Mchengerwa, Makonda wanusa ubadhirifu Samia Girls, DED akalia kuti kavu

Longido. Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda ameibua tuhuma za ubadhirifu wa zaidi ya Sh1.3 bilioni zilizotumika katika utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Samia iliyopo Wilaya ya Longido mkoani Arusha.

Makonda ameibua tuhuma hizo leo Jumatano Septemba 18, 2024 mbele ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais -Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa, aliyetembelea na kukagua miradi mbalimbali wilayani humo.

Kwa mujibu wa Makonda, aliagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru) Mkoa wa Arusha kufanya uchunguzi na baada ya kupokea ripoti, amebaini ubadhirifu wa zaidi ya Sh1.3 bilioni zilizotumika katika ujenzi wa shule hiyo.

Kufuatia tuhuma hizo, Waziri Mchengerwa amemuonya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Nassoro Shemzigwa kuacha kumdanganya kuhusu mradi huo na kumpa muda hadi Novemba Mosi 2024, uwe umekamilika.

Hadi sasa mradi huo ulioanza kutekelezwa Septemba 30, 2023 ulipaswa kukamilika mwisho wa mwezi huu na unatekelezwa kwa kutumia fedha za Serikali Kuu chini ya Mpango wa Kuboresha Elimu ya Sekondari Tanzania (SEQUIP), kwa kutumia ‘force account’ na kwa sasa umefikia asilimia 90.5.

Akizungumzia mradi huo alipowahutubia  wananchi na watendaji wa halmashauri hiyo, Waziri Mchengerwa amesema Serikali imetoa Sh108 bilioni.

Amesema kila mkoa umepokea Sh4.6 bilioni, lakini anasikitika kuona mpaka sasa ujenzi wa  bwalo haujakamilika na ameagiza ufanyike  usiku na mchana hadi ukamilike.

“Nasikitika kuona mradi haujakamilika na fedha zote zimetolewa, inaonekana kuna watu wanaochomoa chomoa hela. Mniletee hiyo ripoti haraka naisubiri, ukigusa fedha utawajibika,” amesema Waziri Mchengerwa.

Amesema ameshuhudia mwenyewe ujenzi wa bwalo na baadhi ya madarasa ukiwa haujakamilika.

Amesema hawatamuonea mtu huruma hasa yule atakayebainika anatafuna senti hata tano za mradi hiyo katika mikoa yote 26.

Waziri huyo amesema watendaji wana wajibu wa kuhakikisha wanatimiza majukumu yao ili kuwaletea wananchi maendeleo badala ya kuleta ujanja ujanja kwenye fedha za miradi zinazotolewa na Serikali.

Katika hatua nyingine, Mchengerwa amekerwa na kitendo cha Mkurugenzi Nassoro kumdanganya kuhusu tarehe ya kukamilika kwa mradi huo na kumweleza kuwa anampa onyo la mwisho.

“Mkurugenzi pale ndani ulinidanganya, ninakupa nafasi ya mwisho ya kujirekebisha, mimi ni waziri wa tofauti na usirudie tena wewe na wasaidizi wako ila msamaha huu hautahusiana na ripoti ya Takukuru,” amesema.

“Nakupa hadi Novemba Mosi, 2024 mrdai huu ukamilike, hakuna nyongeza hata ya siku moja kwa sababu tulikubaliana hadi Septemba 30, uwe imekamilika, la sivyo tutachukua hatua,” amesema waziri huyo.

Makonda alivyonusa ufisadi

Awali Makonda alimweleza waziri kuwa alipoutembelea mradi huo na kuhoji maswali, majibu aliyopewa yalimpa utata na baada ya kumhoji anayeusimamia, akaona ni bora anuagize Kamanda wa Takukuru auchunguze na kumpatia taarifa zake.

Amesema baada ya kukabidhiwa taarifa hiyo leo na kuipitia, amebaini ubadhirifu huo na kwa mujibu wa taarifa hiyo, Takukuru wamebaini zaidi ya Sh1 bilioni zimetumika bila kupitia mfumo wa kielektroniki (EFD) na malipo hayo hayana uthibitisho.

“Lakini pia imegundulika zaidi ya Sh300 milioni zimelipwa hazina nyaraka yoyote ya kuthibitisha zimelipwaje na zimeenda kwa nani, lakini pia tumegundua zaidi ya ongezeko la asilimia 71 ya fedha iliyotolewa kwenda kulipa wazabuni iliongezwa kinyume na utaratibu, hayo ni mambo ambayo nimepitia tu kwa ufupi,” amesema Makonda.

Aliposoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, mkuu wa shule hiyo, Esther Kobelo amesema  mpaka sasa ujenzi umefikia asilimia 90.5 na Sh3 bilioni zimeshatumika.

“Na tayari Sh4.6 bilioni zilishatolewa na Serikali  kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa bwalo na miundombinu na utekelezaji utaanza baada ya utaratibu wa manunuzi kukamilika,” amesema Kobelo.

Mkuu wa Wilaya ya Longido, Salum Kali amesema katika wilaya hiyo shule zote za Sekondari ni za bweni.

“Tumefanya hivyo kwa lengo la kuwasaidia wanafunzi kupata elimu katika mazingira salama zaidi,” amesema mkuu huyo wa wilaya.

Katika hatua nyingine, Waziri Mchengerwa ameagiza wakuu wote wa mikoa kuimarisha ulinzi na usalama hasa ile iliyoko mipakani, inapaswa kudhibiti magonjwa ya milipuko ukiwamo wa Homa ya nyani usiingie nchini.

Amesema ni muhimu maeneo ya mipakani yakaimarisha ulinzi ili kuhakikisha hakuna mgonjwa anayeingia nchini.

“Hakikisheni mipaka yetu hasa wa Kituo cha Forodha cha Pamoja (OSBP) cha Namanga, hakikisheni kinakuwa salama,” amesema Mchengerwa.

Related Posts