Mauaji ya familia yatikisa Dodoma

Dodoma. Katika kipindi cha takribani wiki tatu, Wilaya ya Dodoma imeshuhudia matukio ya kutisha ya uvunjifu wa amani baada ya familia tatu kuvamiwa nyumbani na kushambuliwa na watu wasiojulikana.

Mashambulizi haya yaliyotokea kati ya Agosti 28, 2024 na Septemba 16, yamesababisha watu sita kupoteza maisha, huku wengine wanne wakijeruhiwa.

Katika baadhi ya matukio hayo yaliyotokea usiku, wahusika walichoma moto miili ya waliowaua, hali iliyozua hofu na simanzi miongoni mwa wananchi.

Mbali ya hilo, hakuna kilichochukuliwa ndani ya nyumba baada ya mauaji hayo.

Hadi sasa polisi wanaendelea na uchunguzi wa matukio hayo kuwabaini waliotekeleza mauaji hayo.

Matukio hayo yaliyozua hofu miongoni mwa wananchi, huku baadhi ya mashirika ya haki za binadamu yakijitokeza kulaani la kwanza lilitokea usiku wa kuamkia Agosti 28, katika Mtaa wa Mbuyuni Kata ya Kizota wilayani Dodoma.

Katika tukio hilo, Michael Richard (36) aliuawa, huku mkewe Agnes Eliah na wanawe Ezra, Witness na Ephrahim Michael wakijeruhiwa na kulazwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

Hilo likiwa bado halijasahaulika, usiku wa kuamkia Septemba 6, mauaji yalitokea kwenye Mtaa wa Muungano A, Kata ya Mkonze.

Mwamvita Mwakibasi (33) na mtoto wake, Salma Ramadhan (13), waliuawa na watu wasijulikana katika tukio hilo, pia walifanyiwa vitendo vya ukatili.

Mbali ya hilo, Septemba 16, katika Mtaa wa Segu Bwawani, Kata ya Nala, Milcah Robert (12), mhitimu wa darasa la saba mwaka huu katika Shule ya Msingi Chilohoni na Mkazi wa Mailimbili jijini Dodoma, Fatuma Mohamed (20) waligundulika kuuawa ndani ya nyumba.

Katika tukio hilo, mtumishi wa ndani Micky anayekadiriwa kuwa na miaka 16 pia aliuawa, huku mama wa familia hiyo, Lusajo Mwasonge (40) akijeruhiwa na akulazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

Wananchi katika maeneo hayo wanaeleza kuingiwa hofu, baadhi wakichukua tahadhari, wakiomba Serikali kufanya uchunguzi kubaini wahusika na kudhibiti matukio hayo.

Wakizungumza na Mwananchi Septemba 17, 2024, baadhi ya wananchi wamesema mauaji hayo yanatishia usalama wao kwa kuwa hawana uhakika hata wanapokuwa ndani ya nyumba zao.

“Unakimbilia wapi kama wauaji wanakuja kukufuata nyumbani kwako ukiwa umelala na kukuua, na cha kushangaza hakuna vitu wanavyochukua na katika matukio yote majirani hawasikii kelele,” amesema mkazi wa Mailimbili, Mwanaisha Ally.

Mkazi wa Mbuyuni A, Kata ya Kizota, Clement Maganga ameiomba Serikali kuangalia kwa jicho la karibu mauaji hayo kwa sababu yamekuwa yakiacha makovu kwa kuwaumiza watu wengi kwa kiwango kikubwa.

“Hatuna amani, matukio yamekuwa mengi. Jeshi la Polisi na Serikali liangalie suala hili, tunaumia,” amesema.

Ameomba Jeshi la Polisi iwapo linakamata watu kwa tuhuma za mauaji basi liwachukulie hatua za kisheria na kama kuhukumiwa wahukumiwe na siyo waliofanya matukio kama hayo kuonekana baada ya muda mfupi mitaani.

Viongozi wa dini      

Askofu wa Kanisa la The Gospel Special Message Ministry (Gome), Majid Salim Ally amesema yamekuwapo matukio ya mauaji na mengine ya watu kupotea, kutekwa na watoto kuibiwa, hivyo mamlaka zinazohusika na usalama wa raia, zifanye kazi kukabiliana nayo.

Amedai kuna kulegalega kwa Jeshi la Polisi katika ufuatiliaji wa matukio hayo, akihoji ni kwa nini watuhumiwa wa matukio ya mauaji hawakamatwi.

Askofu Ally amesema anaamini Serikali ina uwezo wa kutosha wa kufuatilia matukio hadi watu wakapatikana.

“Ninaomba Serikali ilishughulikie hili, ninafahamu Serikali ikiamua kulifanyia kazi mambo haya yatakwisha,” amesema Askofu Ally.

Amewataka wananchi kushirikiana na Serikali kutoa taarifa za uhalifu wanapoona mienendo isiyofaa katika jamii.

Amesema matukio ya mauaji ya mamna hiyo yamekuwa yakitokea uchaguzi unapokaribia baadhi yakihusishwa na masuala ya ushirikina.

Askofu Ally amewataka viongozi wa dini kushirikiana na Serikali kukemea vitendo hivyo na kuwafundisha watu wanaoongoza kuwa na maadili mema ili kuliponya Taifa na maovu.

Sheikh wa Mkoa wa Dodoma, Alhaj Mustafa Shaban amesema ni lazima kumuomba Mungu na kuwahubiria watu watende matendo yaliyo mema.

“Kwa hali ilivyo sasa, imefika wakati kila kiongozi kulivalia buti jambo hili, tuhakikishe tunashirikiana na viongozi wa mitaa, mabalozi waliopewa dhamana na polisi kuwabaini wahalifu,” amesema Sheikh Shaban.

