Septemba 15, mwaka huu, Tanzania iliungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Demokrasia katika kipindi ambacho wanazuoni na ripoti mbalimbali zikionyesha dosari katika misingi ya demokrasia nchini.
Kwa mitazamo ya wanazuoni waliozungumza na Mwananchi, uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ndiyo ulikuwa ukomo wa safari ya demokrasia nchini, baada ya hapo, kushuhudiwa misingi ya kidemokrasia ikivunjwa.
Uongozi katika Serikali ya awamu ya tano, unatajwa kukiuka misingi ya kidemokrasia ikiwemo kuzuia mikutano ya hadhara kwa vyama vya upinzani, kudhibiti uhuru wa vyombo vya habari na kukiukwa kwa utawala wa sheria.
Hali iliyoshuhudiwa katika kipindi hicho iliendelea na demokrasia haikuwahi kutengamaa hadi sasa, kwa mujibu wa wanazuoni hao waliozungumza na gazeti hili.
Historia ya Tanzania katika safari ya demokrasia ilianza baada ya uhuru, mwaka 1961, wakati huo nchi ikiendeshwa chini ya mfumo wa chama kimoja cha Tanu na baadaye CCM hadi mwaka 1992 ulipoanzishwa mfumo wa vyama vingi.
Kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi kulifungua milango kwa vyama vya siasa kushiriki katika chaguzi na kutoa fursa kwa wananchi kushiriki katika kufanya uamuzi wa kisiasa kuhusu taifa lao.
Kuporomoka kwa viwango vya demokrasia nchini kunadhihirishwa kwenye Ripoti ya Freedom House ya mwaka 2023 iliyoipa Tanzania alama 32 kati ya 100 katika kipimo cha uhuru.
Katika utafiti huo, nchi hupimwa kulingana na uhuru wa kisiasa na kiraia na kwa mujibu wa takwimu hizo Tanzania imetafsiriwa kuwa nchi isiyo huru.
Hali hiyo inaashiria changamoto katika maeneo kama uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa kujieleza na uwazi wa uchaguzi.
Mbali na Freedom House, Ripoti ya Democracy Index ya The Economist Intelligence Unit (EIU) ya mwaka 2022, iliiorodhesha Tanzania kuwa nchi yenye utawala wa mabavu, ikiwa na alama 3.44 kati ya 10.
Hii ni ishara kuwa bado kuna vikwazo vinavyoathiri demokrasia ya nchi hasa katika ushirikishwaji wa kisiasa na utawala wa sheria.
Sambamba na ripoti hizo, mifano ya hivi karibuni nayo inaonyesha changamoto katika demokrasia, mathalan uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Katika uchaguzi huo, kuliibuka ukandamizaji wa wapinzani, udanganyifu katika kuhesabu kura na kuzuiliwa kwa wagombea wa upinzani kufanya kampeni zao kwa uhuru.
Kwa mujibu wa ripoti ya Tume ya Uchaguzi ya Tanzania (NEC) wakati huo, aliyeshinda uchaguzi huo ni Hayati Magufuli akipata asilimia 84 ya kura zote.
Hata hivyo, vyama vya upinzani kama Chadema na ACT Wazalendo vilipinga matokeo hayo vikidai uchaguzi haukuwa huru na wa haki.
Akizungumza na Mwananchi, mhadhiri wa sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Conrad Masabo anasema demokrasia ya Tanzania iliharibiwa tangu mwaka 2016.
Kuharibika kwake, Dk Masabo anasema kulitokana na uamuzi uliofanywa na Watanzania kuamini mtu na sio utaratibu na hilo lilifanyika tena mwaka 2021 alipoaminiwa mtu na sio mifumo.
“Tunachokipitia ni matokeo ya huo uamuzi wetu. Demokrasia kama haki nyingine hudaiwa na sio kuombwa, pia inapaswa kulindwa ili walioitoa wasiipokonye tena,” anasema.
Katika vipindi hivyo, Dk Masabo anasema Watanzania wote waliamini Hayati John Magufuli ni mkombozi na 2021 waliamini Rais Samia Suluhu Hassan atawakomboa, hadi kupigiwa chapuo na vyama vya upinzani.
Kwa mtazamo wa mwanazuoni huyo, kwa hali ilivyo hadhani kama maboresho yanawezekana.
