Kigoma. Meli ya mafuta ya Mv Sangara iliyokuwa ikifanya safari kutoka mkoani Kigoma kwenda Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), inatarajia kuanza safari zake rasmi Oktoba, 2024 baada ya kusimama kufanya kazi tangu mwaka 2020.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Septemba 18, 2024, msimamizi wa mradi wa ukaratabati wa meli hiyo ya mafuta, mhandisi Devid Jenga amesema ukarabati unaofanywa umefikia asilimia 96.
“Ukarabati ulipangwa kufanyika kwa miaka miwili na unagharimu Sh8.4 bilioni,” amesema msimamizi huyo.
Amesema kwa sasa hatua zilizofikiwa katika ukarabati huo ni za mwisho, ikiwemo kukagua na kufanya majaribio ya mashine zilizofungwa na kukabidhiwa rasmi kwa Serikali kwa ajili ya kuanza kazi Oktoba (mwezi ujao).
Jenga amesema meli hiyo yenye uwezo wa kubeba tani 380 za mafuta, sawa na magari 11, imefanyiwa ukarabati mkubwa kwa kutoa mifumo yote ya zamani na kuwekwa mipya na ya kisasa.
“Tumebadilisha mifumo yote ya zamani na kuweka mifumo ya kisasa kuanzia kwenye injini, pampu na mfumo wa uongozaji wa meli, kwa sasa unaweza kupeleka mzigo wa mafuta DRC na kugeuza siku hiyo hiyo tofauti na awali,” amesema Jenga.
Naye Kaimu Meneja Tawi wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), Kigoma Mtembelo amesema kukamilika kwa ukarabati wa meli ya Mt Sangara kutapunguza muda wa kusafirisha mafuta hayo kwenda nchi za jirani kutoka saa nane hadi saa tatu kwa siku.
“Pamoja na kupungua kwa saa za kusafirisha mafuta, pia gharama zitapungua za usafirishaji baada ya timu ya masoko kufika na kufanya utafiti pamoja na kujadiliana na wadau kupata bei elekezi, ili kila mteja aweze kuimudu,” amesema Mtembelo.
Amesema; “Meli hii kongwe ina faida kubwa, kwani inahakikisha lita za mafuta za mteja zinafika bila kupungua, tofauti na meli nyingine zinazobeba mafuta. Hii ndiyo sababu watu wengi wanapenda kuitumia kwa ajili ya kusafirisha mizigo yao kwa usalama na uhakika zaidi na ilivyosimama hivi, wengi wanaumia sana.”
Nahodha wa meli ya hiyo, Titus Mnyanyi amesema kwa sasa ipo tayari kuingia kazini baada ya ukarabati mkubwa uliofanyika.
Amesema meli hiyo mitambo yake ilikuwa imechoka na kuwachukua muda mrefu kusafiri na kupakua mzigo. Ilikuwa inatumia zaidi ya saa 20 kupakua mzigo, lakini kutokana na ukarabati huo, sasa itatumia saa nane.