Mashujaa ni mapigo na mwendo tu Ligi Kuu Bara

MASHUJAA wana kauli mbiu yao ya ‘Mapigo na Mwendo’ na hadi sasa Ligi Kuu Bara ikiwa raundi ya nne kikosi hicho kipo nafasi ya pili katika msimamo na mmoja wa makipa wa timu hiyo, Erick Johora amefichua kuwa presha waliyoanza nayo imeondoka baada ya kugawa dozi zilizowaongezea mzuka.

Mashujaa imevuna pointi saba katika mechi tatu, ikishinda mbili na kutoka sare moja, ikiwa nyuma ya vinara Singida Black Stars iliyocheza mechi nne na kushinda zote ikikusanya pointi 12, na Johora aliyewahi kuzidakia Yanga na Geita Gold, alisema pointi hizo zimewapa ari ya kujiamini katika ligi.

Kipa huyo aliyewahi kusugulishwa benchi akiwa Yanga kutokana na viwango vya Djigui Diarra, Metacha Mnata na Aboutwalib Mshery, aliliambia Mwanaspoti kuwa pointi saba walizokusanya Mashujaa katika mechi tatu za ligi zinawafanya kuanza kwa kujiamini na kwamba wataendeleza  kauli mbiu ya Mapigo na Mwendo kwa mechi zijazo kwani wameanza kuchangamka zaidi kuliko msimu uliopita.

Johora aliyesaliwa na Yanga 2021 akitokea Aigle Noir ya Burundi, alisema kocha wa timu hiyo, Abdallah Mohamed ‘Baresi’ hana mzaha kwenye kazi yake kwani kila mchezaji anayepafomu vizuri mazoezini ndiyo atakayepewa nafasi ya kucheza.

“Tulikuwa na presha kubwa ukiangalia mashabiki muda mrefu hawakushuhudia timu ikifanya vizuri. Kwa hiyo tulianza kwa hekaheka lakini matokeo mazuri tuliyoanza nayo kidogo yametupunguzia,” alisema Johora na kuongeza:

“Kwa Baresi hakuna kipa mzuri wala mwenye uzoefu kama huonyeshi kitu mazoezini basi ujue kwenye mechi imekula kwako hivyo tunapambana kuhakikisha tunapata nafasi ya kucheza.”

Mashujaa imecheza mechi tatu dhidi ya Dodoma Jiji iliposhinda bao 1-0 nyumbani, sare ya 0-0 na Tanzania Prisons na kushinda bao 1-0 ugenini dhidi ya Coastal Union ikikaa nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi.

Kwenye mechi hizo tatu Baresi alianza na Munthary na Lameck Kanyonga akianzia benchi huku Johora akikosekana kwenye kikosi hicho.

Related Posts