kutoka kwa wazalishaji ambao wakati wa uongozi uliopita, ziliagizwa zifanye na kampuni ya uzalishaji sukari ya wazalendo wa Tanzania.
Mzigowandevu pamoja na mambo mengine anadaiwa kuwa mabadiliko hayo yanaipa mamlaka kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ya uagizaji wa sukari.
Amedai kitendo hicho kitazuia au kitafanya ugumu wa mazao yao ya miwa kutouzika katika viwanda vya miwa.
Kwa mara ya kwanza, shauri hilo lilitajwa Agost 28, 2024