Amewataka watu kutokubali kuishi na watu wasioelewa wamefikaje walipo na kuwaripoti kwenye vyombo vya ulinzi na usalama wenye mienendo mibaya hata kama ni ndugu wa karibu.

Amesema vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi wa dini na wasimamizi katika ngazi ya Serikali watakaposimama katika nafasi zao kukemea masuala hayo itawezesha kukabiliana na uhalifu huo.

Sheikh Shaban amesema kufanyike semina elekezi kwa raia kueleza madhara na dhambi zinazopatikana kwa watu kujidhuru au kuwadhuru wengine.

“Inawezekana wanajua lakini imani bado haijakita katika nafsi zao. Mwisho kabisa kama familia tuhakikishe tunahudhuria katika nyumba za ibada,” amesema Sheikh Shaban.

Amewataka wanaotilia shaka familia, watoto na wenza wao, kuripoti kwa vyombo vya ulinzi na usalama kwa ajili ya uchunguzi ili kukomesha mauaji.

“Umefika wakati wa kuweka huruma pembeni, tuwabaini wahalifu, hata kama wanatokana na familia zetu tuwataje,” amesema Sheikh Shaban.

Kuhusu sababu za mauaji hayo, Sheikh Shaban amesema ni wananchi kutowafichua wahalifu, visasi, imani za kishirikina, chuki binafsi na masuala ya kisiasa.

“Mtu anaweza kulifanya jambo hilo kwa sababu mtu huyu anakuja juu zaidi, pengine tuko naye ndani ya chama kimoja (cha siasa), inawezekana katwaa nafasi yangu basi unatumika uhalifu kumharibia,” amesema Sheikh Shaban.

Kamishna Mwandamizi Msaidizi wa Jeshi la Polisi mstaafu, Jamal Rwambow amesema mahali popote ambako uhalifu umekithiri ni muhimu Jeshi la Polisi kushirikiana na wananchi wa eneo husika kuukabili.

Amesema uhalifu ni zao la jamii kwa sababu wahalifu wanaishi katika jamii, na itakapofika mahali ikikataa uhalifu basi kazi ya polisi itakuwa rahisi.

“Kwa hiyo ni lazima jamii ishirikiane na Jeshi la Polisi katika kuwafichua wahalifu kwa sababu wanaishi nao, wanawajua, hiyo kitu inaweza kumaliza uhalifu mahala popote siyo Dodoma tu. Lakini wakati fulani wananchi wanasita kushirikiana na Polisi wa sehemu husika kwa sababu mbalimbali, ikiwemo kutokuwa rafiki kwao,” amesema Rwambow.

Amesema sababu nyingine ya wananchi kuacha kushirikiana na polisi, ni jeshi hilo kutofungua milango ya mazungumzo na majadiliano na watu wa eneo husika kuhusu masuala ya usalama.

“Kama ndiyo hivyo, ni lazima polisi kujisahihisha ili kupata ushirikiano kutoka kwa wananchi na hapo ndipo watakapofanikiwa,” amesema.

Rwambow ametoa mfano akiwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza mwaka 2008 hadi 2010 alimaliza tatizo la mauaji ya watu wenye ualbino, akifichua mbinu aliyotumia ni kuwashirikisha wananchi.

Amesema wananchi waliwaamini polisi chini ya uongozi wake, hivyo walipata taarifa nyingi juu ya wahalifu wa makosa ya aina hiyo na kuchukua hatua iliyowezesha kukomesha mauaji ya watu wenye ualibino.

“Kwangu tatizo litakoma pale wananchi watakapokataa uhalifu na kushirikiana na polisi katika kupambana na hali hiyo,” amesema Rwambow.

Akizungumzia kuhusu mauaji kufanyika na wahusika kutochukua chochote, Rwambow amesema kila tukio linakuwa na sababu yake, hivyo upelelezi ndiyo utaonyesha kwa nini tukio husika limetokea.

Hata hivyo, amesema ni vizuri kuzuia uhalifu kabla ya kutokea na kama umetokea, juhudi kubwa zielekezwe katika kuwatafuta wahusika na kuwafikisha mahakamani ili makosa kama hayo yasitokee.

“Lakini wananchi ndiyo nyenzo kubwa ya kukomesha hayo (mauaji), polisi hawapo kila mahali,  lakini wananchi wako kila mahali inawezekana mtu anatoka katika nyumba ya kupanga anaenda kufanya uhalifu na kurudi. Wapangaji wapo na nyendo zake wanazitilia shaka ni vyema kuliarifu Jeshi la Polisi lichukue hatua,” amesema.

Rwambow amesema baadhi ya watu hufanya matukio hayo kulipiza kisasi au kutokana na kudhulumiana. Hata hivyo, amesema uhalifu ni uhalifu, haupaswi kuvumiliwa kwa namna yoyote ile.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Anania Amo amesema wana mkakati wa kupambana na vitendo hivyo ikiwa ni pamoja na kusogeza vituo vya polisi hadi ngazi ya kata.

“Hawa wanatoa elimu huko wanapoishi, lengo mojawapo la kupambana na uhalifu ni kushuka chini ili wananchi wajue uhalifu na kuuchukia waweze kutoa taarifa,” amesema Kaimu Kamanda Amo.

Amesema wajibu wa kulinda usalama ni kwa kila mmoja, na kwamba Jeshi la Polisi linasaidia kukabiliana na uhalifu, lakini mwananchi mmoja mmoja anao wajibu wa kusaidiana na Jeshi hilo.

Amesema Jeshi hilo limekuwa likifanya operesheni kulingana na matukio yanayojitokeza.

Kaimu Kamanda amesema operesheni hazilengi kuumiza watu, bali kumpata mhalifu aliyetenda uhalifu.

Related Posts