Dar es Salaam. Mahakama Kuu, Masjala ya Dar es Salaam, imetupilia mbali ombi lililowasilishwa na Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina la kuomba Mahakama hiyo imruhusu awasilishe majibu ya nyongeza katika kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na mwanasiasa huyo dhidi ya Waziri wa Kilimo, Waziri wa Fedha pamoja na taasisi tano, zikiwemo kampuni.
Uamuzi huo umetolewa leo Jumatano Septemba 18, 2024 na Jaji Arnold Kirekiano anayesikiliza shauri hilo, baada ya kukubaliana na mapingamzi yaliyowekwa na Serikali pamoja wajibu maombi wengine walioomba Mahakama hiyo isitoe nafasi hiyo kwa waleta maombi (Mpina) kuwasilisha mahakamani hapo majibu ya nyongeza.
“Nimekataa ombi la waleta maombi mahakamani hapa, ambao walikuwa wanaiomba Mahakama hii iwaruhusu wawasilishe majibu ya ziada, baada ya kupokea majibu kutoka kwa wajibu maombi,” amesema Jaji Kirekiano.
Mpina amefungua shauri hilo la kikatiba namba 18383/2024, akipinga mambo kadhaa, ikiwemo uamuzi wa Waziri wa Kilimo kutoa vibali vya ununuzi wa sukari kupitia Bodi ya Sukari kwa kampuni ambazo hazimiliki viwanda vya sukari wala sukari.
Chimboko la ombi hilo linatokana na kiongozi wa jopo la mawakili watano wanaomtetea Mpina, Dk Rugemeleza Nshala kuomba waruhusiwe na Mahakama hiyo kuleta majibu ya nyongeza baada ya wajibu maombi kuwasilisha majibu yao.
Dk Nshala alidai shauri hilo lilitwa kwa ajili ya usikilizwaji wa hatua ya awali, lakini wanaomba kuwasilisha hoja kuwa waleta maombi ambao ni Serikali na kampuni nyingine wamewasilisha majibu yao ambayo baadhi yamebua hoja mpya.
Dk Nshala amedai kutokana majibu ya wajibu maombi waliyopewa, anaomba Mahakama iwape nafasi ya kuzipitia nyaraka hizo, kisha kuwasilisha majibu ya nyongeza mahakamani hapo ili kesi hiyo itakapofikia hatua ya usikilizwaji kwa hatua ya awali, yale yanayobishaniwa kiushahidi yawe yamekwisha kamilika.
Wakili Nshala baada ya kuwasilisha ombi hilo, Serikali pamoja wajibu maombi wengine walipinga ombi la Mpina la kuwasilisha majibu ya nyongeza.
Hali hiyo ilisababisha kuwepo kwa ubishani wa kisheria kwa muda, huku pande zote zikijenga hoja zao.
Dk Nshala amedai upande wa Serikali waliwasilisha majibu yao Septemba 6, 2024, lakini baadhi ya kampuni na taasisi ambao ni wajibu maombi waliwasilisha majibu yao jana, hivyo kutokana na kucheleweshewa majibu hao wamepitia na kuona kuwa kuna haja ya kuwasilisha majibu ya nyongeza mahakamani hapo.
Wakili Nshala baada ya kueleza hayo, Wakili wa Serikali Mkuu, kutoka Ofisi ya Wakili wa Serikali, Hangi Chang’a alipinga ombi hilo akiomba Mahakama lisikubaliana na ombi la Dk Nshala.
Chang’a ambaye anayewatete, mjibu maombi namba moja(Waziri wa Kilimo), namba mbili( Bodi ya Sukari), namba sita(Waziri wa Fedha), namba saba( Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato nchini –TRA) Pamoja na namba nane ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali- AG, alidai kwenye mashauri ya kikatiba kuna utaratibu wake, hivyo lazima muombaji afuate utaratibu.
“Kwa kawaida kuna utaratibu na utaratibu huo ni kwamba unapokuwa una mashauri ya kikatiba, huwa kuna sheria ambazo zinasimamia uendeshaji wa mashauri haya kuanzia kwenye kuandaa nyaraka za kuwasilisha mahakamani mpaka kwenye usikilizwaji wa mashauri hayo mahakamani,” amedai wakili Chang’a na kuongeza
“Sisi upande wa Serikali tunapinga upande wa waleta maombi kuruhusiwa na Mahakama hii kuleta majibu ya nyongeza,” amedai wakili Chang’a.
Wakili Chang’a amedai kinachowaongoza mahakamani ni sheria na sheria imekataa kuhusu habari ya kuwasilisha majibu ya nyongeza mahakamani.
Amedai upande wa waleta maombi walikuwa wanaishawishi Mahakama kuwa sheria inayosimamia uendeshaji wa mashauri ya kikatiba haijatoa na kuelezea utaratibu wa kuwasilisha majibu ya nyongeza mahakamani.
Kwa upande wake, wakili Dayness Mkoko anayeitetea kampuni ya Itel East Africa Limited na Zenj General Merchandize, aliunga mkono pingamizi liliwasilisha na Serikali la kutaka Mahakama isimpe nafasi Mpina ya kuwasilisha majibu ya nyongeza.
Vile vile kwa upande wa wakili Thobias Laizer anayeitetea kampuni ya Yasser Provision Store Ltd, naye aliungana na upande wa Serikali kupinga ombi la Mpina.
Jaji Arnold Kirekiano, baada ya kusikiliza hoja za pande zote alitoa uamuzi wa kutupilia mbali ombi la Mpina na badala yake alielekeza kesi hiyo ianze kusikilizwa.
Baada ya kueleza hayo, Jaji Kirekiano aliahirisha shauri hilo hadi Oktoba mosi, 2024 saa 3:00 asubuhi, ambapo kesi hiyo itaitwa kwa ajili ya usikilizwaji wa uhalali wa shauri hilo kuwepo mahakamani au laa.
Katika shauri hilo, mbunge huyo anapinga uamuzi wa Waziri wa Kilimo kutoa vibali vya ununuzi wa sukari kupitia Bodi ya Sukari kwa kampuni ambazo hazimiliki viwanda vya sukari wala sukari.
Pia, anapinga Waziri wa Fedha kuruhusu Kamisha wa Mamlaka ya Mapato (TRA) kuamuru kampuni za vocha kuingiza sukari nchini bila kulipa kodi na kupelekea Serikali kupoteza mapato ya zaidi ya Sh1.548 bilioni.
Vile vile, amezishtaki kampuni za sukari kwa kukubali kuingiza sukari na kukubali kupewa msamaha wa kodi.
Mbali na Waziri wa Kilimo, wajibu maombi wengine ni Bodi ya Sukari, Kampuni ya Itel East Africa Limited na kampuni ya Yasser Provision Store Ltd
Nyingine ni Zenj General Merchandize, Waziri wa Fedha, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Mbali na Dk Nshala, mawakili wengine waliomtetea leo Mpina ni John Seka ambaye pia ni rais mstaafu wa TLS, Ferdinand Makore na Edson Kilatu na Fredrick Masaki.
Kwa mara ya kwanza shauri hilo lilitajwa mahakamani hapo Agosti 28, 2024.