Arusha. Msako unaendelea kumtafuta mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Bagara, Joel Johannes (14) aliyepotea walipokwenda Mlima Kwaraa kwa ziara ya masomo.
Katika kuongeza nguvu, mgambo 60 wameungana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama na wananchi kumsaka mwanafunzi huyo aliyepotea tangu Jumamosi ya Septemba 14, 2024.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Septemba 18, 2024, Katibu Tawala Wilaya ya Babati, Halfan Matupula amesema uchunguzi unaendelea na hadi sasa bado hawajapata chanzo cha uhakika kama amepotelea msituni au ametoroka.
Amesema msako unafanyika mlimani na mitaani kwenye hosteli za wanafunzi.
Matupula amesema mbiu imepigwa kwa wananchi waishio pembezoni mwa mlima huo, ambao wanashiriki kumtafuta.
Joel na wanafunzi wenzake 102, walikwenda ziara ya masomo katika mlima huo na walipokuwa wakirejea mwanafunzi hakuonekana.
Matupula amesema kuanzia jana (Septemba 17) mgambo hao 60 kwa kushirikiana na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), Jeshi la Polisi na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya wameungana na wazazi na wananchi kumtafuta Joel.
“Uchunguzi unaendelea, ila mpaka sasa hatujapata chanzo cha uhakika kama amepotea au ametoroka, timu zinaendelea na kazi ya kutafuta kule msituni na wengine wanaendelea na uchunguzi.
“Tumeongeza nguvu, tuna askari, TFS, mgambo 60 na tumeenda wote mlimani kuanzia asubuhi jana (Septemba 17) ila hatujafanikiwa kumpata,” amesema.
Amesema kwa sababu mlima huo una maeneo mawili ya kutokea na kuna njia ya kutokea kijiji kingine upande wa pili, timu itaanzia huko kumtafuta.
“Leo tutaongeza nguvu pia, kwani hata sasa nguvu ipo ukiachia watu ambao wamepanda, huku lakini jamii yote inayopakana na mlima wameshapata taarifa na wameshapiga mbiu, moja kati ya vitu tunavyofanya kama mtoto aliteremka akawa kwenye nyumba za huku kwa wenzake,” amesema.
“Hapa yako mambo mawili, tunaweza kusema mtoto amepotea mlimani, lakini kumbe yupo amebaki kwenye maeneo huku ya wenzake. Pamoja na viongozi wa mitaa, mbiu imepigwa kwa ajili ya kupita nyumba kwa nyumba na maeneo ambayo kuna wanafunzi wamepanga wanaosoma Veta na maeneo mengine,” amesema.
Amesema, “yako maeneo kama hosteli za wanafunzi tupite kule nyumba kwa nyumba, ili tuone kwenye hizo nyumba nani amekaa na wanafunzi gani wako mle, ili kama tutaona kuna mwanafunzi ambaye yuko tofauti na taarifa tulizozitoa aondolewe kama atakuwa kwenye maeneo haya ya mtaani,” amesema.
Baba wa mtoto huyo, Johannes Mariki, amesema kuna ushirikiano mkubwa kutoka kwa vyombo vya ulinzi na usalama katika kumtafuta mtoto wake.
Mhifadhi Msaidizi wa TFS Wilaya ya Babati, Naomi Andrew amesema wameungana na wadau wengine kumtafuta mwanafunzi huyo.
Amesema wamejitahidi kuangalia kama watabahatika kumuona, ila hawajafanikiwa wala kuona dalili yoyote ya uwepo wake.
Mkuu wa shule hiyo, Emanuel Dahaye amesema kwa sasa uongozi wa shule hauwezi kuzungumza chochote hadi watakapompata mwanafunzi huyo.
“Bado suala hili liko chini ya kamati ya ulinzi na usalama ambao wanaendelea na uchunguzi, bado hatuwezi kusema kitu kwa sasa mpaka tutakapompata mwanafunzi huyo ndipo tunaweza kuzungumza na vyombo vya habari,” amesema.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Babati, Simon Mdee alisema janakuwa safari hiyo ya masomo ilihusisha wanafunzi 103, wakiwa na walimu na waongozaji wapanda mlima.
Alisema baada ya Joel kutopatikana taarifa zilitolewa polisi na kazi ya kumsaka ilianza.