Hata hivyo, anaeleza uwezekano upo katika mambo mawili ambayo ni kuja kwa kiongozi mwenye hisani aijenge demokrasia licha ya kuwa jambo hilo ni gumu kwa mfumo wa demokrasia ya vyama uliopo.
Jambo la pili, anasema wananchi wajiunge kuidai, kitu ambacho ni kigumu kwa vile raia wameamua kuwaachia wanasiasa jukumu hilo.
“Kuna uwezekano mkubwa wa kulipa thamani kubwa ili kurejea tulipokuwa mwaka 2015, swali ni nani wa kulipa gharama hii?” anahoji.
Dk Masabo anasema kinachoitesa Tanzania ni kwa sababu demokrasia yake ni ya vyama na sio ya raia, hivyo raia au wananchi wanaamini hawana wajibu wa kudai na kuilinda.
“Mafanikio ya Reject Financial Bill (kuondolewa kwa muswada wa fedha) ya Kenya ni kwa vile ilikuwa inaongozwa na kusimamiwa na raia na ndio maana baada ya vyama kuingia, malengo na mafanikio yamepotea,” anafafanua.
Mtazamo kama huo unatolewa pia na mwanazuoni mwingine, Profesa Mohamed Bakary anayesema kuna anguko kubwa la demokrasia linaloendelea kushuhudiwa nchini ukilinganisha na ilivyokuwa mwanzo.
Anasema Tanzania ilianza kuingia katika mfumo wa demokrasia kwa mguu wa kulia, lakini kwa kadri siku zinavyokwenda hali inakuwa mbaya zaidi.
Msingi wa hoja yake hiyo ni kile anachofafanua kwamba Tanzania ilianza kuiishi demokrasia baada ya kuruhusu mfumo wa vyama vingi na katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1995, ilishuhudiwa demokrasia ya hali ya juu.
Anasema hali ilikuwa hivyo hadi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, vyama vya upinzani vilishuhudiwa vikipata nafasi ya kuongeza katika ngazi ya mitaa, vijiji, vitongoji na hata majimbo.
“Ile hali iliashiria kuimarika na kuendelea kukua kwa demokrasia tangu mfumo wa vyama vingi ulipoanza,” anaeleza.
Anguko la demokrasia, anasema lilianza kushuhudiwa mwaka 2015, ule uhuru wa uchaguzi na mambo mengine yanayoijenga misingi ya demokrasia ilianza kuyeyuka.
Badala ya kusonga mbele, Profesa Bakary anasema Tanzania ilianza kurudi nyuma kidemokrasia hadi ulifika wakati idadi ya washindi wa vyama vya upinzani katika nafasi mbalimbali ziliporomoka.
“Hata matukio ya watu kupotea yanayoripotiwa sasa ni ishara ya kuonyesha kwamba tumerudi nyuma. Tulitarajia kama tungekuwa tumepiga hatua, haya matukio yangefanyiwa uchunguzi na watuhumiwa wangetangazwa hadharani na hatua zingechukuliwa,” anasema.
Lakini hali iliyopo sasa, mwanazuoni huyo anasema unakuta watu wanajichukulia sheria mkononi na uwajibikaji hauonekani.
“Kuna kurudi nyuma kwa kiwango cha kutisha na inaweza kuleta hatari ya demokrasia kusambaratika kabisa,” anasema.
Licha ya changamoto hizo, kuna fursa ya kuboresha hali ya demokrasia nchini. Mabadiliko yaliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan tangu alipoingia madarakani mwaka 2021 yanaonyesha matumaini.
Rais Samia ameonyesha utayari wa kufanya mageuzi katika maeneo kama uhuru wa vyombo vya habari na haki za kisiasa.
Serikali yake imeruhusu upya mikutano ya kisiasa ya vyama vya upinzani, hatua iliyopongezwa na viongozi wa kisiasa na wanaharakati wa haki za binadamu.
Pia, kumekuwa na jitihada za marekebisho ya Katiba. Wanaharakati wa haki za binadamu na vyama vya siasa wameendelea kusisitiza haja ya katiba mpya itakayoweka misingi imara ya haki za kiraia, usawa wa kisiasa, na uhuru wa vyombo vya habari.
Rais Samia ameonyesha utayari wa kufufua mjadala wa Katiba mpya na hii ni ishara ya matumaini kwa maendeleo ya demokrasia nchini.