Bunda. Miili ya watu watatu kati ya watano waliozama katika Ziwa Victoria, baada ya mtumbwi waliokuwa wakisafiria kupasuka imepatikana, hivyo kuhitimisha kazi ya utafutaji iliyodumu kwa takriban siku nne.
Kupatikana kwa miili hiyo kunafanya idadi ya watu waliofariki dunia kwenye ajali hiyo iliyotokea Septemba 15, 2024 kufikia sita na manusura 14.
Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dk Vicent Naano amesema akizungumza na Mwananchi leo Septemba 18, 2024 amesema mwili wa mwisho umepatikana leo asubuhi.
“Wote wametambuliwa na kuchukuliwa na ndugu zao na hivi sasa mwili wa mwisho nao ndio unaondolewa hapa na familia kwenda kuuzika,” amesema Dk Naano.
Amesema kutokana na msiba huo, Serikali imetoa ubani wa Sh100,000 kwa kila familia sambamba na usafiri kwa ajili ya kuzipeleka maiti hizo maeneo yaliyoamriwa na kila familia ikazikwe.
Mkuu huyo wa wilaya amesema tayari ameliagiza Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac), kufanya oparesheni ya kukamata vyombo vyote vya majini vinavyofanya shughuli zao kinyume cha utaratibu ndani ya wilaya hiyo.
“Haiwezekani kila mara tunakutana kutafuta watu waliokufa kutokana na ukiukwaji wa taratibu, kuanzia wiki ijayo Tasac watafanya oparesheni ya kuwakamata wote wanaofanya shughuli zao kinyume cha utaratibu, mfano wanaosafirisha abiria bila kuwa na jaketi okozi (life jacket) na mambo mengine,” amesema Naano.
Pia amepiga marufuku chombo chochote cha majini kufanya shughuli tofauti na usajili wake, huku akitolea mfano mtumbwi huo uliosababisha vifo vya watu hao sita.
“Huu mtumbwi ulikuwa mahsusi kwa shughuli za uvuvi na una uwezo wa kubeba wavuvi watano tu, lakini ulibadilishiwa matumzi na kusafirisha watu wengi kushinda uwezo wake,” amesema Naano.
Septemba 15, 2024 saa moja usiku, mtumbwi huo uliokuwa umebeba watu waliokuwa wakitoka kwenye harusi Kijiji cha Mwiruruma ulizama ziwani, ziwani wakati unaelekea katika kitongoji cha Bulomba katika kijiji cha Igundu.
Katika tukio hilo, watu 14 waliopolewa wakiwa hai na mwili mmoja kuopelewa, huku watu watano waliokuwa miongoni mwa waliokuwa kwenye mtumbwi huo wakikosekana.
Watu hao ambao wali0kuwa ndugu, jamaa na marafiki wa bwana harusi walikuwa wakirejea nyumbani kwa ajili ya maandalizi ya harusi kwa upande wa bwana harusi sherehe ambayo ilipangwa kufanyika Septemba 16, 2024 kijijini Igundu.
Mtumbwi huo uliopigwa na wimbi na kupasuka, kisha maji kujaa ndani kabla ya kubinuliwa na kuwamwaga watu waliokuwemo ziiwani ulikumbwa na na hali hiyo takriban kilomita 1.5 kabla ya kufika katika ufukwe wa kijiji cha Igundu.
Hilo ni tukio la pili kutokea ndani ya kipindi cha takriban miezi 14 ambapo Julai 30,2023 mitumbwi miwili ilizama na kuuwa watoto 14, wakiwepo wanafunzi 13 wa Shule ya Msingi Bulomba.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Igundu, Sumera Nyamkinda amesema agizo la mkuu wa wilaya linaoaswa kutekelezwa kwa wakati ili kunusuru maisha ya watu.
“Tumepoteza watu sita pia mwaka jana tulipoteza watoto 14 na chanzo kikubwa ni chombo kisichokuaa na sifa kutumika kusafirisha watu, ukaguzi ufanyike ili kuruhusu vyombo vyenye sifa kufanya shughuli za usafirishaji,” amesema Nyamkinda.
Mkazi wa Kijiji cha Igundu, Nyamisi Malima amesema wananchi pia wanatakiwa kuchukua tahadhara kuepuka ajali zisizokuwa za lazima.
“Hii mitumbwi huwa ni midogo sana, ingawa sitaki kulaumu lakini watu walitakiwa kuchukua tahadhari ni bora hata wangesombwa kwa awamu kuliko kujazana kwenye chombo kidogo hivyo,” amesema.